Kila kijana ana wajibu wa kuimarisha hali ya maisha popote alipo-Banice

Bi. Banice Mbuki Mburu, mwakilishi kutoka jumuiko la asasi za kiraia za Afrika kuhusu Idadi ya watu na maendeleo akihutubia wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya ICPD kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani. (16 Julai 2019)
UN / Evan Schneider
Bi. Banice Mbuki Mburu, mwakilishi kutoka jumuiko la asasi za kiraia za Afrika kuhusu Idadi ya watu na maendeleo akihutubia wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya ICPD kwenye makao makuu ya UN, New York, Marekani. (16 Julai 2019)

Kila kijana ana wajibu wa kuimarisha hali ya maisha popote alipo-Banice

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu maendeleo endelevu, SDGs ukiendelea hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani, imeelezwa kuwa ushiriki wa vijana katika kufanikisha malengo hayo  sio suala la mjadala kwani ni lazima kundi hilo lishiriki kikamilifu ili malengo hayo yafanikishwe ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo ni yake Banice Mbuki Mburu, mwakilishi kutoka ushirika wa mashirika ya kiraia barani Afrika kuhusu idadi ya watu na maendeleo, kauli ambayo ametoa katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kandoni mwa mkutano huo.

Bi. Mburu amesema vijana lazima wapaze sauti zao kuhusu malengo hayo kwa kuwa, "mambo haya yanaathiri maisha yao na vizazi vijavyo ama watoto wao wanaokuja, kwa kweli wanafaa wajihusishe na wasione kuwa wakereketwa kama hawana kazi au wanataka kuonekana.  Ni ile tu ari, ile unaona tunaangamia na sisi ndio viongozi wa leo na viongozi wa kesho.  Kwa hiyo ni lazima kuchukua jukumu leo kwa sababu tusipochukua jukumu leo tutaangamia."

Bi. Mburu ambaye pia ni mwanharakati wa masuala ya vijana nchini Kenya ameongeza kwamba vijana kwa ujumla wana jukumu la kufanya ili kuimarisha hali ya sasa na kwa vizazi vijavyo akisema kuwa, "kila sekta ambayo kijana yupo, iwe elimu au afya, iwe sekta yoyote, wawe wanapigania haki pale alipo. Ikiwa anapigania haki ,hapo ndio tutakuwa tunasonga mbele. Lakini kuachia mwanaharakati pekee wapiganie masuala ya utawala bora, haki  au afya, sasa wanachoka na hawawezi wote kufanya vitu vyote.