Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lakwama kupitisha azimio kusaidia Syria, Katibu Mkuu wa UN asikitishwa

WFP imesambaza vyakula vilivyoko tayari kwa kuliwa na vifaa vingine ambavyo si chakula kwa familia zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi katika kitongoji cha Al Mashariqa huko Aleppo, Syria.
© WFP/Hussam Al Saleh
WFP imesambaza vyakula vilivyoko tayari kwa kuliwa na vifaa vingine ambavyo si chakula kwa familia zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi katika kitongoji cha Al Mashariqa huko Aleppo, Syria.

Baraza la Usalama lakwama kupitisha azimio kusaidia Syria, Katibu Mkuu wa UN asikitishwa

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesikitishwa kwa kuona kwamba Baraza la Usalama halikuweza kufikia makubaliano leo kuhusu kurefusha idhini kwa operesheni za Umoja wa Mataifa za uvushaji wa misaada ya kibinadamu mpakani Uturuki kuingia nchini Syria. 

Akihutubia waandishi wa habari leo (Jul 11), Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu, amesema, "Msaada wa Umoja wa Mataifa wa kuvuka mpaka bado ni njia ya kweli ya maisha kwa mamilioni ya watu kaskazini-magharibi mwa Syria kwani mahitaji ya kibinadamu yamefikia kiwango cha juu tangu kuanza kwa vita, wakati athari ya matetemeko ya ardhi yenye uharibifu Februari ingali inahisiwa sana. 

Pia amesema Katibu Mkuu anatoa wito kwa wajumbe wote wa Baraza hilo kuzidisha juhudi zao ili kuunga mkono kuendelea kuwasilisha misaada ya kuvuka mpaka kwa mamilioni ya watu wenye mahitaji makubwa kaskazini-magharibi mwa Syria kwa muda mrefu zaidi. 

Baada ya kuisha kwa muda wa uvushaji misaada kwenye mpaka wa Bab al-Hawa, uwasilishaji wa usaidizi wa kuvuka mpaka utaendelea kupitia vivuko vya Bab Al-Salam na Bab Al-Ra'ee. 

Vivuko hivi viwili vilifunguliwa kwa idhini ya Serikali ya Syria kufuatia tetemeko la ardhi la Februari na idhini imeongezwa hadi tarehe 13 Agosti. 

Dujarric amesema, "Tutaendelea kutetea kupanua njia zote za kutoa msaada wa kibinadamu kwa mamilioni ya watu wenye uhitaji kaskazini-magharibi mwa Syria. Kuhuishwa kwa idhini hiyo ni muhimu, kwani Bab al-Hawa inasalia kuwa kitovu cha mvuto kwa mwitikio wetu wa kuvusha misaada mpakani, ikiwa ni pamoja na kuwa karibu na Idleb, ambako watu wengi wanaohitaji msaada kaskazini-magharibi mwa Syria wanaishi. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yalitoa utangulizi wa vifaa katika maeneo ya kaskazini-magharibi ili kuhakikisha kwamba mahitaji ya kibinadamu yataendelea kutimizwa katika siku zijazo. 

Imekuwaje? 

Urusi imepiga kura ya turufu kupinga nyongeza ya miezi tisa lakini pia nayo Urusi ikashindwa kufanikisha kupitisha azimio lake ambalo lingerefusha operesheni hiyo kwa miezi sita. 

Mamlaka ya operesheni hiyo, ambayo imekuwa ikitoa misaada ikiwa ni pamoja na chakula, dawa na malazi tangu 2014, ilimalizika Jumatatu Julai 10. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alikuwa ameomba kuendelezwa upya kwa miezi 12. 

Azimio la kwanza, lililoletwa na Brazil na Uswisi, wadau wenza kwenye suala la kibinadamu la Syria, lingeidhinisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu kuendelea kutumia kivuko cha Bab al-Hawa kwenye mpaka wa Syria na Uturuki kwa muda wa miezi tisa, hadi tarehe 10 Aprili 2024 lakini Urusi ikalipinga.  

China haikupiga kura ya kwanza, huku wajumbe 13 waliosalia wa Baraza la Usalama wakipiga kura ya ndio. 

Ni Urusi na China pekee ndizo zilizopiga kura kuunga mkono pendekezo la Urusi la kuongeza muda wa miezi sita. Wajumbe kumi wa Baraza la Usalama hawakupiga kura, na Marekani, Uingereza na Ufaransa zikapiga kura dhidi ya pendekezo la Urusi.