Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mswada Hijabu na ‘usafi’ kwa wanawake wa Iran waisikitisha OHCHR

Kuvaa hijabu hadharani ni lazima kwa wanawake nchini Iran.
© Unsplash/Hasan Almasi
Kuvaa hijabu hadharani ni lazima kwa wanawake nchini Iran.

Mswada Hijabu na ‘usafi’ kwa wanawake wa Iran waisikitisha OHCHR

Wanawake

Hatua ya Bunge la Iran kupitisha mswada mpya utakaowabana zaidi wanawake kuhusu uhuru wa miili yao na pia uvaaji wao hususani vazi la Hijab imepokelewa kwa masikitiko makubwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR.

Tunasikitika sana Bunge la Iran kupitisha Mswada mpya wa Usafi na Hijabu ambao unaongeza kwa kiasi kikubwa vifungo vya jela na faini ya kuwakandamiza wanawake na wasichana ambao hawatatii kanuni za lazima za uvaaji, imesema Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu kupitia kwa Msemaji wake Ravina Shamdasani alipozunguza na waandishi wa Habari jijini Geneva, Uswisi.  

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, ametuma ujumbe kwamba mswada huu wa kikatili unaopeperushwa waziwazi mbele ya uso wa sheria za kimataifa lazima usitishwe. 

Wale wanaopuuza kanuni kali ya mavazi ya Kiislamu ya kufunika kichwa na mavazi yanayoitwa ya heshima wako hatarini kukumbwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela, kuchapwa viboko pamoja na kutozwa faini ya hadi rial za Iran milioni 360 sawa na takribani dola za kimarekani 8,522.  

Kwa hatua mswada huu ulipofikia, kinachosubiriwa ni kupitishwa na Baraza la Uongozi linaloundwa na wazee 12 walioidhinishwa kikatiba ambao wana nguvu na ushawishi mkubwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

Chini ya sheria ya awali, kosa kama hilo lilibeba kifungo cha hadi miezi miwili jela, au faini ya hadi rial 500,000 za Iran sawa na takribani dola 11.84 za kimarekani.