Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandishi ya nukta nundu ni muarobaini wa kujumusha kwenye  jamii wasioona na wenye uoni hafifu

Mshiriki akitumia kifaa chenye maandishi ya nukta nundu wakati wa kikao cha 10 cha nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa  haki za watu wenye ulemavu 2017
UN /Manuel Elias
Mshiriki akitumia kifaa chenye maandishi ya nukta nundu wakati wa kikao cha 10 cha nchi wanachama wa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu 2017

Maandishi ya nukta nundu ni muarobaini wa kujumusha kwenye  jamii wasioona na wenye uoni hafifu

Haki za binadamu

Leo ni siku ya kimataifa ya maandishi ya nukta nundu ambayo hutumiwa na watu wenye ulemavu wa kutoona.

Kwa mara ya kwanza Umoja wa Mataifa unaadhimisha rasmi maadhimisho hayo kwa kutambua umuhimu wa machapisho ya nukta nundu kama njia muhimu ya mawasiliano kwa wasioona na pia kuwawezesha kundi hilo na wale wenye uoni hafifu kupata haki yao ya msingi ya mawasiliano.

Nukta nundu ni nini?

Nukta nundu ni muwasilisho wa herufi kwa njia inayoshikika au kutambulika kwa vidole ambapo herufi na namba au hata noti za muziki na alama za kisayansi zinachorwa kiasi kwamba mtu asiyeona au mwenye uoni hafifu anaweza kutambua na kusoma kama kawaida.

Mbinu hii inatokana na mgunduzi wake Louise Braille kutoka Ufaransa ambaye aliigundua karne ya 19.

Mtu akisoma kwa kutumia maandishi ya nukta nundu
UN/Eskinder Debebe
Mtu akisoma kwa kutumia maandishi ya nukta nundu

Matumizi ya nukta nundu huwezesha kundi hilo kusoma vitabu na majarida na hivyo kuimarisha ubobezi wao, uhuru na usawa katika nyanja mbalimbali.

CRPD inasemaje?

Ibara ya 2 ya mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu inataja nukta nundu kama mbinu muhimu kwenye elimu, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, kupata taarifa na mawasiliano mbalimbali.

Halikadhalika nukta nundu inasaidia ujumuishaji kwenye jamii kwa watu wasioona na wenye uoni hafifu kama ilivyobainishwa katika ibara ya 21 na 24 ya mkataba huo wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, au CRPD.

Nchini Tanzania hali iko vipi?

Nchini Tanzania matumizi ya maandishi ya nukta nundu ni jambo la kawaida kwenye taasisi za elimu ambapo Amon Mpanju, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Katiba nchini humo, ambaye pia ni mlemavu wa kwanza wa macho kushika wadhifa wa juu wa uongozi nchini  humo ameieleza idhaa hii kuwa kanuni na sheria nchini humo zinatambua maandishi ya nukta nundu kama njia rasmi ya mawasiliano kwa wasioona na wenye uoni hafifu. "Nashukuru Umoja wa Mataifa kwa kutambua na kutenga siku hii Januari 04 kuwa siku ya kimataifa ya maandishi ya nukta nundu," amesema Mpanju akifafanua kuwa nchini Tanzania kuna shule lukuki kwa wasiioona na hata shule jumuishi.

Shule za kufundishia wasiioona Tanzania ni  nyingi- Amon Mpanju

Ametaja Chuo cha Patandi mkoani Arusha nchini Tanzania kuwa kinatoa mafunzo kwa walimu wa wanafunzi wasioona, "na tunatumia nukta nundu hadi Chuo Kikuu na kuna maprofresa wasioona na hiki ni kithibitisho kuwa kuwa mlemavu wa kutoona si mwisho wa maisha, unaweza kuwasiliana na kusoma vile utakavyo." 

Hata hivyo amesema hivi sasa wanaandaa mwongozo kwa mujibu wa sheria na mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha majengo yanakuwa ni rafiki kwa watu wote wenye ulemavu wakiwemo wasioona.