Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yakaribisha tamko la viongozi wa G20 ikiwa ni pamoja na kuupokea Muungano wa Afrika

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari katika mkutano wa G20 mjini New Delhi, India.
UN India/Ruhani kaur
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akitoa maelezo kwa waandishi wa habari katika mkutano wa G20 mjini New Delhi, India.

UN yakaribisha tamko la viongozi wa G20 ikiwa ni pamoja na kuupokea Muungano wa Afrika

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa umekaribisha kupitishwa leo kwa Azimio la Viongozi wa Kundi la Nchi 20 zenye Maendeleo Makubwa ya Kiuchumi Duniani (G20) New Delhi, na kulielezea kama mfano wa uongozi bora wakati wa mgawanyiko mkubwa duniani. 

Viongozi wa dunia, wanaokutana katika mji mkuu wa India kwa ajili ya mkutano wa kila mwaka wa G20, wamefikia makubaliano alasiri ya leo Jumamosi Septemba 9, 2023 kwa saa za India kuhusu tamko hilo, ambalo linahusu masuala kuanzia mabadiliko ya tabianchi na ukuaji wa kijani hadi usawa wa kijinsia na kukabiliana na ugaidi. 

Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema Umoja wa Mataifa unakaribisha hasa lugha ya tamko kuhusu kuharakisha maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). 

"Tunafuraha hasa kusoma kuhusu ahadi huko, na jinsi ni lazima sote tutie nguvu tena na kuwekeza tena katika Malengo ikiwa tutakaribia hata kuyatimiza kufikia tarehe iliyolengwa ya 2030," amesema. 

Bwana Dujarric amesema kupitishwa kwa tamko hilo kwa makubaliano baada ya mazungumzo ya muda mrefu - hasa katika enzi ya mgawanyiko wa kimataifa - ilikuwa ni heshima kwa juhudi za India, ambayo kwa sasa inashikilia urais wa G20. 

"Pia inaonesha jukumu la India kama kiongozi wa Eneo la Kusini la Ulimwengu na nchi zinazoendelea. Hii inaangazia uwezo wa India kama mjenzi wa daraja, kisiasa na kijiografia.

Bara la Afrika katika G20 

Wakati huo huo, G20 pia imekubali leo kuukubali Muungano  wa Afrika (AU) kama mwanachama wake mpya zaidi, uamuzi uliokaribishwa na Umoja wa Mataifa. 

"Hii ni taswira ya kuongezeka kwa ushawishi na umuhimu wa Afrika katika hatua ya kimataifa," ameeleza Katibu Mkuu wa UN kupitia Msemaji wake na kuongeza, "Wakati sehemu kubwa ya usanifu wa kimataifa uliopo wa kimataifa ulipojengwa, sehemu kubwa ya Afŕika ilikuwa bado inatawaliwa na koloni na haikuwa na fuŕsa ya kusikilizwa sauti zao. Hii ni hatua nyingine ya kurekebisha usawa huo."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alikuwa amewasili New Delhi na kile alichokitaja kama "ombi rahisi lakini la dharura" kwa viongozi wa G20: kuja pamoja kutatua changamoto kubwa za ubinadamu. 

Amesisitiza kuwa uongozi wa kimataifa ni muhimu hasa katika hatua za hali ya hewa na maendeleo endelevu. 

Mapema leo, Bwana Guterres amehutubia kikao cha kilele kinachohusu masuala ya tabianchi na mazingira, na kuwataka viongozi waoneshe nia kubwa ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuunga mkono haki ya tabianchi. Wanachama wa G20 kwa sasa wanachangia 80% ya uzalishaji wa hewa chafuzi duniani.