Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo ya AI lazima yazingatie mkataba wa UN na haki za binadamu: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akizungumza hii leo kwenye mkutano wa usalama wa akili mnemba mjini London nchini Uingereza
United Nations
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) akizungumza hii leo kwenye mkutano wa usalama wa akili mnemba mjini London nchini Uingereza

Maendeleo ya AI lazima yazingatie mkataba wa UN na haki za binadamu: Guterres

Masuala ya UM

Kasi na ufikiaji wa teknolojia ya kisasa ya akili mnemba au AI haijawahi kutokea amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza hii leo kwenye mkutano wa usalama wa akili mnemba nchini Uingereza.

Guterres amesema “Kitendawili ni kwamba katika siku zijazo, akili mnemba  polepole kama leo na pengo kati ya AI na uthibiti wake ni pana na linakua.”

Katibu Mkuu amesema hatari zinazohusiana na AI ni nyingi na tofauti. Kama ilivyo AI yenyewe, bado zinaibuka, na zinadai suluhu mpya.

Amesisitiza kwamba, “Lakini wacha tuwe wazi, kanuni za udhibiti wa AI zinapaswa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa au chater na azimio la kimataifa la Haki za binadamu. Tunahitaji haraka kujumuisha kanuni hizo katika usalama wa akili mnemba.”

Mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na serikali ya Uingereza umezitela pamoja serikali, makampuni yanayoongoza katika AI, makundi ya asasi za kiraia na wataalam wa utafiti ili kutathimini hatari za AI na jinsi gani zinaweza kukabiliwa kupitia hatua za kimataifa zilizoratibiwa.

Sekta ya filamu kwenye mstari wa mbele: Majadiliano ya hali ya juu kuhusu AI katika tasnia ya sauti na kuona yalifanyika hivi majuzi huko Paris, Ufaransa.
UNESCO
Sekta ya filamu kwenye mstari wa mbele: Majadiliano ya hali ya juu kuhusu AI katika tasnia ya sauti na kuona yalifanyika hivi majuzi huko Paris, Ufaransa.

Mkataba mpya juu ya usalama wa AI

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa kilele wa AI, nchi 28 pamoja na Umoja wa Ulaya walikubaliana Azimio la Bletchley kuhusu usalama wa AI, ambalo linaanzisha "Uelewa wa pamoja wa fursa na hatari zinazoletwa na AI ". 

Nchi zilikubali "haja ya dharura ya kuelewa na kudhibiti kwa pamoja hatari zinazoweza kutokea kupitia juhudi mpya ya pamoja ya kimataifa ili kuhakikisha AI inaendelezwa na kutumiwa kwa njia salama, inayowajibika kwa manufaa ya jumuiya ya kimataifa."

Nchi zilizoidhinisha Azimio hilo ni pamoja na Marekani, China, Brazil, Ufaransa, India, Ireland, Japan, Kenya, Ufalme wa Saudi Arabia, Nigeria na Umoja wa Falme za Kiarabu. Azimio hilo pia limeonyesha kuwa hatari za AI "zinashughulikiwa vyema kupitia ushirikiano wa kimataifa".

Hatua tatu za udhibiti wa AI 

Wakati wa taarifa yake, Katibu Mkuu ametaja maeneo matatu ya utekelezaji ili kushughulikia pengo linaloongezeka kati ya AI na udhibiti wake.

Mosi:  Ametoa wito wa mifumo ya kukabiliana na hatari za kutolewa kwa miundo yenye nguvu ya AI ambayo inaweza kutumika vibaya na wahalifu au hata magaidi.

Pili: amesema ni kuhusu matokeo mabaya ya muda mrefu ya AI. Masoko ya ajira na uchumi vinaweza kukabiliwa na usumbufu, kunaweza kuwa na upotevu wa mchsnganyiko wa kitamaduni kwa sababu ya kanuni za algorithim zinazoendeleza upendeleo na fikra potofu na mvutano wa kijiografia na kisiasa unaweza kuongezeka ikiwa AI itajikita katika nchi na makampuni machache.

Bwana Guterres ameongeza kuwa "Madhara ya muda mrefu yanaenea kwa uwezekano wa utengenezaji wa silaha mpya hatari zinazowezeshwa na AI, mchanganyiko mbaya wa AI na teknolojia ya kibayolojia, na vitisho kwa demokrasia na haki za binadamu kutoka kutokana na taarifa potofu zinazosaidiwa na AI."

Bwana Guterres ametioa wito wa kuwa na mifumo ya kufuatilia na kuchambua mienendo hii ili kuizuia.

Tatu: na mwisho ameeleza kwamba bila hatua za haraka, AI itazidisha ukosefu mkubwa wa usawa ambao tayari unasumbua ulimwengu wetu. 

Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Oxford Insights imegundua kuwa hakuna nchi ya Kiafrika iliyo katika 50 bora kwa utayari wa AI.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihudhuria mkutano wa kilele kuhusu usalama wa AI unaofanyika London, Uingereza.
United Nations
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihudhuria mkutano wa kilele kuhusu usalama wa AI unaofanyika London, Uingereza.

Hata hivyo  AI ina uwezo mkubwa, Bwana Guterres amesisitiza. Inaweza kusaidia serikali kupanga bajeti, kupanua wigo wa biashara, wanasayansi wa hali ya hewa kutabiri ukame na dhoruba, pamoja na watu kupata huduma muhimu za afya na elimu. Inaweza pia kuwa kichochezi cha utimizaji Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu.

"Lakini ili hilo lifanyike, kila nchi na kila jumuiya lazima ipate AI na miundombinu ya kidijitali na takwimu inayohitaji," Bw. Guterres amesema, akitoa wito wa "juhudi za kimfumo kubadilisha ukweli kwamba teknolojia za AI kwa sasa zina kikomo kwa nchi na makampuni kadhaa.”

Juhudi za kimataifa

Ili kuzuia kukosekana kwa mshikamano na mapungufu katika udhibiti, Katibu Mkuu ametoa wito wa uangalizi wa kimataifa wa AI, akieleza kwamba Umoja wa Mataifa ni "jukwaa shirikishi, la usawa na la kimataifa la uratibu wa udhibiti wa AI."

Wiki iliyopita, Bw. Guterres alitangaza kuundwa kwa Bodi ya Ushauri ya AI, ambayo inaleta pamoja utaalamu wa kimataifa kutoka kwa serikali, biashara, jumuiya ya teknolojia, mashirika ya kiraia na wanazuoni. 

Mwishoni mwa 2023, Baraza la Ushauri litaripoti mapendekezo ya awali katika maeneo matatu ambayo ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa juu ya udhibiti wa AI, kujenga makubaliano ya kisayansi juu ya hatari na changamoto na kuifanya AI ifanye kazi kwa wanadamu wote.

Mapendekezo haya yataingia kwenye mkataba wa kimataifa wa kidijitali uliopendekezwa kupitishwa na wakuu wa nchi katika mkutano wa Wakati Ujao Septemba 2024.

Amehitimisha tarifa yaje kwa kusema kwamba "Tunahitaji mkakati wa pamoja, endelevu, wa kimataifa, unaozingatia ushirikiano wa kimataifa na ushiriki wa washikadau wote. Umoja wa Mataifa uko tayari kutekeleza wajibu wake”