Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shaka na shuku zimetawala dunia, mashauriano ni muhimu- Guterres

Viongozi wa mataifa ya kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa na unaokua kwa kasi, G20 pamoja na Kaitbu Mkuu wa wa UN wakiwa kwenye picha ya pamoja huko Osaka, Japan kabla ya kuanza kwa mkutano wao hii leo.
G20 Osaka Summit 2019
Viongozi wa mataifa ya kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa na unaokua kwa kasi, G20 pamoja na Kaitbu Mkuu wa wa UN wakiwa kwenye picha ya pamoja huko Osaka, Japan kabla ya kuanza kwa mkutano wao hii leo.

Shaka na shuku zimetawala dunia, mashauriano ni muhimu- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mkutano wa kundi la mataifa 20, G20 unafanyika wakati ambapo shaka na shuku zimekumba dunia nzima katika nyanja zote kuanzia kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Osaka, Japan kabla ya kuhutubia kesho Jumamosi mkutano huo wa kundi la mataifa yenye uchumi mkubwa na unaokua kwa kasi kubwa, Bwana Guterres amesema “ni nyakati za kutokuwa na uhakika wa uchumi wa dunia, ukosefu wa uhakika kutokana na mizozo ya kibiashara, lakini pia ukosefu wa uhakika kutokana na kiwango cha juu cha madeni, masoko ya fedha yasiyo tulivu na hatari ya kudorora kwa uchumi.”

Amesema ingawa anatambua ari ya serikali ya Japan na Waziri wake Mkuu ya kuona mkutano huo unamalizika na hitimisho lenye maana, “ni dhahiri shairi kuwa itakuwa vigumu kupata majawabu kuhusiana na changamoto kubwa zaidi zinazokumba dunia hivi sasa.”

 Hata hivyo amesema “Umoja wa Mataifa si sehemu ya G20, sisi si wanachama wa G20, lakini ninashukuru kwa fursa hii ya kuhutubia viongozi na kuwasilisha shaka na shuku zetu.”

 Katibu Mkuu ametaja changamoto kubwa mbili ambazo ni mabadiliko ya tabianchi na utekelezaji wa ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, akisema katika masuala yote mawili, dunia bado iko nyuma katika kufanikisha.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia waandishi wa habari kabla ya kushiriki mkutano wa G20 Osaka Japan (Tarehe 28 Juni 2019)
UN Japan/Takashi Okano
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia waandishi wa habari kabla ya kushiriki mkutano wa G20 Osaka Japan (Tarehe 28 Juni 2019)

Akifafanua changamoto ya mabadiliko ya tabianchi akisema kuwa sasa anaanamini sayansi, Bwana Guterres amesema kasi yake ni kubwa kasi ya kukabili, “tunashuhudia mikondo ya joto huko Ulaya, ukame Afrika, vimbunga barani Afrika pia na Karibea na hata Marekani. Tunashuhudia msururu wa majanga ya asili ambayo yanakuwa na madhara makubwa na athari kubwa zaidi kwa binadamu.”

Ametaka hatua zaidi kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa ili kiwango cha joto na kila taifa litekeleze mchango wake.

SDGs, Mvutano Iran na Marekani, Wakimbizi 

Kuhusu SDGs ametaka kuchagiza rasilimali zaidi za nje na za ndani na kuchukua hatua kama vile kudhibiti rushwa na kusimamia utawala wa sheria.

Waandishi wa habari walimuuliza Katibu Mkuu kuhusu mvutano kati ya Iran na Marekani wakati huu ambapo Iran inatarajiwa kukiuka kiwango cha mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kuhusu urutubishaji wa Uranium, jambo linaloleta mvutano, Bwana Guterres amesema, “tumekuwa tunaamini sana JCPOA kuwa ni msingi wa utulvu na itakuwa vyema kuuzingatia. Kwa hiyo nasihi kila mtu pamoja na Iran. Ni wazi kuwa ni muhimu kupunguza mvutano kwenye eneo la ghuba.”

Amesema kwa sasa hatuhitaji mvutano wowote kwa kuzingatia hali ya mvutano iliyopo akizingatia  shambulio la hivi karibuni la meli ya mafuta kwenye mfereji wa Hormuz na Ghuba ya Oman.

Alipoulizwa kuhusu suala la wakimbizi hususan kwenye mpaka wa Marekani na Mexico na picha ya mtoto na baba yake kuzama maji wakati wakihaha kuingia Marekani, Katibu Mkuu amesema, hana uhakika iwapo suala la wakimbizi Amerika ya Kusini litajadiliwa kwenye mkutano huo wa G20 lakini, “jawabu la hali hii ni kutumia ipasavyo mkataba wa kimataifa wa uhamiaji na kurejesha utu wa mkataba wa kulinda wakimbizi.”