Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita na njaa vinaweza kusambaratisha Sudan – Mkuu wa OCHA

Wanawake wakipanga foleni kwa ajili ya kupokea msaada wa fedha wa WFP katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Darfur Kusini, Sudan.
© WFP/Leni Kinzli
Wanawake wakipanga foleni kwa ajili ya kupokea msaada wa fedha wa WFP katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Darfur Kusini, Sudan.

Vita na njaa vinaweza kusambaratisha Sudan – Mkuu wa OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Vita inayoendelea nchini Sudan inachochea dharura kubwa ya kibinadamu ambapo vita na njaa, magonjwa na watu kufurushwa makwao vilivyofuatia sasa  inatishia ‘kutafuna’ nchi nzima, amesema Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Martin Griffiths. 

Taarifa iliyotolewa na OCHA hii leo jijini New York, Marekani imemnukuu mkuu wa ofisi hiyo Martin Griffiths akisema kuwa mapigano makali yaliyoanzia mji mkuu wa Sudan, Khartoum na jimbo la Darfur katikati ya mwezi Aprili mwaka huu yamesambaa hadi Kordofan. 

Amesema katika mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kusini, Kadugli hifadhi ya vyakula imekwisha kwa kuwa mapigano na vizuizi njiani vinasababisha wahudumu wa misaada washindwe kufikia wenye njaa. 

Huko El Fula, mji mkuu wa jimbo la Kordofan Magharibi, ofisi za watoa misaada zimevamiwa na misaada imeporwa. 

Bwana Griffiths amesema hofu yake sasa ni usalama wa raia kwenye jimbo la Al Jazira wakati huu ambapo mzozo huo unasogelea eneo hilo tegemewa kwa uzalishaji wa chakula Sudan. 

Mkuu huyo wa OCHA amesema kadri mapigano yanavyoendelea, vivyo hivyo madhara yanayongezeka. Mamia ya maelfu ya watoto wana utapiamlo uliokithiri na wako hatarini kufa iwapo hawatapata tiba. 

WHO inawasaidia wahudumu wa afya wa Sudan kwa kuwapatia madawa muhimu, msaada wa manusura na vifaa vya upasuaji, na mafuta ili kudumisha huduma za afya.
© WHO/Lindsay Mackenzie
WHO inawasaidia wahudumu wa afya wa Sudan kwa kuwapatia madawa muhimu, msaada wa manusura na vifaa vya upasuaji, na mafuta ili kudumisha huduma za afya.

Magonywa ya kuambukizwa kwa vimelea kama vile Malaria, Kifaduro, Kidingapopo yanasambaa nchi nzima na yanatishia uhai kwa wale wenye waliodhoofishwa tayari na utapiamlo. 

Wagongwa hao hawawezi kupata matibabu kwani mapigano yamesambaratisha mfumo wa afya. 

Bwana Griffiths amesema vita ya muda mrefu itapoteza kizazi cha watoto kwani mamilioni hawaendi shuleni, na watakumbwa na kiwewe na kusalia na kovu la vita katika maisha yao. 

Amesema ripoti za kwamba watoto wanatumika pia kwenye mapigaon ni za kuchukiza. 

Mkuu huyo wa OCHA ametaka pande kinzani kuweka mbele maslahi ya wananchi Sudan badala ya uroho wao wa madaraka, watoa misaada wapatiwe ruhusa ya kufikisha mahitaji na zaidi ya yote jamii ya kimataifa ipatie janga la Sudan udharura unaohitajika.