Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi katika Michezo: Kutana na Timu ya Taifa ya Kandanda ya Wanawake ya Afghanistan

Timu ya Taifa ya Kandanda ya Wanawake ya Afghanistan.
UNHCR Video
Timu ya Taifa ya Kandanda ya Wanawake ya Afghanistan.

Wakimbizi katika Michezo: Kutana na Timu ya Taifa ya Kandanda ya Wanawake ya Afghanistan

Wanawake

Katika uwanja wa mpira mjini Melbourne katika jimbo la Victoria nchini Australia. Wanawake wakimbizi wanafanya mazoezi ya mpira wa miguu kwa furaha lakini hajasahau madhila waliyoyakimbia nchini mwao Afghanistan.

Soundcloud

Fatima Yousufi hata huku ukimbizi ni Nahodha wa Timu ya mpira wa miguu wa Wanawake ya Taifa la Afghanistan hata kama nchini mwao hawatambuliki tena, anasema, "Hisia za kucheza soka kwangu ni za maajabu hasa kila ninapokuwa ndani ya uwanja najihisi kuwa salama. Ninajaribu kusahau matukio hayo yote mambo yote ambayo nimepitia.” 

Wakati Taliban waliponyakua mamlaka nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka 2021, haikuwa salama tena kwa timu ya taifa ya kandanda ya wanawake. Msichana huyo alilazimika kukimbilia uwanja wa ndege yeye na familia yake. Baada ya juhudi za kimataifa, serikali ya Australia ilikuwa imetoa viza za dharura kumhamisha Fatima na wachezaji wengine 37 wanawake, pamoja na wanafamilia wao, hadi Australia. Lakini katika machafuko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kabul, wazazi wa Fatima na dada yake mdogo walirudishwa nyuma na hawakufanikiwa kuingia kwenye ndege iliyombeba Fatima na kaka yake. 

Dada yao mwingine alijiunga nao baadaye baada ya kutoroka kwa njia nyingine. Fatima anaeleza hali ilivyokuwa akisema, "Tulienda kwenye uwanja wa ndege na ilikuwa vigumu sana kuona. Kwa mtazamo wangu ilikuwa kama tukio la mazombi. Kila mtu aliogopa na kujaribu kutoroka. Kila mtu alikuwa akikimbia. Milio ya bunduki, sauti za mayowe ya watoto masikioni mwangu.” 

Fatima anaendelea kueleza akisema, "Sikuwa na nafasi ya kuwaaga mama na baba yangu na mara ya mwisho kuwaona ilikuwa uwanja wa ndege. Na ilikuwa huzuni sana. Na walipigwa na Taliban na hawakuweza kuendelea na safari yao.” 

Timu hiyo ya taifa la Afghanistan ya wanawake ilifikia katika mji wa Melbourne na ikahifadhiwa na klabu ya Melbourne Victory FC. Sasa, wanawake hawa wanacheza msimu wao wa pili katika Ligi ya Jimbo la Victoria. 

Caroline Carnergie ambaye ni Mwendeshaji Mkuu wa Melbourne Victory FC anasema, "Nadhani imekuwa safari ya kufurahisha kwetu kutumia jukwaa letu la mpira kufanya zaidi ya kushinda michezo ya mpira wa miguu na tutaendelea kuwaunga mkono kwa muda mrefu tuwezavyo ili kuhakikisha kuwa tunawasaidia sio tu ndani bali pia nje ya uwanja wa mpira." 

Mchechemzi wa haki za binadamu na aliyekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya wanaume ya Australia Craig Foster alisaidia katika harakati za kuwahamisha wanawake hawa kutoka Afghanistan hadi nchini Australia, anasema, "Wamekuwa ishara ya haki za wanawake na wasichana nchini Afghanistan na kote ulimwenguni na pia wamekuwa kikundi muhimu sana ndani ya jamii ya Australia na wanatusaidia kuunda upya simulizi kuhusu wakimbizi nchini Australia." 

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi Filippo Grandi hivi karibuni amekutana na timu hiyo nchini Australia anasema,  "Wakimbizi wanapopewa fursa katika nchi kama Australia, wanaweza kustawi, wanaweza kuchanua na wanaweza kuchangia katika jamii, ambayo ni muhimu sana. UNHCR inajishughulisha sana na mipango inayohusiana na michezo katika muktadha wa wakimbizi. Tunajaribu kuleta michezo na nguvu zake katika mazingira magumu sana ya watu wasiojiweza. Mchezo ni mzuri kwa kuwapa watu matumaini ya siku zijazo."