Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto walio hatarini Sudan ni zaidi ya idadi ya watu wote Sweden, Ureno au Rwanda - UNICEF 

Watoto wa Sudan waliopoteza makazi yao wakiwa kwenye makazi ya muda.
© UNICEF/Ahmed Elfatih Mohamdee
Watoto wa Sudan waliopoteza makazi yao wakiwa kwenye makazi ya muda.

Watoto walio hatarini Sudan ni zaidi ya idadi ya watu wote Sweden, Ureno au Rwanda - UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), James Elder amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba "watoto wengi zaidi nchini Sudan wanahitaji usaidizi wa kuokoa maisha kuliko hapo awali", huku watoto milioni 13.6 wakihitaji msaada wa haraka.

Akifanya kulinganisha idadi hiyo ya watoto wenye uhitaji wa kuokoa maisha nchini Sudan, Msemaji wa UNHCR amesema kwamba, "Hiyo ni zaidi ya idadi ya watu wote wa Sweden, Ureno au Rwanda," 

Kwa mujibu wa ripoti zilizopokelewa na UNICEF, mamia ya wasichana na wavulana wameuawa katika mapigano hayo. "Ingawa hatuwezi kuthibitisha haya kutokana na ukubwa wa vurugu, pia tuna ripoti kwamba maelfu ya watoto wamejeruhiwa," Bwana Elder amesema.  

Msemaji huyo wa UNICEF ameongeza kwamba taarifa za watoto kuuawa au kujeruhiwa ni za wale tu waliokuwa na mawasiliano na kituo cha matibabu, akimaanisha kwamba hali halisi “bila shaka ni mbaya zaidi” na inachangiwa na ukosefu wa huduma za kuokoa maisha ikiwa ni pamoja na lishe, maji salama, na afya. 

Bwana Elder ametahadharisha kwamba "mambo haya yote kwa Pamoja yanahatarisha kuwa hukumu ya kifo, hasa kwa walio hatarini zaidi". 

UNICEF imetoa wito wa ufadhili wa dola milioni 838 za kimarekani kushughulikia mzozo huo, ongezeko la dola milioni 253 tangu mzozo wa sasa uanze Aprili ili kuwafikia watoto milioni 10. Bwana Elder amesisitiza kuwa ni asilimia 5 tu ya kiasi kinachohitajika kilichopokelewa hadi sasa, na kwamba bila chakula cha matibabu na chanjo ambazo fedha hizi zingeweza kupata, watoto wangekuwa wanakufa. 

WHO 

Naye Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, Tarik Jašarević amesema hali mbaya ya huduma za afya Sudan imechochewa na kuendelea kwa mashambulizi kwenye vituo vya matibabu. Tangu kuanza kwa vita tarehe 15 hadi 25 Mei, WHO imethibitisha mashambulizi 45 dhidi ya huduma ya afya, ambayo yalisababisha vifo vya watu wanane na majeruhi 18. 

Pia ametaja ripoti za uvamizi wa kijeshi katika hospitali na maghala ya vifaa vya matibabu, jambo ambalo liliwafanya watu wenye uhitaji kupata dawa za magonjwa sugu au matibabu ya malaria kushindwa kufanya hivyo. Bwana Jašarević amekumbushia kwamba mashambulizi dhidi ya huduma ya afya ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na lazima yakome.