Uchunguzi wa ukiukwaji mkubwa wa haki na uhalifu Sudan unaendelea: Chande Othman
Uchunguzi wa ukiukwaji mkubwa wa haki na uhalifu Sudan unaendelea: Chande Othman
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutafuta ukweli nchini Sudan umeanza kazi yake kwa ujumbe wa awali kuwasili mjini Geneva wiki hii, ukizitaka pande zinazozozana nchini Sudan kumaliza mzozo wa kivita nchini humo, kutekeleza wajibu wao wa kulinda raia na kuhakikisha kwamba wahusika wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu wanawajibishwa.
Akizungumza baada ya siku kadhaa za mazungumzo na viongozi na mashirika ya kiraia nchini Sudan, Mohamed Chande Othman, mwenyekiti wa Ujumbe huo wa kuutafuta ukweli, alisema leo kwamba uchunguzi kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu unaendelea.
Bwana Othman ameongeza kuwa “Mashirika ya kiraia ya Sudan na wadau wengine wameanza kushiriki nasi madai ya ukiukaji mkubwa wa haki unaoendelea. Madai haya yanasisitiza umuhimu wa uwajibikaji, umuhimu wa uchunguzi wetu, na hitaji muhimu la ghasia kukomeshwaa mara moja.”
Kuhusu ujumbe wa kutafuta ukweli Sudan
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilianzisha Ujumbe wa Kutafuta Ukweli mwezi Oktoba 2023 kuchunguza ukiukwaji wote wa haki za binadamu katika mgogoro kati ya Jeshi la Sudan SAF, Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na pande zingine zinazopigana tangu 15 Aprili 2023, na nia ya kuhakikisha kwamba waliohusika wanawajibishwa kwa ukiukaji na uhalifu unaohusiana na mzozo huo.
Mzozo huo umesababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na mamilioni kuyahama makazi yao wengine wakivuka mpaka na kuwa wakimbizi nchi jirani.
Tarehe 18 Desemba mwaka jana, Baraza liliteua wajumbe watatu wa ujumbe huo akiwemo Othman Chande, Mona Rishmawi, na Joy Ezeilo.
"Pande zinazopigana zina wajibu wa kisheria wa kimataifa kulinda raia dhidi ya mashambulizi, kuhakikisha upatikanaji wa msaada wa kibinadamu na kujiepusha na mauaji, kulazimisha watu kuhama makazi yao, kuteswa, kuwekwa kizuizini kiholela na kulazimisha watu kutoweka chini ya hali yoyote," amesema Rishmawi mmoja wa wajumbe na kuongeza kuwa "Tutathibitisha kwa uangalifu madai yote yaliyopokelewa na kufanya uchunguzi wetu wa ukweli kwa uhuru na bila upendeleo."
Ukiukwaji unaolenga wanawake na watoto
Naye mjumbe mwingine Ezeilo amesema Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli utazingatia hasa ukiukwaji unaolenga wanawake na watoto, hasa unaohusu unyanyasaji wa kijinsia.
"Madai ya ubakaji yanayolenga hasa wanawake na wasichana na madai ya kuajiri watoto kwa ajili ya matumizi vitani ni miongoni mwa masuala ya kipaumbele katika uchunguzi wetu," amesema Ezeilo.
Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli umetoa wito kwa pande zote kushirikiana na uchunguzi wao.
Ujumbe umealika watu binafsi, vikundi na mashirika kuwasilisha kwa siri taarifa muhimu kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Sudan kwa Kiingereza au Kiarabu.
Ujumbe huo unatakiwa kuwasilisha taarifa yake ya awali kuhusu matokeo ya awali katika kikao cha 56 cha Baraza la Haki za Binadamu mwezi Juni-Julai 2024, ikifuatiwa na ripoti ya kina kwa kikao cha 57 cha Baraza hilo mwezi Septemba-Oktoba na kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha 79 mwezi Oktoba 2024.