Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni kutumia vikwazo vya kimataifa kama silaha - Rais Mnangangwa

Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa wakati akihutubia mkutano wa 78 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani
UN Photo/Cia Pak
Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa wakati akihutubia mkutano wa 78 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani

Acheni kutumia vikwazo vya kimataifa kama silaha - Rais Mnangangwa

Masuala ya UM

“Tunalaani vikwazo vinavyowekwa na nchi tajiri kwa nchi kama zimbabwe na Cuba ambavyo ni haramu na vinatumiwa kama nyenzo ya sera za kigeni ya mataifa tajiri kwani vikwanzo hivyo vinatatiza uaminifu, mshikamano na umoja wa kimataifa.“ Amesema leo Rais wa Zimbabwe Emmerson Dambudzo Mnangagwa wakati akihutubia mkutano wa 78 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani.

Katika hotuba yake hiyo iliyochukua dakika 11 na Sekunde 40 Rais Mnangagwa ameeleza taifa lake la Zimbabwe kwa miaka 23 limeathirika na vikwazo vya kiuchumi vya kimataifa vilivyowekwa na nchi za magharibi akisema “Vikwazo hivyo vimewekwa ili kukandamiza uhuru wa wananchi wa Zimbabwe.”

Ameeleza pamoja na kushukuru msaada na mshikamano unaotolewa na nchi zilizoendelea katika jumuiya ya kimataifa “Tunataka vikwazo visivyo vya haki vya upande mmoja viondolewe bila masharti, ikiwa ni pamoja na vile vilivyowekwa kwa nchi kama Cuba.”

Amesema kuondolewa kwa vikwazo hivyo ni muhimu kwani itasaidia kuelekeza juhudi za pamoja katika kujenga amani na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo, kwa ustawi wa pamoja. “Kuna mengi zaidi ambayo yanatuunganisha, kuliko yale yanayotutenganisha.”

Amegusia pia hitaji la kufanya mabadiliko katika mashirika ya kimataifa yakutoa fedha za maendeleo akisema lazima kuwe na mipango si ya muda mfupi pekee bali pia ya muda mrefu.

Undumilakuwili

Amezishukia na kulaani vikali baadhi ya nchi tajiri ambazo amesema “zina hubiri amani, haki za binadamu na demokrasia na wakati huo huo zikitoa fedha kufadhili migogoro na kufanya mabadiliko ya serikali kinyume cha katiba kwa maslahi yao binafsi.”

Amerejelea pia wito unaotolewa na viongozi mbalimbali wa Afrika wanaotaka kufanyike mabadiliko makubwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mabadiliko ya tabianchi

Kabla ya kuhitimisha hotuba yake ametuma salamu za pole na rambirambi kwa nchi ya Morocco ambayo ilikumbwa na tetemeko la ardhi na nchi ya Libya ambayo ilikumbwa na mafuriko hivi karibuni na kueleza kuwa “kujenga mnepo wa kughulikia changamoto ziletwazo na mabadiliko ya tabianchi inapaswa kuwa kipaumbele cha dharura kwetu sote.”  

Amegusia nchini kwake Zimbabwe na mataifa mengine yaliyo kusini mwa Afrika nayo yamekuwa waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya nchi hizo. 

“Kuna haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti za mabadiliko ya tabianchi badala ya ahadi hewa ili tuweze kuweze kukabiliana, kuwa na ustahimilivu na mnepo. Pia tunapaswa kuhamia kwenye nishati jadidifu, kilimo endelevu na ujenzi unaozingatia kutunza mazingira.” 

Amesema wakati nchi yake ikiendelea kuboresha utoaji wa taarifa za mapema kwa wananchi kuhusu majanga, tayari taifa hilo linatekeleza sera ya mabadiliko ya tabianchi.

 Katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu amesema nchi yake imeendelea kujenga mabwawa, vituo vya afya na matumizi ya nishati ya sola hususan vijijini.

Kutazama video ya hotuba nzima ya Rais huyo wa Zimbabwe bofya hapa.