Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN tuondoleeni vikwazo vya silaha - Rais Salva Kiir

Rais wa Sudan Kusini, Salvar Kiir Magardit akihutubia katika Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78.
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Sudan Kusini, Salvar Kiir Magardit akihutubia katika Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78.

UN tuondoleeni vikwazo vya silaha - Rais Salva Kiir

Amani na Usalama

Rais wa Sudan Kusini, Salvar Kiir Magardit, ametaka nchi yake kuondolewa vikwazo vya silaha akieleza vinakwamisha maendeleo ya nchi yao.

Akihutubia katika Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78 hii leo Rais huyo amesema “tunatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kutuondolea vikwazo vya silaha vilivyowekwa kwa nchi yetu ili kusaidia utekelezaji wa amani na kulinda uchaguzi.”

Amebainisha kwamba “marufuku ya silaha iliyowekwa dhidi yetu imekwamisha utekelezaji wa mipango ya usalama kwasababu utekelezaji madhubuti wa vikosi vya pamoja hautaweza kutekelezwa bila silaha”.

Tumehemewa na wakimbizi

Akizungumzia suala la ulinzi na usalama amesema nchi yake imepakana na taifa la Sudan na tangu mwezi Aprili wamekuwa wakipokea idadi kubwa ya wakimbizi. 

“Utitiri huu wa watu umezifanya jumuiya zilizopo mipakani kuhemewa na kusababisha mgororo wa kibinadamu.” 

Ametoa ombi kwa jumuiya za kimataifa kutoa misaada kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wa ndani ambao wanaingia nchini mwake. 

“Wakati dunia inakabiliana na matatizo mengi, tunatoa wito wa kutolewa kwa usaidizi endelevu kwa watu hawa waliokimbia makazi yao tunaposhughulikia jinsi ya kurejesha amani na utulivu nchini Sudan.”

Vile vile Magardit, amepongeza Azimio la Nairobi kuhusu mabadiliko ya tabianchi lililopitishwa hivi karibuni nchini Kenya.

Amehimiza pia viongozi kuboresha uaminifu na kurejesha mshikamano wa kimataifa ili kudumisha malengo ya maendeleo Endelevu ya ajenda 20230.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake ametoa wito kwa wadau mbalimbali waongeza ushirikiano ili kuhakikisha mchakato wa amani wa Sudan Kusini unaendeleshwa na wananchi wao.

Kutazama hotuba yake yote tafadhali bofya hapa