Mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri na hatuna tena pa kujificha:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani 10 septemba 2018
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitoa hotuba muhimu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani 10 septemba 2018

Mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri na hatuna tena pa kujificha:Guterres

Tabianchi na mazingira

Mabadiliko ya tabia nchi sio ndoto wala kiini macho ni dhahiri, tusipochukua hatua sasa mustakabali wa dunia kwa kizazi hiki na vijavyo uko mashakani , ameonya leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihimiza mshikamano wa kimataifa kuhusu suala hili.

Mabadiliko ya tabia nchi ni dhahiri na sayansi imethibitishja hilo hivyo hatuna pa kujificha bali ni kuchukua hatua madhubuti kukabiliana nayo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati wa hotuma mahsusi ya kuwataka nchi wanachama kuchukua hatamu za uongozi na kuhakikisha ushiriki wa kila mmoja katika kuilinda Dunia na watu wake dhidi ya athari za zahma ya mabadiliko ya tabia nchi.

Guterres amesema mabadiliko ya tabia nchi yanatishia mustakabali wa Dunia hivyo umefika wakati wa “kuondokana na njia zinazoitumbukiza dunia katika tanuru la moshi”ameongeza kuwa ingawa uwezo wa kudhibiti janga hilo upo kuna tatizo moja “Kile  kinachokosekana kwa sasa , hata baada ya kutiwa saini mkataba wa Paris, ni uongozi na utashi wa kutekeleza kinachohitajika.”

Image
Mabadiliko ya tabia nchi:Picha na UM/Elias Barjanos

 

Ametoa wito kwa serikali, makampuni ya biashara, wanasayansi, na walaji kufanya mabadiliko makubwa na pia kuwa chachu ya mabadiliko hayo ambayo yatairejesha dunia katika mstari unaotakiwa ili kuwa na mtakbali bora kwa vizazi vya leo na vijavyo.  Amekumbusha kuwa hali ya mabadiliko ya tabianchi ikiendelea kwa mwenendo huu  maji yataadimika, watu wengi watalazimika kuhama kutoka majumbani mwao na ukame, mafuriko, au vimbunga vitazidisha adha katika maisha yao. Amesisitiza kuwa kasi ya mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa kuliko juhudi za kupambana nayo akitolea mfano “Utabiri wa shirika la hali ya hewa dunaini WMO miongo miwili iliyopita imekuwa yenye joto 1850.Na mwaka huu 2018 unaonekana kushika nafasi ya nne ya mwaka wenye joto zaidi duniani. Wimbi la joto, mioto ya nyikani, na mafuriko  vinasababisha maafa makubwa .”

Guterres amesema mataifa tajiri yanachangia kwa kiasi kikubwa zahma hii , lakini wanaobeba gharama zake ni mataifa masikini. Amewataka viongozi wa Dunia kutumia fursa kati ya sasa na wakati wa mkutano uatakaofanyika Poland mwezi Desemba mwaka huu kusaka suluhu mbalimbali za mabadiliko ya tabia nchi. Pia ameelezea mtazamo wa mkutano mpya wa mabadiliko ya tabia nchi mwaka 2019 ambao atauitisha kwa ajili ya kuichagiza Jumuiya ya kimataifa kuongeza hatua katika baadhi ya maeneo ikiwemo uzalishaji wa nishati, ukuaji wa uchumi, uwekezaji unaojali mazingira, na ulinzi bora wa maliasili.