Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jopo jipya la ushauri la UN kuwezesha Akili Mnemba (AI) kuwa ya manufaa kwa wote

Jopo la ushauri kuhusu Akili Mnemba au AI litachambua nafasi ya AI kwenye kusongesha SDGs.
© Unsplash/Steve Johnson
Jopo la ushauri kuhusu Akili Mnemba au AI litachambua nafasi ya AI kwenye kusongesha SDGs.

Jopo jipya la ushauri la UN kuwezesha Akili Mnemba (AI) kuwa ya manufaa kwa wote

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wataalamu 39 wenye uzoefu mkubwa kutoka serikalini, sekta binafsi, teknolojia, mashirika ya kiraia na wanazuoni wamepatiwa jukumu la kusaidia juhudi za Umoja wa Mataifa za kuhakikisha Akili Mnemba au (AI) inatumika kwa maslahi mapana ya binadamu.

Jopo hilo la Ushauri wa Akili Mnemba limezinduliwa Alhamisi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres jijini New York, Marekani na litachunguza hatari, furs ana usimamizi wa kimataifa wa teknolojia hiyo ambayo sasa inaonekana kuwa na faida na hatari.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Bwana Guterres ametaja maendeleo ya aina yake ya teknolojia hiyo na uwezo wa matumizi yake katika mwaka uliopita ikiwemo kunakili sauti ya mtu halisi, kutengeneza picha na apu za video.

Fursa za AI katika kusongesha SDGs

“Uwezo mkubwa wa mabadiliko wa Akili Mnemba ni mzuri kiasi kwamba ni vigumu kuelewa,” amesema Katibu Mkuu akizungumzia sasa umuhiu wa kukabili changamoto hiyo wakati huu ambapo nchi zinakabiliwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na na wakati huo huo harakati za kukamilisha malengo ya maendeleo endelevu zinasuasua.

“Akili Mnemba inaweza kubadili mwelekeo huu na kusongesha kasi ya kukamilisha SDGs ifikapo mwaka 2030,” amesema Katibu Mkuu.

Halikadhalika Akili Mnemba au (AI) inaweza kuongeza kasi na kurahisisha kazi za serikali, mashirika ya kiraia na Umoja wa Mataifa kwa kutabiri na kutatua majanga, hadi kutoa huduma za afya ya umma na elimu.

Cha kuzingatia

Pamoja na faida zake hizo ikiwemo kusaidia nchi zinazoendelea kurukia maendeleo makubwa kwa kasi, Katibu Mkuu amesema hatua zinahitajika kuhakikisha matumizi yake yanazingatia kanuni na vile vile huduma hizo za AI zipatikane kwa watu wote.

“Kwa sasa utaalamu huo umeshikiliwa na kampuni na nchi chache,” ameonya Katibu Mkuu jambo ambalo amesema linaweza kuongeza zaidi pengo la usawa wa kidijitali duniani.

Halikadhalika changamoto ya AI kutumika kusambaza habari za uongo na habari potofu na zinazoegemea upande mmoja, kuingilia faragha za watu na kukiuka haki za binadamu.

Kuhusu Jopo la Ushauri

Linajumuisha wataalamu 39 kutoka maeneo mbalimbali ya dunia, likizingatia jinsia, jiograpia na umri mbali mbali.

Kutoka Afrika wajumbe wanatoka nchi Tano ambazo ni Ethiopia, Afrika Kusini, Senegal, Zimbabwe, Misri na Kenya.

Mjumbe kutoka Kenya ni Philip Thigo, Mshauri kwa serikali ya Kenya,

Jopo linatarajiwa kutoa mapendekezo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kwneye maeneo ya usimamizi wa kimataifa wa AI, uelewa wa pamoja kuhusu hatari na changamoro za AI, fursa kuu, na viwezeshaji vya kutumia AI ili kusongesha SDGs.

Mpendekezo hayo yataelekezwa kwenye maandalizi ya mkutano wa Zama Zijazo utakaofanyika mwezi Septemba mwaka ujao.