Tunapokabiliana na mabadiliko ya tabianchi tusipuuze tabaka la Ozoni-Guterres 

16 Septemba 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema dunia inapojikita katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi basi isipuuze tabaka la Ozoni na kuwa na tahadhari ya tishio kubwa linalosababishwa na matumizi haramu ya gesi zinazotoboa tabaka la Ozoni au chlorofluorocarbons.“utambuzi wa hivi karibuni wa utoaji wa moja ya gesi hizo (CFC-11) unatukumbusha kwamba tunahitaji kuendelea na mifumo ya kufuatilia , kutoa taarifa, kuboresha na kuchukua hatua.”

Antonio Guterres ameyasema hayo katika ujumbe wake maalum kuhusu siku ya kimataifa kwa ajili ya kulinda tabaka la Ozoni ambayo kila mwaka huadhimishwa Septemba 16, akiikumbusha dunia kwamba wiki ijayo viongozi wa dunia watakusanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kwa ajili ya mkutano wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ambao lengo lake kuu ni kuchagiza kuchukua hatua zaidi kimataifa kushughulikia dharura ya mabadiliko ya tabianchi.

Guterres amesema mwaka huu umevunja rekodi pia ya kuwa na joto la kupindukia, vimbunga na uharibifu uliosababishwa na hali ya hewa hali ambayo amesema “inatujulisha kwamba hatuna chaguo lingine isipokuwa kuchukua hatua sasa kabla hatujachelewa.”

Ameongeza kuwa wakati tukijiandaa na mkutano huu muhimu “ni lazima tukumbuke kuwa Mkataba wa Montreal ni mfano wa kuchagiza jinsi gani binadamu wanavyoweza kushirikiana ili kushughulikia changamoto za kimataifa na chombo muhimu kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa sasa wa mabadiliko ya tabianchi”.

Amesisitiza kwamba chini ya mkataba huu wa kimataifa, mataifa yamefanya kazi kwa miaka 32 kupunguza matumizi ya kemikali za tabaka la Ozoni ambazo zinatumika zaidi na sekta ya vifaa vya baridi . Na matokeo yake tabaka la Ozoni ambalo linatukinga na miale mikali ya jua liko njiapanda.

Amesema mktaba huo wa Montreal unaweza kuleta matokeo mazuri kuhusu mabadiliko ya tabianchi kupitia mkataba wa marekebisho wa Kigali ambao umelenga zaidi kemikali za (HFC) ambazo zinatumika katika mifumo ya kuleta baridi kama viyoyozi

Amesema mkataba huo wa Montreal umefanikiwa kwa sababu ya kuungwa mkono kimataifa na “nawapongeza nchi 81 ambao wameridhia mkataba wa Kigali wa marekebisho na kuwachagiza wengine wote kufuata nyayo.” Mchango wa makampuni makubwa ya kimataifa ni muhimu sana katika kufanikisha ndoto hizo.

Tabaka la Ozoni lililo salama na mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu katika kutimiza malengo yote ya maendeleo endelevu katika kulinda dunia na watu wake.

Katika siku hii ya kimataifa ya kulinda tabaka la Ozoni kuwa hamasa ya kufikia lengo kuhusu masuala ya mifumo ya baridi, kwenye mkutano wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na zaidi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud