Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali imesikia kilio chenu Wakenya ina mikakati chonde chonde kuweni na subira: Susan Mang’eni

Susan Auma Mang’eni (kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirika na Biashara ndogondogo wa Kenya akihojiwa na Flora Nducha katika Makao Makuu y aUmoja wa Mataifa, New York Marekani.
UN News
Susan Auma Mang’eni (kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirika na Biashara ndogondogo wa Kenya akihojiwa na Flora Nducha katika Makao Makuu y aUmoja wa Mataifa, New York Marekani.

Serikali imesikia kilio chenu Wakenya ina mikakati chonde chonde kuweni na subira: Susan Mang’eni

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la Umoja wa Mataifa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu HLPF limekunja jamvi jana hapa Makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani baada ya siku 10 za tathimini ya utekelezaji wa malengo hayo au SDGs. Waakilishi wa nchi na serikali, wanazuoni, mashirika ya Umoja wa Mataifa, wanaharakati na vijana ni miongoni mwa waliohudhuria, na Kenya haikubaki nyuma katika jukwaa hilo.

Susan Auma Mang’eni katibu mkuu wa wizara ya ushirika na biashara ndogondogo wa Kenya alibeba bendera yataifa hilo miongoni mwa waliowasilisha tarifa katika mkutano wa vijana kandoni mwa jukwaa hilo amenieleza kuwa  moja ya changamoto kubwa ya utekelezaji wa malengo hayo hasa kwa nchi zinazoendelea kama Kenya ni ufadhili ulioahidiwa na mataifa tajiri ya G20 ambao bado haujatolewa kwa nchi zinazoendelea, 

“Zikitusaidia sasa tutaweza kuweka mikakati ambayo inatakikana ili tuweze kupunguza hali ngumu ya Maisha na kando ya hapo katika kuangalia masuala ya mabadiliko ya tabianchi tumejitoa ndio maana kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 6 mwezi ujao tutakuwa na kongamano kubwa sana la Afrika la kuweza kuangazia mambo ya hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi tukijiandaa kwenye kwenye kongamano la COP28.”

Susan Auma Mang’eni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirika na Biashara ndogondogo wa Kenya.
UN News
Susan Auma Mang’eni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirika na Biashara ndogondogo wa Kenya.

Susan amekiri kwamba changamoto za hali ngumu ya maisha zinazochangiwa na sababu lukuki ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine hususa kwa Kenya zimechochea hali ya uchumi hasa mifukoni mwa watu kuwa mbayá zaidi wengi wakishindwa kumudu Maisha ya kila siku na kuzusha maandamano, hata hivyo amesema serikali imesikia kilio chao na inajitahidi kuleta afueni amewasihi Wakenya kuwa na subirá,

“Ningependa kuwaambia Wakenya kwamba serikali ina mikakati tulieni, tufanye bidii , tupange pamoja hali itakuwa nzuri, tukiendelea kwenda kufanya maandamano ambayo ni maharibifu katika hiyo hali watu wanapoteza maisha, watu wanaumia hata askari pia wanaumia tuanendelea kufanya hii hali iwe hata ghali kiasi. Ugali hauko barabarani, ugali uko mashambani kwetu , ugali uko kwenye bidii yetu ya biashara ndogondogo. Niwaomba Wakenya kwamba msikubali kupelekwa barabarani bila msimamo kwa sababu hizo changamoto sio za Kenya peke yake.”

Mapema wiki hii ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitoa tarifa ikisema inatiwa hofu na maandamano yanayoendelea Kenya baada ya watu 23 kuuawa katika maandamano hayo huku ikivisihi vyombo vya ulinzi na usalama kutotumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji kwani kuandamana ni haki yao ya msingi ya kiraia.