Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Amani ikitawala malengo ya maendeleo endelevu yatafanikishwa - Lawrence Oluwaseun Adeniyi

Lawrence Oluwaseun Adeniyi raia wa Nigeria anayefanya shughuli zake Houston Marekani amewakilisha taasisi hii ya International Association of World Peace Advocates (IAWPA) katika Jukwaa la ngazi za juu kuhusu SDGs.
UN News
Lawrence Oluwaseun Adeniyi raia wa Nigeria anayefanya shughuli zake Houston Marekani amewakilisha taasisi hii ya International Association of World Peace Advocates (IAWPA) katika Jukwaa la ngazi za juu kuhusu SDGs.

Amani ikitawala malengo ya maendeleo endelevu yatafanikishwa - Lawrence Oluwaseun Adeniyi

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu HLPF ambalo liling’oa nanga Julai 10, litafikia tamati tarehe 20 mwezi huu. Mmoja wa vijana walioshiriki katika mkutano hili ni Lawrence Oluwaseun Adeniyi, raia wa Nigeria anayefanya shughuli zake Houston Marekani ambaye amewakilisha taasisi hii ya International Association of World Peace Advocates (IAWPA) inayojitambulisha kwa kazi kuu mbili ambazo ni Utetezi wa Amani na Kuhakikisha Maendeleo Endelevu.

Lawrence anasema kwamba mambo yanaenda vizuri na wanajaribu kuutekeleza mpango huo katika nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Kwa hivyo, nia yake katika Jukwaa hili ni kuhakikisha kwamba watu wengi kutoka uwakilishi wa nchi mbalimbali waliopo hapa wanaweza kujihusisha na taasisi hii ili hatimaye waweze kwenda sambamba katika kufikia lengo la mwaka 2030 kwa ajili ya SDGs.  

Na kuhusu analoondoka nalo kwenye Jukwaa hili anasema, “Kimsingi, ninaloondoka nalo hapa ni kwamba hatupaswi kumwacha mtu nyuma. Tumeshavuka nusu ya muda na tuna miaka michache tu imesalia. Tunahitaji kuweka juhudi zaidi katika shughuli zetu mbalimbali, kuhakikisha kwamba tunaweza kuzigusa nyanja zote za SDGs kuanzia ya lengo la kwanza hadi la 17. Jambo kuu hapa ni ushirikiano. Tunajaribu kuona jinsi tunavyoweza kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba tunaweza kufikia lengo la mwaka 2030. Ndiyo, hilo ndilo ninaondoka nalo. Kwa hiyo, hatuna muda wa kupoteza. Hatuachi jiwe lolote juu ya jingine, na lazima tufanye kazi kwa bidii hadi mashinani kupitia serikali, kuhakikisha tunakutana na wawakilishi wa ngazi za chini, kutengeneza wawakilishi zaidi katika maeneo mbalimbali ili tuwe na  wigo mpana zaidi wa katika nchi mbalimbali.” 

Mwisho, Lawrence anatoa ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa, “Amani! Amani ndiyo pekee tunachohitaji. Ninataka kutumia jukwaa hili kuuomba Umoja wa Mataifa kuona jinsi gani wanaweza kukuza amani ndani ya mgogoro ambao tayari unafanyika ndani ya Urusi na Ukraine. Ninaamini, si siku nyingi, wataweza kuhakikisha kuwa amani inatawala ndani ya nchi hizi mbili na kufikia msingi wa pamoja. Huo ndio wito wangu kwa Umoja wa Mataifa.”