Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muungano wa mabadiliko ya tabianchi wadai hatua, huku Guterres akionya Ubinadamu umefungua milango ya kuzimu

Viongozi wa mataifa, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia walikusanyika mjini New York kwa ajili ya Mkutano wa Kilele wa Matarajio ya Hali ya Hewa ulioandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
© UN News/Anton Uspensky
Viongozi wa mataifa, wafanyabiashara na mashirika ya kiraia walikusanyika mjini New York kwa ajili ya Mkutano wa Kilele wa Matarajio ya Hali ya Hewa ulioandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Muungano wa mabadiliko ya tabianchi wadai hatua, huku Guterres akionya Ubinadamu umefungua milango ya kuzimu

Tabianchi na mazingira

"Joto la kupindukia linaleta madhara ya kutisha duniani ", kwa mujibu wa mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akizungumza leo katika mkutano wa kwanza kabisa wa ngazi ya juu wa matarajio kuhusu mabadiliko ya tabianchi mbele ya mbele ya muungano wa kimataifa wa kuchagiza hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ulijumuisha wachagizaji, watendaji, wanasiasa, wafanyabiashara, mashirika ya kimataifa na viongozi wa asasi za kiraia waliokusanyika New York kandoni mwa mjadala wa Baraza kuu UNGA78.

Mkutano huo umetawaliwa na wito wa haraka wa kuchukua hatua, kuzuia maafa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi  kwa kumbatia mpitowa kuihamia kwenye nishati safi ambao ni  wa haki na usawa kabla hatujachelewa.

Katika hotuba yake Katibu Mkuu António Guterres ametoa onyo kali kuhusu matokeo mabaya ya kutochukua hatua.

Huku matukio ya hali ya hewa yakizidi kushika kasi ubinadamu umefungua milango ya kuzimu," Amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akieleza matukio ya kuhuzunisha ya wakulima wakitazama bila msaada mazao yakisombwa na mafuriko, kuibuka kwa magonjwa hatari kutokana na kupanda kwa kiwango cha joto, na umati mkubwa wa watu wanaokimbia moto wa nyika wa kihistoria.

Mbio za kusaka suluhu

Amesisitiza kwamba "Lengo letu hapa ni suluhisho dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kazi yetu ni ya dharura.”

Ameonya kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi "zinapunguzwa na ukubwa wa changamoto, huku binadamu wakielekea kwenye ongezeko la joto la nyuzi joto 2.8 ° C, na kuongeza hatari na kukosekana kwa utulivu.”

Lakini  amesema "Mustakbali wetu haujapangwa. Bado tunaweza kujenga ulimwengu wa hewa safi, ajira zinazojali mazingira, na nishati safi ya gharama nafuu kwa wote.”

Chachu ya kuleta mabadiliko

Wanaharakati wanakataa kunyamazishwa,watu wa asili wanakusanyika kutetea ardhi ya mababu zao, na watendaji wa mashirika wanabadilisha jinsi wanavyofanya biashara.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa anatoa wito wa kuwepo kwa Mkataba wa Mshikamano wa mabadiliko ya tabianchi ambao utawawajibisha watoa gesi chafuzi wengi zaidi, na kutoa wito kwa nchi tajiri kuunga mkono nchi zinazoinukia kiuchumi ili ziweze kukabiliana na janga hilo.”

Wito huo wa kuzisaidia nchi zinazoendelea umeungwa mkono na Rais Fillipe Nyuzi wa Msumbiji akisema” Ukiangalia vizuri suala la mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa inayotusumbua sana lakini wote lazima tushikamane na kwa wale walio na fedha za kuweza kusaidia ambao wanachafua Ulimwengu ni afadhali wasaidie pia kuweza kusafisha ulimwengu.”

Haki lazima itendeke

Katibu Mkuu amezungumza pia juu ya hitaji la haki zaidi ya mabadiliko ya tabianchi, akitambua hasira iliyohisiwa na mataifa mengi masikini zaidi ulimwenguni ambayo yameathiriwa kupita kiasi na janga hilo ambalo hawakulisababisha.

"Mataifa mengi maskini zaidi yana haki ya kukasirika," aliongeza, akielezea kuwa fedha zilizoahidiwa hazijatekelezwa huku gharama za kukopa zikibaki kuwa juu.

"Pande zote lazima zifanyie kazi mfuko wa hazina ya hasara na uharibifu katika mkutano wa COP28," amehimiza na kuzikumbusha nchi zilizoendelea lazima zitimize ahadi yao ya dola bilioni 100, kujaza mfuko wa mabadiliko ya tabianchi na kuongeza mara mbili ufadhili wa kukabiliana na janga hilo na kuunda mifumo ya tahadhari ya mapema kwa kila mtu kufikia 2027 ni lazima pia.

Kujenga upya uaminifu

Ajenda ya kuongeza kasi ya hatua pia inatoa wito kwa makampuni ya biashara na taasisi za fedha kushika njia ya kutozalisha kabisa gesi chafuzi, kwa kuzingatia uwazi na uaminifu katika mipango ya kupunguza uzalishaji wake.

Katibu Mkuu amesema "Kila kampuni ambayo ina maana ya biashara, lazima iunde mipango ya mpito ambayo itapunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kutoa haki dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.”

Amehitimisha kwa kutoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi kwenye vyumba vya mikutano mjini New York akisisitiza kwamba "Tunaweza na lazima tuongeze kasi ya hatua.”

Bofya hapa kupata maelezo zaidi.