Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HLPF: Safari bado ndefu kutimiza SDGs duniani

Gavana wa Kauti ya Kakamega Fernandes Baraza (Katikati) pamoja na Mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe ( wa kwanza kushoti) wakiwa katika mahojiano na Leah Mushi( wa kwanza Kulia) katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Gavana wa Kauti ya Kakamega Fernandes Baraza (Katikati) pamoja na Mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe ( wa kwanza kushoti) wakiwa katika mahojiano na Leah Mushi( wa kwanza Kulia) katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

HLPF: Safari bado ndefu kutimiza SDGs duniani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu lijulikanalo kama HLPF linafikia tamati hii leo hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York-Marekani baada ya siku 10 za majadiliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa juu ya utelekelezaji wa SDGs katika nchi zao, maendeleo na changamoto walizokutana nazo ikiwa ni miaka 15 tangu kuanza utekelezaji wake ambao unatarajiwa kufikia tamati mwaka 2030. 

Miongoni mwa waliohudhuria HLPF ni pamoja na wawakilishi wa nchi na serikali, wanasayansi, wanazuoni, mashirika ya umoja wa Mataifa, asasi mbalimbali na vijana. 

Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imefanya mahojiano na wawakilishi kutoka nchini Kenya ambao wameeleza kwa yale waliyosikia kutoka katika nchi mbalimbali zilizowasilisha utelekezaji wa SDGs ni dhahiri kuna safari ndefu kabla ya kuyafikia kikamilifu.

Soundcloud

Akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Mbunge wa jimbo la Likuyani nchini Kenya Innocent Mugabe amesema “Imebainika wazi kwamba malengo 17 ya maendeleo endelevu yapo mbali sana kufikiwa na sasa hivi tukiwa katika muhula wa kwanza ama nusu na ni malengo 12% pekeyake ambayo yameweza kutimia ama yanaenda sawia na ratiba ambayo ilikuwepo ya utekelezaji wake.” 

Mbunge Mugabe amesema takwimu hizo zinamaanisha kwamba mataifa na maeneo na nchi ambazo zinahusika na zinafaa kujidhatiti zaidi na kutilia mkazo ili kuweza kufanikisha malengo hayo. 

Kwa upande wake Gavana wa Kauti ya Kakamega Fernandes Baraza amesema kikubwa alichoshuhudia kikielezwa na nchi nyingi ni suala la haki za binadamu. “Watu wemezungumza sana kuhusu haki na wametaka kuhakikisha kuwa kila mtu anahusishwa katika maendeleo hii inajumuisha watu wenye ulemavu, kina mama, vijana wote wawepo kwenye shughuli za maendeleo.”

Nini kifanyike kutimiza SDGs?

“Ili tuweze kufanikisha malengo haya ni lazima kuwe na ushirikiano, hasa nchini Kenya tunahitaji ushirikiano wa mikono yote ya serikali, ngazi zote kuanzia ya kitaifa na serikali gatuzi kwasababu malengo mengi yanatekelezwa katika serikali gatuzi.” Amesema Mbunge Innocent Mugabe.

Pamoja na janga la CORONA kuathiri kasi ya utelekezaji wa malengo haya lakini kwa kujifunza kutokana na janga hilo baya lililoikumba dunia Mbunge Mugabe amesema inafaa kuwe na mbinu mbadala za kuhakikisha malengo haya yanatekelezwa.

“Sisi kama wabunge wa bunge la kitaifa ni jukumu letu kuweza kuweka sheria na será ambazo zitasaidia serikali kuu na serikali za kaunti kuweza kutekeleza malengo yao.”

Hata hivyo amegusia changamoto kubwa ya ufadhili inayozikumba nchi nyingi zinazoendelea ili kutekeleza malengo. 

Gavana wa Kauti ya Kakamega nchini Kenya Fernandes Baraza akizungumza katika mahojiano na Leah Mushi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
UN News
Gavana wa Kauti ya Kakamega nchini Kenya Fernandes Baraza akizungumza katika mahojiano na Leah Mushi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake Gavana wa Kakamega amesema mbinu nyingine wanazotumia kuhakikisha wanafikia malengo ya maendeleo endelevu ni pamoja na “Kuhusisha kila mwananchi katika shughuli zote kwasababu watu wasipohusisha itakuwa vigumu sana mkono hayo maendeleo. “

Gavana Baraza ameeleza pia gatuzo zote 47 nchini Kenya zimehimizwa kuweka maendeleo endelevu katika ruaza za maendeleo ( ruaza za miaka 5 ijayo) ili kila mwaka wanapotenga bajeti waweze kutilia mkazo vipengele vinavyoenda kusaidia maendeleo.

Ameongeza pia wameweka kipaumbele katika kutafuta fedha za kuweza kutimiza miradi mbalimbali na hata katika ziara yao hapa Marekani katika HLPF wametilia mkazo ushirikiano na mashirika mbalimbali ikiwemo ya Umoja wa Mataifa kwasababu mipango inayofanyika nchini Kenya mfano katika eneo la Kilimo, Afya, Usafi wa Mazingira ikihusisha mashirika ya kitaifa na kimataifa yatasaidia kufanikisha maendeleo hayo. 

Gavana Baraza akagusia pia suala la Mazingira. “Usafi wa mazingira ni jambo ambalo tumeangazia pakubwa tukiwa hapa, na tukienda kule nyumbani tutashughulika sana kuhakikisha kwamba mazingira yetu yapo masafi.”

Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu HLPF liling’a nanga  tarehe 10 Julai na limefunga nanga tarehe 20 Julai 2030.