Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu huru wa UN wataka Israel iwekewe vikwazo vya kuuziwa silaha

Nyumba ya makazi imesalia vifusi katika kitongoji cha Al-Shaboura cha Rafah ity kusini mwa Ukanda wa Gaza.
UN News/Ziad Taleb
Nyumba ya makazi imesalia vifusi katika kitongoji cha Al-Shaboura cha Rafah ity kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Wataalamu huru wa UN wataka Israel iwekewe vikwazo vya kuuziwa silaha

Amani na Usalama

Zaidi ya wataalam 30 huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mauzo ya silaha kwa Israel.

Katika taarifa yao iliyotolewa hii leo huko Geneva Uswisi wataalamu hayo  wameonya kwamba uhamisho wowote wa silaha au risasi kwa Israel ambazo zitatumika huko Gaza huenda ukakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.

“Nchi zote lazima 'zihakikishe kuheshimiwa' kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu kwa wahusika katika mzozo wa silaha, kama inavyotakiwa na Mikataba ya Geneva ya 1949 na sheria za kimila za kimataifa,” wamesema wataalam hao.

“Nchi lazima zijizuie ipasavyo kuhamisha silaha au risasi yoyote - au sehemu za silaha hizo - ikiwa zinatarajiwa, kutokana na ukweli au mifumo ya zamani ya tabia, kwamba zitatumika kukiuka sheria za kimataifa.”

Wataalamu hao wamekaribisha uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama ya rufaa nchini Uholanzi ambayo iliamuru Serikali kusitisha usafirishaji wa sehemu za ndege ya kivita ya F-35 kwenda Israel, wakitaja "hatari ya wazi" ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

Waliongeza kuwa hitaji la kuwekewa vikwazo vya silaha kwa Israel linaongezwa na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki mwezi uliopita kwamba kuna hatari ya kutokea mauaji ya kimbari huko Gaza.

Kundi la wataalamu waliotoa taarifa hiyo wote waliteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na wanahudumu kwa nafasi zao binafsi, bila ya Umoja wa Mataifa na serikali za kitaifa. 

Sio wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na hawapati malipo kwa kazi yao.

Kamishna wa Haki za binadamu wa UN ataka uwajibikaji 

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa wito mkali wa kuwajibika kwa ukiukaji mkubwa unaofanywa na pande zote zinazogombana huko Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, na Israel.

Katika ripoti yake mpya, iliyptolewa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu - OHCHR amebainisha masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mauaji kinyume cha sheria, utekaji nyara, uharibifu wa mali ya raia, adhabu ya pamoja, uhamisho wa kulazimishwa, uchochezi wa chuki na vurugu, unyanyasaji wa kijinsia, na mateso.

Vitendo vyote hivi vimepigwa marufuku na sheria za kimataifa za haki za binadamu na za kibinadamu.

“Matendo ya kuadhibiwa yaliyokithiri yaliyoripotiwa na Ofisi yetu kwa miongo kadhaa hayawezi kuruhusiwa kuendelea. Lazima kuwe na uwajibikaji kwa pande zote kwa ukiukwaji unaoonekana kwa miaka 56 ya kukalia kwa mabavu na miaka 16 ya kuzingirwa kwa Gaza, na hadi leo,” amesema Kamishna  Türk.

Ameongeza kuwa “Haki ni hitaji la awali la kukomesha mizunguko ya vurugu na kwa Wapalestina na Waisraeli kuweza kuchukua hatua za maana kuelekea amani.”

Ripoti hiyo iliangazia kipindi cha miezi 12 hadi tarehe 31 Oktoba 2023. Pia ilibainisha kuwa uchunguzi zaidi unahitajika ili kubaini kiwango kamili cha uhalifu uliofanywa chini ya sheria za kimataifa.

Wito kwa ajili ya mashtaka ya haki

Kamishna Mkuu Türk alizitaka pande zote kusitisha mara moja ukiukaji wa haki za kibinadamu na kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, na kufanya uchunguzi wa haraka, huru, usio na upendeleo, wa kina, unaofaa na wa uwazi katika madai yote ya ukiukaji wa haki.

Wale wote waliohusika na ukiukaji lazima wawajibishwe katika kesi kwa haki, alisema, akitoa wito kwa wahusika wote kushirikiana na mifumo ya kimataifa ya uwajibikaji, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Mashambulizi ya Oktoba 7 na matokeo yake

Ripoti hiyo ilisema Al Qassam, mrengo wenye silaha wa Hamas, na makundi mengine yenye silaha ya Palestina yalifanya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa kwa kiwango kikubwa tarehe 7 na 8 Oktoba.

Haya yalijumuisha mashambulizi dhidi ya raia, mauaji ya kimakusudi na kuwatendea vibaya raia, uharibifu wa ovyo wa vitu vya kiraia, na utekaji nyara, ambao ni sawa na uhalifu wa kivita.

Madai kwamba wanachama wa makundi yenye silaha za Palestina na wengine walifanya ubakaji, unyanyasaji wa kijinsia, na mateso yanahitaji uchunguzi zaidi na uwajibikaji kamili kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ripoti ya OHCHR ilibainisha.

Imeongeza kuwa jibu la kijeshi lililofuata la Israel - na uchaguzi wake wa njia na mbinu za vita - zimesababisha mateso makubwa ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na mauaji ya raia kwa kiwango kikubwa; uhamishaji mkubwa wa watu, unaorudiwa; uharibifu wa nyumba, na kunyimwa chakula cha kutosha na mambo mengine muhimu.

Wanawake na watoto wameteseka hasa na kwamba ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa umefanywa, ilisema.

Matukio makuu matatu 

Ripoti hiyo ilibainisha matukio matatu yaliyoweka alama, miongoni mwa mengine mengi, kuwa yameibua wasiwasi mkubwa kuhusu kufuata sheria za kimataifa za kibinadamu.

Mashambulio mawili kwenye Kambi ya Wakimbizi ya Jabalia na moja kwenye Al-Yarmouk, huko Gaza, yalihusisha matumizi ya silaha za milipuko zenye athari kubwa katika maeneo yenye watu wengi. 

Matukio hayo yalisababisha uharibifu mkubwa, na kulingana na ripoti hakuna onyo lililotolewa, wala juhudi zozote zilizofanywa kuhamisha watu waliokuwa katika majengo kabla ya mashambulizi.

OHCHR ilithibitisha jumla ya vifo 153 katika mashambulizi hayo, lakini idadi inaweza kuwa ya juu hadi 243.

“Kuanzisha mashambulizi ya kiholela na kusababisha kifo au majeraha kwa raia, au shambulio kwa kujua kwamba litasababisha mauaji makubwa ya raia, majeraha au uharibifu, ni uhalifu wa kivita” Kamishna Mkuu Türk alisema.