Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 3 wameikimbia Sudan katika muda wa miezi mitatu: IOM

Wakimbizi kutoka Sudan wanapokea misaada inayosambazwa na UNICEF na washirika wake huko Kounfroun, Chad.
© UNICEF/Donaig Le Du
Wakimbizi kutoka Sudan wanapokea misaada inayosambazwa na UNICEF na washirika wake huko Kounfroun, Chad.

Watu milioni 3 wameikimbia Sudan katika muda wa miezi mitatu: IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika kipindi cha miezi 3 ya vita nchini Sudan idadi ya wakimbizi wanaoenda kusaka usalama nchi jirani imefikia milioni 3 limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya uhamiaji IOM.

Mamia ya maelfu ya watu hao wako katika makambi, majengo ya umma na makazi ya muda na IOM inataja hali ya hatari sana inayowakabilia nje ya nchi  huku ombi kutoka kwa vyombo vya Umoja wa Mataifa linadai uchunguzi wa kina na huru wa kesi za unyanyasaji wa kingono na kijinsia.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, kuna wakimbizi wa ndani milioni 2.2 na karibu wakimbizi 700,000 wanaosaka usalama na makazi kuvuka mipaka ya nchi yao wengi wakikosa huduma za msingi kama chkula, huduma za afya na vifaa vingine vya muhimu.

Mkurugenzi wa kanda wa IOM Othman Belbeisi amerejelea wito wake wa usitishwani wa mapigano hayo yaliyoanza mwezi Aprili2023 na kuondolewa kwa ukiritimba wote unaozuia utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu waliokwama nchini humo katikati ya mapigano na wale walio katika mazingira magumu wenye kuhitaji msaada.

Kukimbilia nchi jirani

Makambi, majengo ya umma na makazi ya muda yanahifadhi watu 280,000 ndani ya eneo la Sudan.

Zaidi ya theluthi mbili ya jumla ya wato wote walipotawanywa na vita inayoendelea wameondoka katika jimbo la Khartoum na sehemu iliyobaki imeondoka katika eneo la Darfur na kuelekea majimbo kama vile Kaskazini, Mto Nile, Darfur Magharibi na White Nile.

Wengi wa Wasudan waliokimbilia nje ya nchi wako Misri, ambako ni nyumbani kwa asilimia 40 ya waliokimbia. 

Wenyeji wengine wa wakimbizi hao ni Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

sita kati ya wakimbizi 10 ni Wasudan na wengine waliorejea au raia wa nchi nyingine. 

IOM pia inaangazia hali ya hatari ya wengi wa wale wanaohamia mataifa jirani.

Wanawake wanachukua hatua kwa ajili ya misaada na kumaliza migogoro

Kwa mujibu wa IOM takriban nusu ya watu, au watu milioni 24.7, wanahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi.

Jumatano wiki hii shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women litangaza kuunga mkono karibu mipango 50 ya amani inayoongozwa na wanawake. 

Mashirika yanayounda jukwaa la amani kwa ajili ya Sudan ni ya kibinadamu na ya kijamii.

Wanachama wa mafunzo katika majimbo mbalimbali ya nchi yanahusisha kuimarisha ujuzi wa mawasiliano na vitendo vinavyokuzwa na wanawake. 

Mbali na kuchukua hatua za kibinadamu na kutetea kukomeshwa kwa mizozo, UN Women inatetea kukomesha unyanyasaji wa kijinsia katika visa ambapo walengwa wakuu ni wakimbizi na wanawake waliokimbia makazi yao.

Wiki hii, Umoja wa Mataifa pia ulijiunga na taasisi kadhaa katika ombi la kukomesha unyanyasaji wa kingono kama mbinu ya vita nchini Sudan.

Ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa 

Miongoni mwa waliotia saini hati hiyo ni ofisi za Umoja wa Mataifa za misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, ofisi ya Haki za binadamu OHCHR, pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu UNFPA na shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO.

Kundi hilo limetoa wito wa uchunguzi kuhusu madai yote ya ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu kufanyika "haraka, kikamilifu, bila upendeleo na huru na kwa wale waliohusika kuwajibishwa.”