Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu 3 zinazotumiwa na UNICEF kuhakikisha watoto wanapata chanjo

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio nchini Nigeria
UNICEF/UN036155/Page
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya polio nchini Nigeria

Mbinu 3 zinazotumiwa na UNICEF kuhakikisha watoto wanapata chanjo

Afya

Waswahili husema “Kinga ni bora kuliko tiba,” na hicho ndicho kinachofanywa na UNICEF katika nchi 190 wanachama wa shhirika hilo la Umoja wa Mataifa lililojikita kushughulika na masuala ya watoto na vijana barubaru lakini pia wanashughulika na familia katika kuhakikisha ulinzi wa watoto kabla ya kuzaliwa kwa wajawazito na baada ya kuzaliwa kwa familia nzima. 

Moja ya kinga kubwa kwa watoto ni chanjo ambazo hutolewa kuanzia kwa wajawazito na mara tu mtoto anapozaliwa na kila baada ya muda fulani kwa mujibu wa miongozo inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO

Je wanafanyaje kuhakikisha watoto kila kona ya dunia wanapata chanjo? Kuna njia tatu. 

Mosi ni Uhamasishaji kupitia michezo inayo wakutanisha kundi la watu mitaani. Mtaalamu wa mabadiliko ya kitabia ya jamii kutoka wilaya ya Adenta nchini Ghana, Charity Nikoi anasema kadri watu wengi zaidi wanavyopata uelewa kuhusu chanjo ndivyo watakavyo hamasika kwenye kuchoma. 

“Kupitia michezo inayo oneshwa mitaani watu wanaweza kupata majibu ya maswali ambayo yamekuwa yakiwaumiza vichwa kwa sababu baada ya kumalizika kwa maonesho ya michezo kunakuwa na wasaa wa kufanya majadiliano.” 

Njia ya pili ni uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba, UNICEF wakishirikiana na watoa huduma na wanajamii wanaojitolea hutembelea wananchi na kuwahasisha wapate chanjo 

Huko Nippes, kusini mwa nchi ya Haiti, Guerline mfanyakazi wa jamii wa kujitolea, kwa miaka 36 amekuwa akitembea kwa saa 6, mara nne kwa wiki, ili kufikia jamii zenye watoto wadogo na kuwahamasisha kuhusu chanjo. “Tunaenda nyumba kwa nyumba ili kutambua iwapo kuna watoto ambao hawajapatiwa chanjo. Baada ya hapo tunaongozana nao hadi katika vituo vya afya ili watoto wao waweze kupatiwa chanjo yao ya kwanza.” 

Na njia ya tatu ni kushirikisha familia nzima katika utoaji chanjo, na hii inahusisha uwekaji wa chanjo kama zile za COVID-19 katika kundi la chanjo ambazo familia zinachoma pindi wakienda katika kituo cha afya. Moja wa wanufaika wa mbinu hii ni Natalie Kabombo, mama wa watoto wawili mkazi wa Bukavu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, alipoenda kumchoma mtoto wake wa miezi mitatu chanjo ya Polio na yeya akaamua kuchoma chanjo dhidi ya COVID- 19. 

“Nilienda wanichome chanjo kwa sababu nilitaka kujikinga binafsi na nikinge familia yang una nikinge jamii yangu yote kwa ujumla.” Amesema Natalie mara baada ya kuchoma chanjo ya COVID-19.

Kuhusu UNICEF

UNICEF inafanya kazi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni hata yale magumu kufikika ili kuhakikisha wanawafikia watoto na vijana barubaru na wanahakikisha haki zao zinalindwa na chochote kinachohitajika ili kuwasaidia watoto kuishi, kustawi na kutimiza uwezo wao, kuanzia utoto hadi ujana.

Miongoni mwa mambo yanayofanywa na UNICEF ni kuhakikisha watoto wanapata chanjo, lishe, maji safi na salama na usafi wa mazingira, elimu bora, kuzuia na matibabu ya VVU kutoka kwa mama Kwenda kwa watoto, na ulinzi wa watoto na vijana dhidi ya unyanyasaji na unyonyaji.