Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi katika Wilaya 5 DRC waahirishwa hadi Machi mwakani

Eneo la mashariki mwa DRC ambako pia kuna jimbo la Kivu Kaskazini limekuwa na matukio ya mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami. Walinda amani wa MONUSCO (Pichani) wamekuwa wakifanya doria ili kuhakikisha kuna amani.
UN /Kevin Jordan
Eneo la mashariki mwa DRC ambako pia kuna jimbo la Kivu Kaskazini limekuwa na matukio ya mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami. Walinda amani wa MONUSCO (Pichani) wamekuwa wakifanya doria ili kuhakikisha kuna amani.

Uchaguzi katika Wilaya 5 DRC waahirishwa hadi Machi mwakani

Haki za binadamu

Tume huru ya taifa ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, CENI imesogeza mwezi Machi mwakani upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi mkuu kwenye wilaya tano nchini humo kwa sababu ya Ebola na ukosefu wa usalama.

Taarifa ya CENI iliyotolewa leo kwenye mji mkuu wa DRC, Kinshasa imetaja wilaya ambazo uchaguzi umeahirishwa kuwa ni Beni, Beni Mjini, Butembo Mjini katika jimbo la Kivu Kaskazini na mji wa Yumbi ulioko jimbo la Mai-ndombe.

CENI imefafanua sababu ya kuahirisha uchaguzi mjini Yumbi kuwa ni matukio ya tarehe 14 na 15 mwezi huu wa Desemba ambapo vifaa vyote vinavyohusiana na uchaguzi ikiwemo nyaraka vilivyochomwa moto na vifaa vya tume vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye bohari viliporwa.

Na katika wilaya hizo zilizopo jimbo la Kivu Kaskazini, CENI imeahirisha uchaguzi kwababu ugonjwa wa Ebola unakwamisha harakati za uchaguzi sambamba na mashambulio yanayofanywa na vikundi vilivyojihami.

Hata hivyo uchaguzi wa rais, wabunge na magavana katika maeneo mengine  utaendelea kama kawaida tarehe 30 mwezi huu wa Desemba.

Halikadhalika CENI imesema matokeo ya uchaguzi yatatangazwa tarehe 15 mwezi Januari mwakani na Rais ataapishwa tarehe 18 mwezi huo huo wa Januari.

Awali uchaguzi mkuu DRC ulikuwa ufanyike tarehe 27 mwezi Novemba mwaka 2016, ukasogezwa  mbele kwa ahadi ya kufanyika mwishoni mwa mwaka jana 2017.

Hatimaye ilipangwa kuwa ungalifanyika tarehe 23 mwezi huu wa Desemba, lakini hata hivyo ukaahirishwa hadi tarehe 30 mwezi huu.

 

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.