Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazingira duni sekta ya malezi yatishia haki za watu wenye ulemavu- Mtaalamu

Haki za watu wenye ulemavu zatishiwa na mazingira duni ya kazi kwa wahudumu
© Unsplash/Zhuo Cheng You
Haki za watu wenye ulemavu zatishiwa na mazingira duni ya kazi kwa wahudumu

Mazingira duni sekta ya malezi yatishia haki za watu wenye ulemavu- Mtaalamu

Haki za binadamu

Mijadala kuhusu hatma ya huduma za malezi katika karne hii ya 21 lazima zipatie kipaumbele mazingira ya kazi na fursa za ajira, la sivyo haki za watu wenye ulemavu zitakuwa mashakani, amesema Mtaalamu huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa hii leo.

Gerard Quinn, ambaye ni Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za watu wenye ulemavu amesema ajira zisizo na mwelekeo wa mtu kusonga mbele, ujira mdogo, mazingira duni ya kazi na bila fursa ya kukua kijamii kwenye sekta ya malezi si njia au mfumo wenye mnepo kama ambavyo COVID-19 ilidhihirisha.

Wahudumu wanawake wanaathirika zaidi

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za watu wenye ulemavu, (CRPD) mjini Geneva, Uswisi, Mtaalamu huyo ameanngazia zaidi mazingira yasiyo rafiki kwa wanawake wanaofanya kazi kwenye sekta ya huduma na malezi ya watu.

“Umaskini kubeba sura ya kike” ambapo wanawake wahudumu ndio wanaokuwa kwenye athari hasi zaidi- hauwezi kuendelea,” ameesma Bwana Quinn , akiongeza kuwa kuwa makini kuhusu haki kuna maanisha lazima tuwe makini na mfumo anuani ambao unawapatia uhalisia au unawakandamizi.

Bwana Quinn amesisitiza kuwa mijadala kuhusu haki za watu wenye ulemavu haukuweko kwenye ombwe, na lazima ujumuishe haki za wanawake na vile vile kuwafanya watoa huduma kwenye sekta hiyo inayojipatia mabilioni ya dola – kutambua kuwa wana dhimay a kufanikisha haki za binadamu.

Ulemavu na mizozo

Kwa mujibu wa Bwana Quinne, CRDP umezingatia maeneo kadhaa kuanzia tabianchi, mizozo, maendeleo na demokrasia.

Mtaalamu huru huyo amedokezea ripoti yake ijayo kuhusu mizozo na ulemavu itakayozinduliwa mwezi Oktoba mwaka huu, akisema alishtushwa baada ya kubaini kuwa ni asilimia 6 tu ya mikataba ya amani duniani iliyopitishwa katika miaka 30 iliyopita inataja ulemavu.

Amelaani fursa hiyo iliyopotezwa ya kujenga mustakabali jumuishi wakati muhimu wa jamii yoyote ile kisiasa, akisisitiza kuwa hali hiyo lazima ibadilike kama ilivyofanyika hoja ya uombaji rasmi msamaha, uwajibikaji wa wahalifu, fidia na kumbukizi ya makosa ya zamani yaliyolenga kuengua ulemavu.

Sera za UN kuhusu miongozo katika sekta ya huduma na malezi

Akizungumza kwenye mkutano huo kwa niaba ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR), Bi. Asako Hattori amesema  kwamba ofisi hiyo inaendelea kufanyia kazi hoja ya huduma jumuishi na mifumo ya usaidizi na kwamba hivi sasa inaandaa ripoti ya mienendo mizuri ya jamii kujumuisha watu wenye ulemavu, ripoti ambayo itawasilishwa kwenye Baraza la Haki za binadamu la UN mwaka ujao.

Amesisitiza kuwa tangu mwezi Aprili mwaka huu, ofisi hiyo imekuwa inachangia katika utungaji wa sera ya UN kuhusu malezi na huduma.

Kwa mujibu wa OHCHR kuna takribani watu bilioni moja wenye ulemavu duniani kote, au asilimia 15 ya wakazi wote wa dunia.

Mkutano huu utaendelea hadi mwanzoni mwa mwezi ujao na utafanyia tathmini ripoti za haki za binadamu za Andorra, Austria, Ujerumani, Israel, Malawi, Mauritania, Mongolia na Paraguay.