Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waziri Mkuu wa Haiti aomba msaada wa polisi na wanajeshi wa kimataifa

Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.

Waziri Mkuu wa Haiti aomba msaada wa polisi na wanajeshi wa kimataifa

Amani na Usalama

Ariel Henry, Waziri Mkuu wa Haiti, akiangazia ugumu wa kufikia maendeleo endelevu bila amani na usalama alipohutubia Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu (UNGA78) amesema kuongezeka kwa janga la usalama, afya, na uhaba wa chakula "kunatukumbusha kwamba tunasonga mbali kutoka kwenye kanuni za msingi za Mkataba wa Umoja wa Mataifa. ”.

Katika ukumbi wa kihistoria wa Baraza Kuu jijini New York, Marekani, Waziri Mkuu Ariel Henry ameeleza kuwa kuzorota kwa hali ya usalama kumesababisha janga jipya la kibinadamu, huku watu waliokimbia makazi yao wakiishi katika hali duni ya kibinadamu kwenye zaidi ya shule 25 katika mji mkuu, Port-au-Prince. 

Bwana Henry anasema ukiukaji wa haki za binadamu unaosababishwa na ghasia za magenge huhatarisha amani, utulivu na usalama wa nchi na kanda. Matokeo yake, Haiti imepitia miaka mitano ya mdororo wa uchumi, viwango hasi vya ukuaji na ongezeko la mfumuko wa bei, na nusu ya watu wanaishi chini ya mstari wa umaskini chini ya dola 2 kwa siku.

Msaada wa kijeshi

Kwa hivyo ameomba msaada ili kuimarisha Polisi wa Kitaifa wa Haiti, akishinikiza Baraza la Usalama kuchukua hatua haraka chini ya Sura ya VII ya Mkataba wa "kuidhinisha kutumwa kwa ujumbe wa msaada wa kimataifa ili kuimarisha usalama wa Haiti". Ujumbe kama huo unapaswa kuwa na askari polisi na wanajeshi kusaidia polisi katika kupambana na magenge na kurejesha amani na utulivu. Matumizi ya nguvu - kama hatua ya awali - inasalia kuwa muhimu ili kuunda mazingira ambayo Serikali inaweza kufanya kazi ipasavyo.

Matetemeko na vimbunga

"Hatuko hapa kufidia au kuhalalisha yaliyopita," amesema; badala yake, "tuko hapa kuuliza nchi marafiki kuelewa kuna jambo la haraka la kufanywa ili kuwanufaisha watu wa Haiti". Nchi hiyo imebeba mishtuko mfululizo katika miaka 15 iliyopita, ikiwa ni pamoja na matetemeko makubwa matatu ya ardhi, vimbunga kadhaa na kuuawa kwa Rais  Jovenel Moïse mnamo mwaka 2021. 

Umaskini

Aidha Waziri Mkuu huyo wa Haiti amesisitiza kuwa suluhu ya umaskini uliokithiri lazima pia ipatikane, kwani hii ndiyo "chimbuko la matatizo yote yanayoikabili nchi yangu". Umaskini kama huo unazidisha ukosefu wa ajira kwa vijana na kuweka kando jamii maskini, na kufanya maisha ya uhalifu kuwa kishawishi.

Uchaguzi

Ametoa wito kwa wahusika wote wa kisiasa kushirikiana na Serikali ili kupambana na magenge, kurejesha usalama na, "kama wanademokrasia wa kweli, watafute mamlaka kupitia sanduku la kura". 

Kuhusu hilo, amesisitiza azma ya Serikali ya kufanya uchaguzi "haraka iwezekanavyo", akisema kwamba Haiti inahitaji kurejea katika hali ya kawaida ili kukabiliana na changamoto kubwa zinazoikabili.