Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mipaka ya Syria lazima isalie wazi kuwafikishia mamilioni ya raia msaada:Tume 

Watoto wakicheza kwenye jengo lililoharibiwa Ghouta Mashariki, Syria.
© UNICEF/Amer Al-Mohibany
Watoto wakicheza kwenye jengo lililoharibiwa Ghouta Mashariki, Syria.

Mipaka ya Syria lazima isalie wazi kuwafikishia mamilioni ya raia msaada:Tume 

Msaada wa Kibinadamu

Azimio la Baraza la Usalama la kuruhusu kuingia kwa misaada ya kibinadamu kupitia kaskazini Magharibi mwa Syria linamalizika tarehe 10 Julai ambapo zaidi ya Wasyria milioni 14 bado wanategemea aina moja au nyingine ya msaada wa kibinadamu kuweza kuishi. 

Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu Syria leo imeonya kwamba  "Itakuwa ni kuwaangusha kwa kiwango cha juu raia wa taifa hilo endapo Baraza la Usalama halitaongeza muda wa mpaka kuendelea kubaki wazi kwa ajili ya utoaji wa misaada ya kibinadamu kwa Syria.” 

Kwa mujibu wa tume hiyo inayoongozwa na Mbrazil Paulo Sérgio Pinheiro, nchi hiyo inakabiliwa na moja ya matatizo mabaya zaidi ya kiuchumi na kibinadamu tangu kuanza kwa mzozo huo, zaidi ya miaka 10 iliyopita. 

Paulo Sérgio Pinheiro, anayeongoza tume ya Syria.
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Paulo Sérgio Pinheiro, anayeongoza tume ya Syria.

Idhini ya kuingiza msaada inamalizika muda wake 

Wataalamu wa tume hiyo wanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kulinda utaratibu wa sasa wa usaidizi kwa kuacha mipaka wazi na kuongeza ufadhili katika kuunga mkono jambo hili. 

Tume ya Uchunguzi inaeleza kuwa uidhinishaji wa kipekee wa Baraza la Usalama wa kuwasilisha misaada ya kibinadamu katika mpaka wa kaskazini-magharibi mwa Syria muda wake unamalizika tarehe 10 Julai. 

Mpaka huo umehakikisha upatikanaji wa msaada kwa mamilioni ya Wasyria tangu mwaka 2014.  

Paulo Sérgio Pinheiro ametangaza kwamba hitaji la azimio la Baraza la Usalama la kuwezesha kuingia kwa misaada ya kibinadamu “ni suala la kimaadili,” kutokana na ukiukwaji wa mara kwa mara unaofanywa na serikali ya nchi na wadau wengine katika vita vya Syria. 

Familia nyingi nchini Syria zinategemea msaada.
© UNICEF/Delil Souleiman AFP Services
Familia nyingi nchini Syria zinategemea msaada.

Mamilioni ya raia wanategemea misaada 

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa Wasyria milioni 14.6 wanategemea msaada wa kibinadamu.  

Raia wapatao milioni 12 kote nchini wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, ikiwa ni ongezeko la asilimia 51 kutoka mwaka wa 2019. 

Huko kaskazini magharibi mwa Syria, tume inasema hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya na ongezeko la uhasama wa mara kwa mara nlakini pia changamoto kubwa ya kiuchumi.  

Kupitia operesheni za misaada za kuvuka mipaka zilizoidhinishwa na Baraza la Usalama, misaada inawafikia watu milioni 2.4 kila mwezi, ikiwa ni rasilimali muhimu kwa wakazi wa kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo. 

Kulingana na tume hiyo ya uchunguzi kuhusu Syria, pande zinazohusika katika mzozo zinaendelea kushindwa "katika wajibu wao wa kuruhusu na kuwezesha upatikanaji wa haraka na usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa raia kote nchini".