Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama huimarisha afya yao na ya mama - Wanaharakati Kenya

Kina mama kutoka Kenya ambao wananyonyesha watoto wao, wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa wiki ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kunyonyesha.
UN News/Thelmaa Mwadzaya
Kina mama kutoka Kenya ambao wananyonyesha watoto wao, wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa wiki ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kunyonyesha.

Unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama huimarisha afya yao na ya mama - Wanaharakati Kenya

Afya

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya uhai wanapiga hatua nzuri za kiafya kama anavyoelezea Kasha Mutenyo kwamba, "umuhimu wa kwanza wa kunyonyesha ni kwamba afya ya mtoto inaimarika na haugui kila wakati. Sio ghali, ni salama na hauhitaji vifaa vyovyote kumnyonyesha mtoto. Pia inamsaidia mama kupanga uzazi.”

Soundcloud

Uhamasisho wa umuhimu wa kunyonyesha hufanyika kila wiki ya kwanza ya Agosti kwa ushirikiano wa Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, na wizara ya afya ya Kenya. Kasha Mutenyo anaongeza kuwa kina mama wengine wa mara ya kwanza wanahitaji elimu ya ulezi na uzazi ili kuwatazama wana wao vizuri. 

Laura Kiige, afisa wa lishe, UNICEF.
UN News/Thelmaa Mwadzaya
Laura Kiige, afisa wa lishe, UNICEF.

UNICEF mstari wa mbele kusambaza elimu

UNICEF limekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya ulezi na afya ya uzazi kwa kina mama ili kuimarisha afya zao na za wana wao. Laura Kiige ni afisa wa lishe wa UNICEF, Nairobi na anaelezea kuwa, 

Tunawafunza kina mama jinsi ya kupata lishe tangu wakati wa uja uzito hadi wanapojifungua.Baada ya hapo tunawaeleza njia bora za kumnyonyesha mtoto na lishe mujarab kwa mama ili awe na maziwa ya kutosha.Mtoto anayenyonya maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ya uhai wake haambukizwi magonjwa kwa haraka na hilo linawapa wauguzi nafasi kushughulikia matatizo mengine ambayo wanaweza kuwa nayo.” 

Abubakar Bashir na familia yake kutoka Kenya. Yeye ni mwanaharakati na muelekezi wa masuala ya kunyonya katika jamii.
UN News/Thelmaa Mwadzaya
Abubakar Bashir na familia yake kutoka Kenya. Yeye ni mwanaharakati na muelekezi wa masuala ya kunyonya katika jamii.

Kina baba watiwa shime kujumuika 

Wazazi wa kiume wana mchango muhimu katika mchakato mzima wa mama kunyonyesha kila wakati. Kwenye taarifa yao ya pamoja wakati wa mwanzo wa maadhimisho ya wiki ya elimu ya umuhimu wa kunyonyesha, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO na lile la kuhudumia watoto, UNICEF, tathmini mpya ilibaini kuwa idadi ya watoto wanaonyonya maziwa ya mama pekee katika miei ya mwanzo ya maisha imeongezeka kwa 10% na kufikia 48% kote ulimwenguni. 

Abubakar Bashir ni mwanaharakati na mmoja ya wahamasishaji wa umuhimu wa kunyonyesha watoto na anasisitiza kuwa lishe bora ndio msingi wa afya bora kwa watoto kwani, Wazazi wote wawili wakishikana ili kuhakikisha mtoto ananyonya maziwa ya mama basi afya yake inaimarika kwa kiasi kikubwa.Sisi wanaume, sisi kina baba tuna nafasi muhimu ya kuwashika mkono wake zetu ili waweze kunyonyesha kila wakati. Hata ikiwa hupo nyumbani, piga simu uulizie iwapo mtoto amenyonya ipasavyo. Ni wajibu wetu sote kama wazazi kwani hakuna majukumu ya baba au mama.” 

Maziwa ya mama yabamba

Mada kuu ya wiki ya uhamasisho wa umuhimu wa kunyonyesha ni kuwawezesha kina mama wanaofanya kazi kunyonyesha kazini. Martha Mugi ni muasisi na mwenyekiti wa shirika la kina mama wanaofanya kazi ambao wananyonyesha, CAMFEB na alipitia wakati mgumu alipokuwa anarejea kazini baada ya kujifungua. Hilo lilimsukuma kuanzisha shirika hilo linalohusika na kuwaelimisha wasimamizi wa makampuni kuhusu umuhimu wa kutenga nafasi maalum za wafanyakazi wao wa kike kuonyesha. Martha anaelezea kuwa,

Martha Mugi, muasisi wa shirika la CAMFEB nchini Kenya linalosambaza bidhaa za kuwasaidia kina mama kukamua na kuhifadhi maziwa wakiwa kazini ili waendelee kunyonyesha wanaporejea ofisini au nyumbani.
UN News/Thelma Mwadzaya
Martha Mugi, muasisi wa shirika la CAMFEB nchini Kenya linalosambaza bidhaa za kuwasaidia kina mama kukamua na kuhifadhi maziwa wakiwa kazini ili waendelee kunyonyesha wanaporejea ofisini au nyumbani.

”Tumefanikiwa kusambaza elimu na kusababisha makampuni kadhaa kutenga nafasi za wafanyakazi wanawake kunyonyesha wanaporejea kazini baada ya kujifungua. Tumepata kushirikiana na kampuni kadhaa na sasa kuna mabadiliko.Kwa mashirika ambayo hayana nafasi kubwa, tumeunda kabati maalum lililo na beseni la kuoshea mikono, sehemu ya jokofu ya kuhifadhia maziwa ya mama na hata kifaa cha kupashia chakula moto ili mama aweze kula kwa amani. Tumetimiza vigezo vya wizara ya afya vya usafi na utendaji.” 

WHO na UNICEF kwa pamoja wanasisitiza kuwa ili kutimiza lengo la idadi ya kina mama wanaonyonyesha kufikia 70% ifikapo mwaka 2030, vikwazo wanavyokabiliana navyo wanawake sharti viondolewe katika jamii na sehemu za kazini. Laura Kiiige, afisa wa lishe wa UNICEF anasisitiza kuwa pale mtoto anaponyonya maziwa ya mama pekee matokeo ni mazuri kwasababu, ”Pindi mtoto anapozaliwa na kupewa titi la mama, anaanza safari ya kuwa na afya bora kwani atapata lishe kamili. Watoto walionyonya maziwa ya mama wanakua vizuri na hawatatiziki maishani. Hilo ni jambo la kujivunia kwa taifa lolote.”

UNICEF na WHO zinazitolea wito serikali na mashirika ya binafsi kote ulimwenguni kutunga sera zinazowawezesha kina mama wanaorejea kazini kuendelea kunyonyesha ima ofisini au hata kwenye biashara zao.