Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya watu 43 Goma, OHCHR yatoa tamko

Mchoro wenye ujumbe nchini DRC
UN/Esther Nsapu
Mchoro wenye ujumbe nchini DRC

Mauaji ya watu 43 Goma, OHCHR yatoa tamko

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, (OHCHR) imesema imekumbwa na hofu kubwa juu ya taarifa za vifo vya watu takribani 43 huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, vifo vilivyotokea wakati wa maandamano dhidi ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine siku ya Jumatano ambako pia watu 56 walijeruhiwa.

Msemaji wa OHCHR mjini Geneva, Uswisi, Ravina Shamdasani amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa miongoni mwa waliouawa ni polisi mmoja akiongeza kuwa “tumepokea ripoti zinazodokeza kuwa pengine idadi ya watu waliokufa kwenye tukio hilo inaweza kuwa ni kubwa.”

Uchunguzi uwe wa kina na usiegee upande wowote

Maandamano hayo, kwa mujibu wa Bi. Shamdasani,  yaliandaliwa dhidi ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, jeshi la kikanda la jumuiya ya Afrika Mashariki, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.

Bi. Shamdasani amesema wanatambua tangazo la serikali kuwa uchunguzi dhidi ya tukio hilo umeanza na “tunatoa wito uchunguzi uwe wa kina, fanisi na usiegemee upande wowote.”

Amesema kwa uchunguzi huo uende sambamba na kuchunguza matumizi ya nguvu kutoka vikosi vya usalama na kwamba watakaobainika kukiuka kanuni lazima wawajibishwe bila kujali wanatoka upande gani.

Watu 222 wanashikiliwa wakiwemo wanawake na watoto

Afisa huyo wa OHCHR amesema takribani watu 222 wanashikiliwa na polisi wakiwemo wanawake na watoto.

“Tuna wasiwasi juu ya hatari ya uwezekano mkubwa wa ukiukwaji wa haki katika mazingira hayo. Ni muhimu haki za wao walioswekwa korokoroni ziheshimiwe, ikiwemo mchakato wa haki, na mamlaka husika zihakikishe watu hao hawanyimwi haki ya kuonana na Ofisi ya pamoja ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini humo,” amesema Bi. Shamdasani.

Watu wana haki ya kuandamana hata kama ni dhidi ya UN

Amekumbusha kuwa watu wana haki ya kutoa maoni yao kwa uhuru na kukusanyika kwa amani, hata kama maandamano hayo yalikuwa dhidi ya Umoja wa Mataifa na watendaji wengine. “Mamlaka lazima zifanikishe haki ya watu kukusanyika kwa amani.”

Amemnukuu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk akitoa wito kwa mamlaka kuhakikisha hatua za siku za usoni zinazochukuliwa na vikosi vya usalama kwenye mikusanyiko ya umma zinazingatia sheria na kanuni za kimataifa za haki za binadamu.

Na ni kwa mantiki hiyo amesema wako tayari kushirikiana na mamlaka DRC kufanikisha jambo hilo.