Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yazindua mkakati wake wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye nyanja zote

Chama cha watu wenyeulemavu nchini Mali kinafundisha wanachama wake jinsi ya kuzalisha na kutengeneza bidhaa kama vile sabuni na kushona viatu. (Picha maktaba-2017)
MINUSMA/Sylvain Liecht
Chama cha watu wenyeulemavu nchini Mali kinafundisha wanachama wake jinsi ya kuzalisha na kutengeneza bidhaa kama vile sabuni na kushona viatu. (Picha maktaba-2017)

UN yazindua mkakati wake wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye nyanja zote

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa leo umezindua mkakati wake wa ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali kama mojawapo ya hatua za kutekeleza kwa vitendo kwa mfano ahadi yake ya kutomwacha nyuma mtu yeyote kwenye utekelezaji wa ajenda 2030.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametangaza uzinduzi huo leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 12 wa nchi wanachama wa mkataba wa haki za watu wenye ulemavu, CRPD ulioanza leo.

Bwana Guterres amesema msingi wa kuanzisha mkakati huo ni baada ya ripoti iliyodhihirisha kuwa hali ya ujumuishi wa watu wenye ulemavu ndani ya chombo hicho inatisha, kuanzia makao makuu hadi katika ofisi za uwakilishi wa chombo hicho akisema kuwa kuna kutokuelewa ni jinsi gani Umoja huo unapaswa kutekeleza majukumu yake kuhusiana na ujumuishi.

Amegusia pia mantiki ya uamuzi wa kuanzisha mkakati huo kuwa ni maneno ya msichana mkimbizi mwenye mtindio wa ubongo kutoka Syria Nujeen Mustapha ambaye alipohutubia Baraza la Usalama wiki chache zilizopita alitaka kauli ya Umoja wa Mataifa ya hakuna mtu kuachwa nyuma itekelezwe kwa vitendo na si maneno tu, akisisitiza kuwa katu hawawezi kusubiri zaidi.

Ni kwa kuzingatia hayo Katibu Mkuu amesema,“huu si mkakati wa maneno, ni mkakati wa vitendo, hatua za kuongeza viwango vya utendaji vya Umoja wa Mataifa kuhusu ujumuishaji wa watu wenye  ulemavu katika ngazi zote na hatua za kuleta mabadiliko ya pamoja na ya dhati tunayohitaji.”

Amesema mkakati unataka ufuatiliaji na uwajibikaji na ukiangazia maeneo muhimu ikiwemo uongozi, mipango, upatikanaji wa huduma na kutoa wito kwa watu wenye ulemavu kufanya kazi na Umoja wa Mataifana wapatiwe usaidizi zaidi.

Guterres amesema, “nataka Umoja wa Mataifa uwe ni mwajiri anayechaguliwa na watu wenye ulemavu. Nataka operesheni zetu za kibinadamu, maendeleo na amani zitambue na zisongeshe haki za watu wenye ulemavu.”

Amesema ni lazima Umoja wa  Mataifa uwe wa kila mtu akiongeza kuwa, “ni jambo rahisi sana: Hatuwezi kuwa jukwaa la mabadiliko pindi watu wenye ulemavu hawawezi kupata fursa ya jukwaa la kuzungumza. Nategemea uungwaji mkono thabiti  kutoka kwa nchi wanachama ili kusongesha mkakati huu.”