Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawezesha wanahabari watoto kupasha umma kuhusu changamoto za maji DRC

Sostine ambaye ni mchuuzi wa maji katika mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC anamweleza mwanahabari mtoto Liesse ya kuwa hulazimika kuweka dawa kwenye madumu ya maji kwa sababu maji ya Ziwa Kivu yana taka.
UNICEF VIDEO
Sostine ambaye ni mchuuzi wa maji katika mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC anamweleza mwanahabari mtoto Liesse ya kuwa hulazimika kuweka dawa kwenye madumu ya maji kwa sababu maji ya Ziwa Kivu yana taka.

UNICEF yawezesha wanahabari watoto kupasha umma kuhusu changamoto za maji DRC

Afya

Hii leo ni siku ya maji duniani na ninakupeleka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako huko mtoto Liesse mwenye umri wa miaka 17 amefuatilia upatikanaji wa maji safi ya kunywa kwenye eneo la Goma jimboni Kivu Kaskaizini baada ya kupatiwa mafunzo ya uandishi wa habari na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF na hatimaye taarifa yake kutangazwa na Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo

Video ya UNICEF inaanza kwa kuonesha msikilizaji akirekebisha redio yake kupata masafa ya Radio Okapi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kisha anaonekana Liesse na kamera yake akikutana na Sostine, mchuuzi huyu wa maji akikokota kwa baiskeli madumu yaliyojaa maji aliyoteka kutoka Ziwa Kivu hapa Goma, jimboni Kivu kaskazini.

Sostine anamweleza mwanahabari mtoto Liesse ya kuwa“kila asubuhi nachukua baiskeli yangu na kisha nakwenda ziwani kuteka maji. Kutokana na taka zilizotupwa kwenye ziwa inabidi niweka dawa ya kusafisha maji kwenye madumu halafu hayo maji nakwenda kuuza. Nafanya hii kazi hapa kwenye mji wetu wa Goma kwa sababu katika huu mji wetu kuna shida ya kupata maji safi na salama.”

Dawa anayosema anaweka ni Klorini ya kutakatisha maji kwani kwenye ziwa kuna uchafu.

Ripoti hii ya Liesse iko hewani kupitia Radio Okapi kwa ufadhili wa UNICEF kwa kuwa kila wiki watu milioni 24 huwasha redio zao kusikiliza na sasa wasikilizaji wametegesha redio zao na Liesse kupitia matangazo hayo anasema, habari zenu nyote mimi ni Liesse. Nimekuwa kwenye mji wa Goma kwa miaka mitatu. Tunahitaji maji na tunahitaji mabomba yanayotoa maji vizuri.”

Na kisha ana ujumbe  “mimi mwanahabari kijana napenda Waziri wa Mazingira ajaribu kutatua haya matatizo kwa sababu tukiwa na maji safi na salama itatusaidia, au sio? Kwa sababu wanasema maji ni uhai. Tunahitaji maji kila mahali. Hospitalini, nyumbani, shuleni ambako kuna wasichana wengi. Naona maji ni mtambuka katika maisha yetu, ni kila kitu.”