Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zimepigwa katika utoaji chanjo lakini changamoto bado zipo:WHO/UNICEF

Mtoto akipokea chanjo ya polio nchini Burundi. (Maktaba)
© UNICEF Burundi
Mtoto akipokea chanjo ya polio nchini Burundi. (Maktaba)

Hatua zimepigwa katika utoaji chanjo lakini changamoto bado zipo:WHO/UNICEF

Afya

Takwimu mpya zilizotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani WHO na la kuhudumia watoto UNICEF, zinaonyesha dalili za huduma za chanjo kuongezeka katika baadhi ya nchi, lakini bado huduma hizo hazifikii viwango vya kabla ya janga la COVID-19, hasa katika nchi zenye kipato cha chini, na hivyo kuwaweka watoto katika hatari kubwa ya kupata maambukizi na milipuko ya magonjwa.

Mashirika hayo ynasema huduma za chanjo duniani kote zilifikia watoto milioni nne zaidi mwaka wa 2022, ikilinganishwa na mwaka mmoja nyuma huku nchi zikiongeza juhudi zilizokusudiwa kupambana na kusuasua kwa chanjo kulikosababishwa na janga la COVID-19.

Mamilioni wakosa chanjo

Hata hiyo takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka huo wa 2022, watoto milioni 20.5 walishindwa kupokea chanjo moja au zaidi ya diphtheria, pepopunda na pertussis (DTP), ikilinganishwa na watoto milioni 24.4 mwaka wa 2021.

Chanjo za DTP hutumiwa kwa kawaida kama kiashirio cha kimataifa cha chanjo.

Licha ya uboreshaji huo, ripoti inasema idadi hii bado ni zaidi ya watoto milioni 18.4 ambao walishindwa kupata chanjo moja au zaidi mwaka 2019, kabla ya usumbufu unaohusiana na janga la huduma za kawaida za chanjo kuanza.

Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO amesema 

"Takwimu hizi ni za kutia moyo, na ni pongezi kwa wale ambao wamefanya kazi kwa bidii kurejesha huduma za chanjo za kuokoa maisha baada ya miaka miwili ya kupungua kwa huduma ya chanjo. Lakini wastani wa kimataifa na wa kikanda hauelezei hadithi nzima na hufunika pengo la usawa linaloendelea. Wakati nchi na maeneo yanaposuasua kutoa chanjo watoto ndio hulipa gharama.”

Mtoto wa kiume wa miezi 6 akipata chanjo katika kituoni katika jimbo la Sindhi Pakistan
© UNICEF/Saiyna Bashir
Mtoto wa kiume wa miezi 6 akipata chanjo katika kituoni katika jimbo la Sindhi Pakistan

Tofauti zinazotia wasiwasi

Kwa mujibu wa WHO na UNICEF hatua za mwanzo za kujikwamua katika viwango vya chanjo hazijatokea kwa usawa. 

Maendeleo katika nchi zilizo na rasilimali nyingi zenye idadi kubwa ya watoto wachanga kama vile India na Indonesia, huficha viwango vya chini vya kujikwamua, au hata kuendelea kupungua, katika nchi za kipato cha kati na cha chini.

Kati ya nchi 73 ambazo zilirekodi kupungua kwa huduma, za chanjo 15 zimejikwamua hadi viwango vya kabla ya janga la COVID-19, na nchi 24 ziko ziko mbioni kujikwamua na, muhimu zaidi, nchi 34 zimekita palepale au zinaendelea kupungua, yamesema mashirika hayo.

Chanjo ya surua bado inademadema

Ripoti ya mashirika hayo inasema chanjo dhidi ya surua, mojawapo ya viini vinavyoambukiza zaidi, haijajikwamua na kufikia viwango kama vile vya chanjo nyingine.

Mwaka jana, watoto milioni 21.9  ikiwa ni milioni 2.7 zaidi ya mwaka wa 2019 walikosa chanjo ya kawaida ya surua katika mwaka wao wa kwanza wa maisha, wakati watoto milioni 13.3 zaidi hawakupokea dozi yao ya pili ya chanjo hiyo. 

Hii imeweka watoto katika jamii zisizo na chanjo katika hatari kubwa ya kuzuka mlipuko wa ugonjwa huo.

Takwimu zinaonyesha nchi zilizo na chanjo endelevu katika miaka kabla ya janga hili zimeweza kurejesha hali ya utulivu wa huduma hiyo ya chanjo.

Asia Kusini, ambayo iliripoti kuongezeka polepole kwa chanjo katika muongo mmoja kabla ya janga hili, imeonyesha ahueni ya haraka na ya nguvu zaidi kuliko maeneo ambayo kiwango kimeshuka, kama vile Amerika ya Kusini na Karibbea.

Kanda ya Afŕika, ambayo iko nyuma katika kujikwamua na mdororo wa chanjo, inakabiliwa na changamoto ya ziada inayotokana na ongezeko la watu. 

Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka, nchi lazima ziongeze huduma za chanjo ili kudumisha viwango vya kutosha vya chanjo na kuokoa Maisha yamesisitiza mashirika ya WHO na UNICEF.

Mvulana akipokea chanjo ya surua katika kituo cha afya katika jimbo la Tigray la Ehtiopia. (Maktaba)
© UNICEF/Hema Balasundaram
Mvulana akipokea chanjo ya surua katika kituo cha afya katika jimbo la Tigray la Ehtiopia. (Maktaba)

Kugeuza mwelekeo

Kwa msaada kutoka kwa Gavi, Muungano wa chanjo duniani, chanjo ya DTP3 katika nchi 57 za kipato cha chini iliongezeka kutoka asilimia 78 mwaka 2021 hadi asilimia 81 mwaka 2022, huku idadi ya watoto ambao hawapati chanjo ikipungua kwa milioni mbili katika kipindi hicho.

Ongezeko la huduma za chanjo ya DTP3 katika nchi zinazotekeleza huduma za Gavi lilijikita zaidi katika nchi za kipato cha kati, hata huku nchi nyingi za kipato cha chini bado hazijaongeza chanjo.

"Inatia moyo sana, baada ya usumbufu mkubwa unaosababishwa na janga la COVID-19, kuona chanjo ya kawaida ikipata ahueni kubwa katika nchi zinazoungwa mkono na Gavi, haswa katika suala la kupunguza idadi ya watoto wasiopata chanjo kabisa," amesema Dkt. Seth Berkley Mkurugenzi mtendaji wa Gavi.