Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sote tunahitaji kujitokeza kuokoa SDG's na kupigania mustakabali bora: Mkuu wa UN

Ufunguzi wa wikiendi ya hatua kwa ajili ya SDGs. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akionekana kwenye skrini wakati akitoa hotuba yake
UN Photo/Cia Pak
Ufunguzi wa wikiendi ya hatua kwa ajili ya SDGs. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akionekana kwenye skrini wakati akitoa hotuba yake

Sote tunahitaji kujitokeza kuokoa SDG's na kupigania mustakabali bora: Mkuu wa UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Jumamosi amehimiza makundi mbalimbali ya mashirika ya kiraia kutumia sauti zao, vitendo na mitandao ya mashinani "kusaidia kuokoa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kupigania mustakbali bora wa baadaye ambao kila mtu anastahili."

Huku viongozi wa dunia wakitarajiwa kukusanyika wiki ijayo kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa ngazi ya juu wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ya Midtown Mashariki mjini New York wikiendi hii ni mwenyeji wa watendaji mbalimbali wenye nguvu kuanzia makundi ya vijana na mashirika ya wanawake, hadi mameya, wanaharakati wa jamii na viongozi wa sekta ya biashara wanaotazamia kuongeza uungwaji mkono kwa Malengo hayo kabla ya Mkutano maalum wa SDG.

Mkutano wa kilele wa malengo hayo tarehe 18-19 Septemba utaashiria kufika katikati ya  muda wa utimizaji SDGs, tangu yaalipozindulia 2015 na tarehe ya mwisho ya utimizaji wake mwaka 2030.

Kila mtu lazima achakarike

Kwa hali ilivyo sasa, Katibu Mkuu amesema “Malengo na ahadi za nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zilipopitisha Ajenda ya 2030 ya kutomwacha mtu yeyote nyuma ziko katika matatizo makubwa kwani licha ya hatua fulani zilizopigwa kwa miaka mingi mapungufu ya utekelezaji yamejitokeza katika malengo yote 17, ambayo yanalenga kukabiliana na kila kitu kuanzia umaskini, njaa na usawa wa kijinsia, kufikia elimu na nishati safi kwa wote.”

Ameongeza kuwa kudorora kwa hamasa ya umma katika kufikia Malengo hayo, mgongano wa kijiografia na pengine muhimu zaidi, janga la kimataifa la COVID-19, vimeyaacha malengo ya SDGs yakihitaji mpango wa kimataifa wa kuyaokoa malengo hayo.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa "Leo, ni asilimia 15 tu ya malengo ndio yametimia, na mengi yanarudi nyuma. Mkutano wa SDG wa Jumatatu utakuwa wakati wa serikali kuja mezani na mipango na mapendekezo madhubuti ili kusongesha mchakato wa utimizaji wa malengo hayo ya maendeleo.”

Sio tu kuweka alama ya vema kwa idadi ya SDGs

Lakini mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa malengo ya SDGs si kuhusu kuangalia na kuweka alama ya vema. 

Bali “Yanahusu matumaini, ndoto, haki na matarajio ya watu na afya ya mazingira yetu ya asili. Yanahusu kurekebisha makosa ya kihistoria, kuponya migawanyiko ya kimataifa na kuweka ulimwengu wetu kwenye njia ya amani ya kudumu.” 

Amesisistiza kuwa kila mtu anahitaji kujitokeza ili kusaidia kufufua Malengo na kuhakikisha maisha bora kwa watu na sayari.

Bwana Guterres ameendelea kupongeza ujasiri na imani ya wanaharakati waliohudhuria, akisema kwamba alijua vita vyao vya kimataifa kwa ajili ya SDGs "vinahatarisha usalama wao, uhuru na hata maisha yako."

Wito wake kwao

Guterres amesema "Ninawaomba muendelee” na vile vile akawasihi wanachama wa jumuiya ya wafanyabiashara waliohudhuria "kuona kwamba maendeleo endelevu ni mpango bora zaidi wa biashara".

"Kwa wanawake na vijana wanaojiunga nasi endeleeni kutoa wito wa mabadiliko katika jumuiya zenu na kupigania haki zenu na nafasi katika kila meza," amesema Katibu Mkuu.

Hatimaye, mkuu wa Umoja wa Mataifa akakamilisha tarifa yake kwa kusema "Kwa mamlaka za mashinani mlio hapa, malengo ya SDGs hayataokolewa mjini New York bali yataokolewa katika jamii zenu. Kwa hivyo endeleeni kuwasikiliza watu katika jumuiya zenu na kupachika mahitaji na wasiwasi wao katika sera na uwekezaji wenu.”

Balozi Dennis Francis kutoka Jamhuri ya Trinidad na Tobago kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Balozi Dennis Francis kutoka Jamhuri ya Trinidad na Tobago kuwa Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Wikiendi ya Utekelezaji wa SDGs inajumuisha siku ya uhamasishaji wa SDGs ambayo ni leo Jumamosi, 16 Septemba, na siku ya Kuongeza Kasi ya SDGs ambayo ni kesho Jumapili, 17 Septemba hapa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa  mjini New York Marekani.

Dennis Francis, Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu

Naye Dennis Francis, Rais wa kikao cha 78 cha Baraza Kuu alipopanda kwenye mimbari ya ukumbi wa Baraza Kuu hakutafuta maneno "Neno kuu la siku hii ni uhamasishaji, ambao unapendekeza hisia ya uharaka ambao hatuwezi kupuuza.”

Akaenda mbali zaidi na kukumbusha hadhira iliyokusanyika kwamba “Hizi ni dakika za majeruhi. Ni wakati wa kukunja mashati ya mikono yetu na kugeuza matarajio yetu na ahadi zetu kuwa hali halisii Kwa manufaa ya watu wote.”