Utu na ubinadamu wafaa kurejea tunapojadili wakimbizi: Türk

Umewadia wakati wa kurejesha na kuzingatia utu na ubinadamu tunapohusika na mjadala mkali unaoendelea kuhusu masuala ya wakimbizi. Ni wito uliotolewa na kamishina msaidizi wa ulinzi wa kimataifa katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.
Katika upande mmoja amesema kuna nuru iliyowahamasisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 193 kuunda mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi na kudhihirisha nini kinachoweza kufikiwa watu wanapoamua kuangalia suluhu ya muda mfupi na kuwa na lengo la pamoja. Ametolea mfano walioamua kukumbatia wakimbizi akisema
(SAUTI YA VOLKER TURK)
“Hususan katika bara la Afrika tumeshuhudia makundi ya wachache ambao awali hawakuwa na uraia wakipewa uraia na vitambulisho, jinsi gani wanawake wakimbizi wa ndani walivyoweza kujimudu tena na kuanza maisha mapya.”
Na katika upande mwingine wa shilingi Bwana Turk ameongelea juu ya matokeo ya mataifa kutumbukia katika shinikizo na kuacha kutekeleza majukumu yao na kuongeza
(SAUTI YA VOLKER TURK)
“kwa mfano watoto walipokuwa wakigonga vichwa ukutani kwa kukata tamaa baada ya kutenganishwa na wazazi wao, au wakati vijana wadogo waomba hifadhi walipojiua baada ya kushikiliwa na kunyanyaswa kwenye vituo vya uandikishaji bila kuwa na matumaini yoyote ya mustakabali wao, au wakati raia waliokimbia na kujikuta wamekwama mpakani na kunyimwa vibali vya kuingia.”
Amesisitiza kuwa dunia hivi sasa inakabiliwa na mmomonyoko wa kutoheshimu utu wa binadamu hasa ukizingatia kwamba vita na mateso vimewafungisha virago watu milioni 68.5 duniani na miongoni mwao milioni 25.4 ni wakimbizi.