Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Habari kwa ufupi na yanayoendelea UNGA78

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.
UNMISS/Gregório Cunha
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria ya usiku huko Bentiu, Sudan Kusini.

Habari kwa ufupi na yanayoendelea UNGA78

Masuala ya UM

Leo ni siku ya tatu ya mjadala mkuu wa mabaraza kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78 ambapo wakuu wa nchi na serikali wanaeendelea kutoa hotuba zao kutathimini changamoto na hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa ajenda za Umoja wa Mataifa, na miongoni watakaopanda katika mimbari leo kutoka Afrika ni Rais wa Kenya, Burundi, Sudan Kusini, Zimbabwe, Malawi, Sudan na makamu wa Rais wa Uganda na Tanzania.

Afya

Kandoni mwa mjadala mkuu wa UNGA78 kuna mikutano mingine muhimu inayofanyika mathalani mkutano wa ngazi ya juu kuhusu huduma za afya kwa wote ulioandaliwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO ukiwa umewaleta pamoja wadau mbalimbali. Leo mjadala huo unajikita na mada kubwa mbili , mosi “mbinu ya huduma ya afya ya msingi ni ipi na kwa nini ina umuhimu? na pili Kuoanisha uwekezaji kwa ajili ya afya na ustawi katika ulimwengu wa baada ya coronavirus">COVID-19. Lakini leo pia mkutano huo tayari umepitisha azimio la kisiasa la kuchukua hatua ambalo liliafikiwa kwa pamoja bila kupingwa kwenye majadiliano ya kimataifa yaliyofanyika mapema mwaka huu.

Mawaziri

Pia kuna mkutano mwingine wa ngazi ya mawaziri wa maandalizi ambao unatoa fursa kwa mawaziri kueleza maono na vipaumbele vyao kwa ajili ya mkutano wa kilele wa “Wakati Ujao”, na kueleza matarajio yao ya matokeo yenye mwelekeo wa vitendo yanayoweza kupatikana wakati wakuu wa nchi na serikali watakapokutana kwenye mkutano wa kilele mwaka 2024. 

Amani

Na leo ni siku ya kimataifa ya Amani inayoadhimishwa kila mwaka 21 Septemba. Na mwaka huu siku hii inaadhimishwa dunia ikiwa imeghubikwa na majnga mbalimbali kwa mujibu wa ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa siku hii, kuanzia moto wa nyika, mafuriko, vita , kutoaminiana , umasikini, ukiukwaji wa haki za binadamu,na pengo la usawa.

Ameikumbusha dunia kwamba Amani haiji moja kwa moja ni lazima hatua zichukuliwe kusongesha malengo ya maendeleo endelevu na kutomwacha yeyeto nyuma, lakini pia hatua zichukuliwe kumaliza vita na mizozo ambacho ni chanzo kikuvbwa cha uvunjifu wa Amani.