Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanya na Hasi za miaka 15 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu

Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.
© UNOCHA/Maxime Nama
Waichana walio na ulemavu wakicheza mpira wa vikapu nchini DRC.

Chanya na Hasi za miaka 15 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu

Haki za binadamu

Mkutano wa 15 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, CRPD umeanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kwa lengo la kutathmini miaka 15 tangu kupitishwa kwa mkataba huo ulioridhiwa na mataifa 185.

Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kiwango hicho cha uridhiaji kinachochea ahadi ya jamii ya kimataifa ya kufanikisha ujumuishi, upatikanaji wa huduma na dunia endelevu kwa wote.

Mafanikio ya Mkataba ni dhahiri

Amesema mafanikio ya kutiwa Saini na kuridhiwa kwa mkataba huo kwa kiwango kikubwa ni Dhahiri kwa kuwa, “asilimia 92 ya nchi wanachama wa mkataba huo wamepitisha sheria za kitaifa za maslahi ya watu wenye ulemavu ikiwemo vipengele vya ujumuishi. Zaidi ya asilimia 60 wamechukua hatua za kupiga marufuku ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu kwenye soko la ajira.”

Asilimia 90 wamepitisha sheria za kulinda haki za Watoto wenye ulemavu hususan kwenye elimu, na idadi ya nchi ambazo zina vifaa vya shule kwa Watoto wenye ulemavu nayo imeongezeka maradufu.

Mwanafunzi mwenye ulemavu akiwa katika uwanja wa michezo nchini Brazil
© UNICEF Brazil
Mwanafunzi mwenye ulemavu akiwa katika uwanja wa michezo nchini Brazil

COVID-19 imerudisha nyuma mafanikio na kufichua pengo la ukosefu wa usawa

Katibu Mkuu amesema licha ya mafanikio  yaliyopatikana, janga la COVID-19 limekuwa ‘mwiba’ kwani limefichua changamoto mpya kwa watu wenye ulemavu.

“Hata kabla ya janga, kulikuwa na changamoto kwani ilikuwa ni kwa nadra watu wenye ulemavu wananufaika na huduma za afya, elimu, na mbinu za kujipatia kipato.

Amesema COVID-19 ilipobisha hodi, watu wenye ulemavu waliathirika zaidi. “Na huu ni ukweli kwa majanga mengine. Kwenye vita, watu wenye ulemavu mara nyingi wanashindwa kukimbia na hawapati misaada ya kibinadamu. Vita ya Ukraine imechochea uhaba wa chakula, nishati na fedha, na hii imeathiri zaidi watu wenye ulemavu.”

Ametaka nchi wanachama zitimize wajibu wao kwa mujibu wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu kwa kuhakikisha wanalindwa kwenye mizozo na wanapata misaada ya kibinadamu.

Kote ulimwenguni takriban watu milioni 93 chini ya umri wa miaka 15 wanaishi na ulemavu.
© UNICEF/Vanda Kljajo
Kote ulimwenguni takriban watu milioni 93 chini ya umri wa miaka 15 wanaishi na ulemavu.

Lakini mwelekeo endelevu ni upi? COP15 ya CRPD ifanye nini?

Guterres amesema mkutano huu wa siku tatu wa COP15 ya CRPD una majukumu makuu matatu ya kusongesha haki za watu wenye ulemavu wakati huu majanga yakizingira kila kona.

Mosi: Nguvu ya teknolojia kusongesha ujumuishi

Katibu Mkuu amesema teknolojia inaweza kusongesha usawa wa kupata furs ana kuvunja vikwazo na hivyo kuwa na mazingira jumuishi.

“Zaidi ya watu bilioni moja duniani kote wanahitaji teknolojia saidizi, lakini nchi nyingi hazina vifaa hivyo kwa kila mtu,” amesema Guterres.

Teknolojia hizo ni kama vile za kumwezesha kiziwi kusikia au mtu mwenye ulemavu wa viungo kusonga kutoka eneo moja hadi jingine. 

Pili: kusongesha uwezeshaji kiuchumi na ujasiriamali kwa watu wenye ulemavu

Katibu Mkuu ametaja umuhimu wa kuangazia uwezeshaji wa watu wenye ulemavu kiuchumi na ushiriki wao kwenye harakati za kijasiriamali ili kuweko na usawa kwa watu wenye ulemavu katika soko la ajira.

“Hii ni muhimu sana kuliko wakati wowote kwa kutambua madhara ya janga la COVID-19 kwa watu wenye ulemavu na ukosefu wa usawa unaoota mizizi wakati huu wa kujikwamua,” amesema Guterres.

Chama cha watu wenyeulemavu nchini Mali kinafundisha wanachama wake jinsi ya kuzalisha na kutengeneza bidhaa kama vile sabuni na kushona viatu. (Picha maktaba-2017)
MINUSMA/Sylvain Liecht
Chama cha watu wenyeulemavu nchini Mali kinafundisha wanachama wake jinsi ya kuzalisha na kutengeneza bidhaa kama vile sabuni na kushona viatu. (Picha maktaba-2017)

Tatu: Ongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu kwenye hatua kwa tabianchi

 Guterres anasema watu wenye ulemavu wako mara 2 hadi 4 zaidi ya kufa wakati wa vimbunga, Tsunami na majanga mengine ya kiasili.

Wakati huo huo, watu hao ni rasilimali ya kipekee ya ufahamu na uzoefu wa kujenga jamii zenye mnepo zaidi.

“Sasa tuone ni vipi mashirika yao na wao wenyewe wanashiriki katika hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Katibu Mkuu.

Hata hivyo amesema ushirikiano baina ya serikali, mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia na sekta binafsi ni muhimu kufanikisha vipaumbele hivyo vitatu na zaidi ya yote, “msingi wa ushirikiano huu lazima uwe ushiriki halisi wa watu wenye ulemavu kutoka pande zote na ujumuishi wao katika mchakato wa kupitisha maamuzi.”

Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuongoza kwa mfano kuptia mkakati wake wa ujumuishi wa watu wenye ulemavu ambao umeingia mwaka wa tatu. “Tunataka Umoja wa Mataifa uwe muaijri pendwa kuanzia makao makuu hadi mashinani.”