Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa Umoja wa Mataifa awataka viongozi wa G20 kuungana kwa manufaa ya wote

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akipokelewa na Katibu Mwenezi wa Wizara ya Mambo ya Nje Prakash Gupta alipowasili New Delhi kwa G20.
UN India/Ruhani kaur
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akipokelewa na Katibu Mwenezi wa Wizara ya Mambo ya Nje Prakash Gupta alipowasili New Delhi kwa G20.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa awataka viongozi wa G20 kuungana kwa manufaa ya wote

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewasili New Delhi, India kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa Kundi la nchi 20  zilizoendelea kiuchumi duniani (G20) akiwa na "ombi rahisi lakini la dharura" kwa viongozi wa dunia waliohudhuria: kuungana kutatua changamoto kubwa za ubinadamu. 

Akizungumza katika mkesha wa mkutano wa kilele wa G20, ambao utafanyika katika mji mkuu wa India, New Delhi tarehe 9-10 Septemba, Bwana Guterres amesema uongozi wa kimataifa unahitajika hasa katika maeneo mawili ya kipaumbele - hatua ya mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu. 

“Hatuna muda wa kupoteza. Changamoto zinaenea hadi jicho linavyoweza kuona,” Katibu Mkuu ameuambia mkutano wa waandishi wa habari leo mjini New Delhi. 

Aidha kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba dunia iko katika wakati mgumu wa mpito, inakabiliwa na kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na umaskini na viwango vya njaa na ukosefu wa mshikamano wa kimataifa. 

“Hatuwezi kuendelea hivi. Ni lazima tujumuike pamoja na kutenda pamoja kwa manufaa ya wote.” 

Bwana Guterres amebainisha kuwa nchi wanachama wa G20 ndizo wazalishaji wakuu wa dunia wa hewa chafuzi, zinazowajibika kwa asilimia 80 ya jumla ya uzalishaji wa kimataifa, na kwa hiyo zinahitajika kuonesha uongozi mkubwa juu ya hatua za tabianchi. 

“Uongozi unamaanisha kuweka hai lengo la nyuzijoto 1.5; kujenga upya uaminifu kwa kuzingatia haki ya tabianchi; na kuendeleza mageuzi ya haki na usawa kwa uchumi wa kijani."

Ameongeza kuwa uongozi pia unamaanisha nchi tajiri hatimaye kutimiza ahadi zao za muda mrefu za ufadhili kusaidia nchi zinazoendelea kufikia malengo yao ya kupunguza uzalishaji, kama vile Mfuko wa Tabianchi ya Kijani. 

Katibu Mkuu amesema viongozi lazima pia wachukue hatua madhubuti ili kuhakikisha dunia inafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa wakati uliopangwa ifikapo 2030. 

Bwana Guterres atashiriki wikendi hii katika mkutano wa kila mwaka wa G20, ambao mwaka huu India ndiye rais wake na kaulimbiu ya "Dunia Moja, Familia Moja, Wakati Mmoja". 

Ameigusia kaulimbiu hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari leo kusisitiza kwamba, "lazima tuchukue hatua pamoja kama familia moja ili kuokoa Dunia yetu moja na kulinda maisha yetu ya baadaye."