Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jumuiya ya kimataifa haipaswi kuupa kisogo ufurushwaji mkubwa zaidi wa watu Sudan

Timu za IOM zinatathmini mahitaji ya wakimbizi wa Sudan kwenye mpaka wa Chad-Sudan.
IOM 2023
Timu za IOM zinatathmini mahitaji ya wakimbizi wa Sudan kwenye mpaka wa Chad-Sudan.

Jumuiya ya kimataifa haipaswi kuupa kisogo ufurushwaji mkubwa zaidi wa watu Sudan

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, Amy Pope, kupitia taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, N'Djamena, Chad na Port Sudan nchini Sudan, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za ufadhili, na kutowaacha mamilioni ya raia wanaobeba mzigo mkubwa wa vita ya miezi tisa nchini Sudan. Mwitikio ulioratibiwa na unaoendelea wa kibinadamu unahitajika haraka kushughulikia mahitaji yanayoongezeka ya janga kubwa zaidi la watu kuhama makazi.

Watu milioni 7.7 wamelazimika kukimbia makazi yao nchini Sudan tangu mapigano yalipoanza tarehe 15 Aprili mwaka wa 2023, kwa mujibu wa IOM's Takwimu za IOM za ufuatiliaji wa ufurushwaji , Ripoti ya DTM, iliyotolewa jana tarehe 16 Januari. Watu milioni sita kati ya hao wameyakimbia makazi yao ndani ya Sudan, huku wengine milioni 1.7 wakikimbilia nchi jirani za Sudan Kusini, Chad, Ethiopia, Misri, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Libya. 

Bi Pope kufuatia ziara yake ya hivi majuzi Mashariki mwa Chad ambako alijionea mwenyewe, athari za mzozo kwa watu waliokimbia makazi yao anasema, "kusitishwa kwa mapigano nchini Sudan kunahitajika haraka ili kuwawezesha watu kujenga upya maisha yao kwa heshima. Hatupaswi kugeuka nyuma juu ya mateso ya mamilioni ya watu walioathiriwa na migogoro hiyo yenye uharibifu. Sasa, zaidi ya hapo awali, tunahitaji usaidizi wote unaowezekana ili kuendelea kutoa usaidizi wa kibinadamu wa kuokoa maisha na kuelekea kwenye afueni na masuluhisho ya muda mrefu”.

Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.
© UNICEF/Adriana Zehbrauskas
Wanawake na wasichana wakichota maji kwa ajili ya familia zao katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao nchini Sudan.

Zaidi ya hayo, Bi. Pope amesema kuwa mwaka huu 2024, IOM inaomba dola milioni 307 kufikia watu milioni 1.2 walioathiriwa na mzozo huu, wakiwemo wakimbizi wa ndani, wakimbizi, waliorejea na raia wa nchi zinazoendelea. Zaidi ya 600,000 kati ya wale wanaokimbia ghasia hizo wako Mashariki mwa Chad. Kati ya hao, zaidi ya 136,000 ni Wachadi waliorejea hivi karibuni waliokuwa wakiishi Sudan lakini walilazimishwa na vita hivyo kurejea Chad, pamoja na wafanyakazi wahamiaji kutoka nchi nyingine na familia zao. 

Bi. Pope amehitimisha kuwa, IOM hadi sasa imesaidia zaidi ya watu milioni moja nchini Sudan na nchi jirani. Hii ni pamoja na kutoa msaada wa pesa taslimu kwa karibu watu 73,000 na kuwezesha usafirishaji wa 150,000 hadi maeneo salama katika nchi jirani. IOM na washirika wamekuwa na wanaendelea kutoa huduma muhimu za afya, ulinzi, maji, usafi wa mazingira, usafi na makazi kwa wale walio katika mazingira magumu na vita.

Soma zaidi.