Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti: Suluhu za asili zitumike kutatua changamoto za SDGs na Mabadiliko ya tabianchi

Wanyamapori na misitu yetu iko katika hatari kubwa ya athari mbaya za plastiki.
Pawan Prasad
Wanyamapori na misitu yetu iko katika hatari kubwa ya athari mbaya za plastiki.

Ripoti: Suluhu za asili zitumike kutatua changamoto za SDGs na Mabadiliko ya tabianchi

Tabianchi na mazingira

Suluhu za miundombinu ya asili zinaweza kuleta athiri chanya kwa asilimia 79 ya shabaha zote katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu- SDGs, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa bioanuwai, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa. 

Ripoti hiyo mpya iliyopewa jina la Miundombinu ya Asili: Jinsi ufumbuzi wa miundombinu ya asili unavyoweza kushughulikia changamoto za maendeleo endelevu na mgogoro wa sayari tatu imetolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya utekelezaji wa miradi, UNOPS na Chuo Kikuu cha Oxford jijini Copenhagen nchini Denmark.

Ripoti hii inalenga kuunga mkono juhudi za kuongeza matumizi ya suluhu za asili kama sehemu muhimu ya mifumo endelevu ya miundombinu.

Akizungumzia katika uzinduzi wa ripoti hiyo, Naibu Mkurugenzi wa UNOPS kwenye Kundi la Usimamizi wa Miundombinu na Miradi (IPMG), Steven Crosskey amesema maamuzi ya sasa kuhusu uwekezaji wa miundombinu yanaweza kuamua uwezo wa kufikia ajenda yetu ya pamoja ya kimataifa kuhusu ajenda 2030. 

Crosskey amesema maamuzi hayo pia yatafanikisha “kukabiliana na majanga matatu ya sayari ambayo ni mabadiliko ya tabianchi, mazingira, na upotevu wa bayoanuwai ili kuhakikisha ubora wa maisha yetu ya baadaye ya pamoja. Ripoti hii inaangazia jinsi tunavyoweza kukabiliana na masuluhisho yanayotegemea asili ndani ya upangaji wa miundombinu, utekelezaji na uendeshaji unaoweza kutoa manufaa ya binadamu na bayoanuwai, huku ikipunguza utoaji wa gesi chafu.”

Ripoti inagundua kuwa matokeo chanya mengi zaidi kwenye SDGs hupatikana wakati suluhisho za asili zinapojumuishwa na wakati wa kujenga miundombinu na kwamba zinapojumusihwa zinaathiri SDGs kwa asilimia 95. Kuhusiana na Mfumo wa Kimataifa wa Bioanuwai, miundombinu inayotegemea asili inaweza kuathiri malengo matatu kati ya manne ya muda mrefu na asilimia 70 ya malengo 23. 

Ripoti hiyo imetolea mfano jinsi urejeshaji wa miamba ya matumbawe, mikoko na mimea mingine ya ufuo ulivyosaidia kutoa ulinzi wa mafuriko na fursa za maisha kwa zaidi ya wananchi 8,600 jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania, ambapo miundombinu ya umma na ya kibinafsi yenye thamani ya dola bilioni 5.3 iko hatarini kutokana na mafuriko.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sekta na Uchumi wa UNEP, Sheila Aggarwal-Khan amesema “Dunia inakabiliwa na changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka kwa kasi ya huduma za miundombinu kwa njia ambayo itakuwa na matumizi ya chini ya kaboni, ufanisi wa rasilimali, yenye kuzingatia kutuza asili.” 

Bi. Aggarwal-Khan ameongeza kuwa ripoti hiyo imeangazia jukumu muhimu ambalo miundombinu ya asili inatekeleza katika kutoa huduma nyingi na manufaa shirikishi ambayo yanachangia maendeleo endelevu na jamii zenye afya na uthabiti, na kuongeza athari chanya za SDG kwa karibu asilimia 50 katika baadhi ya sekta. “Ili kufikia manufaa haya, ni lazima tupange miundombinu kwa njia ambayo inawajibika na kulinda mali zetu asilia,” Amesisitiza. 

Waandishi wa ripoti hiyo wamesisitiza michango muhimu ya ufumbuzi wa miundombinu ya asili kwa kupunguza na kufikia malengo yaliyo ndani ya Mkataba wa Paris. 

Wamesema suluhu za miundombinu ya asili zinaweza kuchangia kukabiliana na hali ya hewa kwa kulinda jamii na miundombinu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na pia kusaidia matokeo ya kukabiliana na hali ya kitaifa kwa upana zaidi, kwa kuunda uchumi, jamii na mifumo ya ikolojia inayostahimili zaidi.