Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pande zinazohasimiana Sudan sitisheni uhasama kuwanusuru watoto: UN

El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, unawahifadhi watu wengi waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo wa kikabila nchini Sudan. (Maktaba)
© IOM/Muse Mohammed
El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, unawahifadhi watu wengi waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo wa kikabila nchini Sudan. (Maktaba)

Pande zinazohasimiana Sudan sitisheni uhasama kuwanusuru watoto: UN

Amani na Usalama

Kuongezeka kwa kasi kwa uhasama nchini Sudan kuna athari kwa kiasi kikubwa watoto, ambao tayari wameathiriwa sana na migogoro ya muda mrefu, uharibifu wa nchi kutokana na migogoro hiyo na hali mbaya ya kibinadamu. Wawakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kuhusu watoto na migogoro ya silaha na ukatili dhidi ya watoto wanaunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa pande zote zinazohasimiana kusitisha mapigano mara moja na kuhakikisha kuwa hatua zinazohitajika zinachukuliwa kulinda raia na hasa watoto katika mazingira ya shughuli za mapambano.

Katika taarifa yao ya pamoja maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wamesema, "Maisha, ulinzi na ustawi wa watoto lazima view kipaumbele kuliko operesheni za mapigano, na tunatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano na kuhakikisha ulinzi kamili wa watoto wote. Wanachama wanapaswa kujiepusha zaidi na kushambulia miundombinu ya kiraia kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu, hasa ile inayoathiri watoto, hii ni pamoja na shule na vituo vya matibabu pamoja na mifumo ya maji na usafi wa mazingira".

Majeruhi na vifo vya raia

Maafisa hao wameongeza kuwa wanasikitishwa zaidi na idadi iliyoripotiwa ya raia waliouawa au kujeruhiwa katika mapigano, wakiwemo watoto, na mashambulizi dhidi ya hospitali na kunyimwa misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha kwa watu ambao tayari wanahitaji chakula, maji na vifaa vingine muhimu.

“Raia wote na haswa watoto lazima waweze kupata vifaa muhimu na kuhama kutoka maeneo ya mapigano.” Wamesisitiza katika tarifa yao.

Maafisa hao wa Umoja wa Mataifa pia wanakumbusha kwamba bila kujali majukumu yao, “kwa vyovyote vile watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wasihusishwe katika vita kwa kuwa kuajiri na kutumia watoto vitani ni marufuku chini ya sheria za kimataifa.”

Wamekumbusha kwamba nchi zote wanachama ambazo zimetia saini na kuridhia mkataba wa Haki za mtoto na itifaki zake za hiari, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa watoto katika vita, lazima zihakikishe suluhu zinawalenga watoto katika migogoro inayoendelea na kuwalinda watoto wakati wa shughuli zao za mapambano.

Sheria na misingi ya kimataifa lazima iheshimiwe

Maafisa hao wanaopigania maslahi ya watoto wamenasisitiza umuhimu kwamba kanuni zote za sheria ya kimataifa ya kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu zifuatwe kikamilifu, ikiwa ni pamoja na zile za uwiano, tahadhari na tofauti katika kuwalenga raia na wanajeshi na vitu wakati wa kufanya operesheni, haswa wakati wa operesheni katika maeneo ya makaazi ya raia.

Kwa miongo kadhaa, watoto nchini Sudan tayari wamekuwa wakivumilia viwango vya ajabu vya ukatili na mateso.

Kukomesha uhasama na kupungua kwa mivutano ni hatua za kwanza za dharura za kuhakikisha ulinzi kamili wa watoto nchini humo bila kuchelewa. Wamehitimisha tarifa yao kwa kusema kwamba "Amani bado ni suluhisho bora la kukomesha ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto. Tunatoa wito kwa pande zote kutoa kipaumbele katika mazungumzo ya amani na kwa kufanya hivyo kujumuisha masharti mahususi ya watoto kulingana na mwongozo wa vitendo kwa wapatanishi wa kuwalinda watoto katika hali ya migogoro ya kivita,”