Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akili Mnemba (AI) ilete nuru na si giza – Katibu Mkuu UN

Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018
IISD/ENB
Teknolojia ya droni nayo inaweza kuwa na manufaa bora au hasara kwa kutegemea inatumika kwenye misingi ipi. Hapa ni kwenye maonyesho ya ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu data uliofanyika Dubai 2018

Akili Mnemba (AI) ilete nuru na si giza – Katibu Mkuu UN

Amani na Usalama

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu amani na usalama duniani likimulika fursa na hatari zitokanazo na Akili Mnemba au Akili Bandia, AI ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesihi Baraza hilo lioneshe uongozi katika nyanja hiyo hasa katika kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kujenga madaraja ya kijamii, kidijitali na kiuchumi badala ya kuleta utengano na uharibifu.

Mkutano huo umeitishwa na Uingereza ambayo ndio inashikilia kiti cha urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Julai, na ni mara ya kwanza kwa Baraza hilo kuwa na mjadala kuhusu akili mnemba.

Guterres amesema Baraza linapaswa kuhakikisha kuna mikakati ya pamoja ya kuona mifumo ya Akili Mnemba inatumika kwa uwazi, uwajibikaji na bila kusahau ufuatiliaji wake ili hatimaye iwe na mchango katika kujenga kuaminiana katika amani na usalama.

Katibu Mkuu amesema hatua hizo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa hivi sasa akili mnemba licha ya kuwa na athari chanya, pia ina athari mbaya kwenye Maisha ya kila siku na kusonga kwa kasi kubwa.

Kasi ya AI ni ya ajabu

Ameonesha kustaajabu ya kwamba ilichukua zaidi ya miaka 50 kwa vitabu vilivyochapishwa kupatikaba barani Ulaya, lakini jukwaa la ChatGPT linalotumia akili mnemba limefikia watumiaji milioni 100 ndani ya miezi miwili.

Mchango wa AI kwenye uchumi yakadiriwa kufikia dola kati ya trilioni 10 hadi trilioni 15 ifikapo mwaka 2030.

Ingawa hiyo AI inaweza kuchochea ubaguzi na ufuatiliaji wa kidikteta kupitia serikali, amesema Guterres akimnukuu Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu.

Hivyo amesema, mjadala wa leo ni fursa ya kuangalia athari za AI au Akili Mnemba kwenye amani na usalama ambako tayari imeshaibua shaka na shuku za kisiasa, kisheria, kimaadili na kiutu.

Guterres amesema kasi ya ugunduzi kwenye teknolojia itaendelea kuwa kubwa kwa hivyo “nasihi hili Baraza lishughulikie teknolojia hii kwa haraka, kupitia lensi ya kimataifa na fikra za mtu anayejifunza.”

UN tayari inatumia AI kwenye kazi zake

Amesema tayari Umoja wa Mataifa unatumia AI au Akili Mnemba kwenye kazi zake zinazohusiana na amani, mathalani kubaini mwenendo wa ghasia, kufuatilia mizozo na zaidi ya yote kusaidia kuimarisha harakati za ulinzi wa amani, usuluhishi na usaidizi wa kibinadamu.

Amekumbusha kuwa mbinu za AI zinaweza kutumiwa kwa hila, mathalani kusaidia watu kujidhuru au kudhuriana kwa kiwango kikubwa. 

“Hebu tuwe wazi matumizi ya hila ya mifumo ya AI yanayofanywa na magaidi na wahalifu yanaweza kuleta uharibifu mkubwa, ikiwemo vifo, kiwewe na kisaikolojia,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa kutatua changamoto zitokanazo na AI badala ya kila nchi kuendeleza harakati peke yake za kudhibiti au usimamizi wa teknolojia hiyo.

Mbinu tunazo za usimamizi mzuri wa AI

Amesema tayari kuna mbinu za kimataifa kama vile kanuni ongozi za mwaka 2018-2019 kuhusu mifumo ya silaha hatarai iliyopitishwa kupitia Mkataba wa Kimataifa za Silaha zenye Sumu.

Ametaja pia mapendekezo kuhusu Maadili kuhusu Akili Mnemba yaliyopitishwa na shirika la Umoja wa MAtaifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Guterres ameongeza kuwa harakati zozote za kukabili changamoto za AI hivi sasa zijumuishe pande zote ikiwemo serikali, mashirika ya kiraia, ya kimataifa, wanasayansi huru na wale wote wahusika kwenye ugunduzi wa AI.

AI itokomeze umaskini na njaa

Pamoja na kukaribisha wito wa baadhi ya nchi wanachama wa kuundwa kwa chombo cha Umoja wa Mataifa cha kusimamia AI, Katibu Mkuu amesema kwa upande wake yeye ataitisha mkutano wa ngazi ya juu wa Bodi kuhusu AI ambayo itatoa ripoti mwishoni mwa mwaka huu kuhusu mbinu za usimamizi wa AI au Akili Mnemba.

Halikadhalika Andiko lake la siku chache zijazo kuhusu Ajenda ya Amani litatoa mapendekezo ya jinsi nchi wanachama wa UN zinaweza kusimamia AI.

Guterres ameeleza kuwa jambo muhimu ni kuendeleza AI ambayo ni salama, ya kuaminika na ambayo inaweza kumaliza umaskini, kutokomeza njaa, kutibu saratani na kukabili mabadiliko ya tabianchi.