Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana DRC wamesoma lakini ukosefu wa usalama unawatumbukiza kwenye umaskini – Kijana Florent

Florent Muhindo Nambura, Mkazi wa Beni jimboni Kivu Kaskazini akizungumza na George Musubao, mwandishi wetu DRC.
UN News/George Musubao
Florent Muhindo Nambura, Mkazi wa Beni jimboni Kivu Kaskazini akizungumza na George Musubao, mwandishi wetu DRC.

Vijana DRC wamesoma lakini ukosefu wa usalama unawatumbukiza kwenye umaskini – Kijana Florent

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, vijana kesho wataadhimisha siku yao duniani huku kiza kinene cha ukosefu wa usalama kikiwa kimetanda mashariki mwa taifa hilo la ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika.  

Wakati Umoja wa Mataifa ukipigia chepuo vijana kushika hatamu ya kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ikiwemo hatua kwa tabianchi, kutokomeza umaskini na ajira zenye hadhi, kwa vijana wa mashariki mwa DRC vuguvugu hilo linakumbwa na kikwazo cha usalama hata kama wawe wamepata elimu.  

Shuhuda wa changamoto hizo ni kijana mkazi wa Beni jimboni Kivu Kaskazini na amefunguka hali halisi ilivyo akizungumza na George Musubao, mwandishi wetu DRC.   

Swali 1: Unaitwa nani?  

Kwa majina naitwa Florent Muhindo Nambura mimi ni moja ya vijana wa Beni jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC. 

Swali 2: Unafanya kazi gani? 

"Ninafanya kazi ya kununua kakao nahiyo kakao nayapeleka inji jirani kama kina UGANDA"  

 Swali 3: Kazi hii uliianza lini?  

"Kazi hii niliiaanza tangu nilipomaliza shule. Wazazi wangu waliona kwamba nimemaliza shule inanibidi kujitegemea nisingojee lolote toka huku na kule ndipo wakanifundisha kazi. Ni tangu mwaka 2018 ndio nafanya kazi hiyo ni kazi ambauo inanisaidia hadi leo ndio naendelea kushukuru walionifundisha kuifanya."  

Swali 4: Sasa kazi hii ina changamoto yoyote?  

"Ndio. Hivi sasa kazi haiendelezi vizuri. Kama ndani ya siku zilizopita ni kwa sababu ya ukosefu wa usalama. Tumekosa usalama tangu miaka mingi na hiyo kazi tunachukua kakao kutoka mashambani. Sasa huko tunakochukua kakao hali ya usalama imezidi kuwa mbayá na watu wanaendelea kuuawa. Na sisi huwa tunasafirisha kakao kutoka Beni hadi mjini Mpondwe ili ipelekwe Uganda. Sasa njiani kuna shinda nyingi, magari yanashambuliwa na kuchomwa moto na waasi. Maadui wanavamia barabara kila wakati na hicho ni kikwazo kikubwa kwa sisi kuendelea na kazi yetu. Ndani ya biashara hii tulikuwa tumechunga (tumeajiri) vijana na kuwapatia kazi lakini leo hii tumewaondoa baadhi yao na hawajui namna gani tena wataishi. Nyakati hali ilikuwa sawa, tuliajiri wenzetu vijana.”  

Swali 5: Una ujumbe gani kwa vijana kama wewe?  

"Vijana kama mimi nawaalika kuungana pia na wasipoteze matumaini waita kwa upendo. Hiyo upendo inamaanisha kwamba kama kuna vijana fulani wanaoongea na maadui wanaotukosesha usalama, hao vijana wakate mawasiliano na maadui pia waje tujiunge ili kuona namna gani pamoja tutaweza kurejesha amani inchini kwetu DRC. Nina imani kwamba sisi vijana tukiungana tutarejesha amani kwetu. Vijana wengi wanakunywa pombe na kuangaika pande zote kutafuta maisha ila warudi tuunge nguvu pamoja tutaendelea bila tatizo"  

Swali 6: Una wito gani kwa viongozi wa DRC na Umoja wa Mataifa? 

 "Kwa viongozi wa DRC na kwa Umoja wa Mataifa  natoa wito waone ni kwa namna gani wanaweza kurejesha usalama nchini kwetu. Tumeteseka hatuna mamlaka kufuata adui kwani hatushiki silaha ila ni serikali inayo silaha ambayo ina mamlaka kusaka adui. Hiyo serikali  tunaiita pia isaidie vijana wapate kazi kwani wengi wao wamemaliza shule ila hawana lolote hawajui vipi kufanya kazi. Na Umoja wa Mataifa waone namna gani utasaidia vijana wa Beni ila wao pia waishi kama vijana wanavyoishi katika inchi zingine"  

 
Ripoti hii imeandaliwa na George Musubao, UN News DRC .