Jawabu la maandamano ya kila kona duniani, ni kuziba pengo la usawa:UN Ripoti

9 Disemba 2019

Ripoti ya maendeleo ya binadamu iliyozinduliwa leo na Umoja wa Mataifa inasema suala la kuchukulia kila hali kuwa mazoea haliwezi kutatua changamoto za kizazi hiki kilichoghubikwa na pengo la usawa. 

Ripoti hiyo  iliyotolewa  na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP ya maendeleo ya binadamu 2019 iliyopewa jina “zaidi ya kipato, zaidi ya wastani zaidi ya leo:pengo la usawa katika maendeleo ya binadamu kwenye karne ya 21” inasema maandamano yanayoshuhudiwa kila kona ya dunia hivi sasa ni ishara kwamba licha ya hatua kubwa iliyopigwa katika kutokomeza umasikini, njaa na maradhi jamii nyingi haziishi kama inavyopaswa na sababu kubwa ni pengo la usawa.

Akifafanua kuhusu hilo mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema vishawishi tofauti vinawaleta watu barabarani kuandamana mfano gharama za tikiti za gari moshi, bei ya petroli, madai ya uhuru wa kisiasa, harakati za kusaka usawa na haki. Hii ni sura mpya ya ukosefu wa usawa, na kama ripoti hii ya maendeleo ya Binadamu inavyosema, ukosefu wa usawa sio zaidi ya suluhisho.

Naye Pedro Conceição amesema mwaka huu ripoti imejikita katika ukosefu wa usawa zaidi ya kipato na utajiri, ikiaangalia nyanja nyingine za pengo la usawa kwa ajili ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDGs, mfano usawa wa kijinjia, jamii zenye amani na jumuishi na usawa wa uwezo wa watoto kupata elimu, ambazo amesema zinauwezekano mkubwa wa kuwafanya watu katika karne hii ya 21 kuishi maisha bora zaidi. Na kuhusu nini kifanyike Bwana Conceição amesema, "ripoti inachokifanya ni kutoa muongozo wa kuwawezesha watunga será , kufikiria kuweka será za kuchukua hatua kukabiliana na changamoto hizo zinazoibuka za pengo la usawa. Na ujumbe muhimu ni kwamba tunahitaji kwenda mbali zaidi ya masuala yanayohusiana na kodi na uhamishaji wa fedha tunapofikiria kushughulikia pengo hili la usawa.”

Ripoti hiyo inasema kwamba wakati pengo katika viwango vya msingi vya maisha likizidi kuwa finyu kwa mamilioni ya watu, ulazima wa kuweza kuishi unabadilika.

Pengo jipya la usawa linajotokeza katika suala la elimu na teknolojia na mabadiliko ya tabianchi, mambo mawili ambayo yansipozingatiwa ripoti inasisitiza yataweza kuibua mgawanyiko mpya katika jamii ambao haujashuhudiwa tangu mapinduzi ya viwanda .

Ripoti ikitoa mfano imesema mathalani katika nchi zenye maendeleo makubwa ya binadamu kuwa na broadband kunaongezeka haraka kwa kasi ya mara 15 na idadi ya watu wazima wenye elimu ya juu inaongezeka mara sita zaidi ya nchi zenye maendeleo kduni ya binadamu.

Kwa mujibu wa Conceição, ambaye amehusika pia katika kutoa mtazamo wa kupima maendeleo ya nchi zaidi ya kuangalia tu ukuaji wa kiuchumi amesema ripoti hii inautathimini ukosefu wa usawa katika hatua tatu ambazo ni zaidi ya kipato, zaidi ya wastani na zaidi ya leo. Lakini tatizo la ukosefu wa usawa haliko zaidi ya suluhu, ripoti inapendekeza kuweka será tofauti kushughulikia hilo, mfano uwekezaji katika maisha ya utotoni na ya baadaye,  uzalishaji kwa kujikita katika uwekezaji wa maisha ya watu, na matumizi ya umma na usawa katika kodi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter