Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais Kagame: Tusipooze tu joto linaloathiri tabianchi, bali pia tupooze mizozo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.
UN Photo/Cia Pak
Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia mjadala mkuu wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu.

Rais Kagame: Tusipooze tu joto linaloathiri tabianchi, bali pia tupooze mizozo.

Amani na Usalama

Pamoja na changamoto zinazoendelea duniani ikiwemo athari zilizoletwa na janga la COVID19 pamoja na mabadiliko ya tabianchi, Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema iwapo tunataka kuwa na dunia yenye amani na matumaini basi “tusipooze tu joto linaloathiri tabianchi bali pia tupooze mizozo.”

Tweet URL

Akihutubia katika mjadala Mkuu wa Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78 jijini New York Marekani katika siku ya pili ya mkutano huo Kagame amesema “Mpaka sasa hakuna dalili yoyote inayoleta matumaini ya kumaliza mizozo inayoendelea duniani, hatuoni hata matumaini kutoka kwa wale wenye ushawishi, kuwa mwisho unakaribia.” 

Uwakilishi wa Afrika

Katika hotuba yake hiyo aliyohutubia kwa dakika 10, mkuu huyo wa Rwanda amezungumzia pia umuhimu na udharura katika kuhakikisha bara la Afrika linawakilishwa kikamilifu katika bodi zinazofanya maamuzi kuhusu masuala yajayo ambayo Afrika ina maslahi nayo. 

“Kwa udharura huo huo Afrika lazima ijiandae kikamilifu kuzungumza kwa lugha moja na hatimaye mfumo unaofaa zaidi lazima utoe uzito sawa kwa mahitaji na vipaumbele vya kila mtu. Hilo ndilo linalojenga ubia wa haki na usawa, na ulimwengu wa haki na amani zaidi na hilo ndilo kila mtu anasema anataka.”

Hatutawaacha wahamiaji

Kuhusu mgogoro wa wahamiaji Rais huyu amesema nchi yake ipo bega kwa bega na wahamiaji na wakimbizi.

“Uamuzi huu umeundwa na uzoefu wetu na kutambua kwa dhati maumivu ya kupoteza kila kitu na kutokuwa na sehemu unayoweza kuiita nyumbani. Na hii ni sehemu ya ahadi yetu ya kutomuacha mtu yeyote nyuma.”  

Kila mwaka wahamiaji na wakimbizi wanafanya safari za hatari lengo likiwa ni kusaka maisha bora na Rwanda imeahidi kuendelea kufanya kazi na wadau ikiwemo Umoja wa Mataifa na Kamishna wa Wakimbizi kusaka suluhu ya kudumu. 

Kutazama hotuba nzima ya Rais wa Rwanda bofya hapa.