Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio kuongeza misaada ya kibinadamu Syria lapitishwa

Wakimbizi wa ndani nchini Syria wapokea msaada wa kibinadamu. Picha: UNHCR

Azimio kuongeza misaada ya kibinadamu Syria lapitishwa

Hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea kuighubika syria leo imetawala kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo maafisa wanaoshughulikia suala la kisiasa na kibinadamu nchini humo wametoa tarifa.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Syria Stefaffan de Mistura ametoa tarifa kuhusu  duru ya mwisho ya majadiliano iliyomalizika Geneva Uswis na kuwaleta pamoja wawakilishi wa serikali na upande wa upinzani. Hata hivyo amelalamikia ukweli kwamba hakuna mafanikio yoyote yaliyofikiwa katika mazungumzo hayo.

(SAUTI YA STAFFAN DE MISTURA)

“Fursa ya kuanza mazungumzo ya kweli au majadiliano haikuchukuliwa. Nafasi ya kipekee imeponyoka kwa sababu mbalimbali , za kisaikilojia kwa sababu tuko mwisho wa mwaka, za kisiasa kwa sababu tunaelekea ukingoni, pia tunataka kuamini operesheni kubwa za kijeshi na kwa mtazamo wa kibinadamu  ni kwa sababu Wasyria wengi wamekuwa wakihoji na kusubiri jambo hili ili kuona hali yao inabadilika .”

Naye mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Mark Lowcock, amewataka wajumbe wa baraza kuhakikisha mwaka mpya unaleta ahuweni kwa madhila yanayowakabili watu wa Syria hususani katika maeneo yanayozingizwa kama Mashariki mwa Ghouta ambako raia 400,000 bado wamekwama wakiwemo 500 wanaohitaji huduma za haraka za tiba.

(SAUTI YA MARK LOWCOCK)

“tayari kuna vifo 16 miongoni mwa wanaosubiri rukhsa ya kuondoka Ghouta kwa sababu za matibabu wakiwemo watatu katika siku chache zilizopita. Miongoni mwao ni mtoto mchanga wa siku 45, binti wa miaka 9 na mtu aliyepooza. Kinachohitajika ni ruhusa tu kutoka kwa serikali ya Syria ili watu hawa waende hospitali maili chache nje ya Ghouta Mashariki.”

Kabla ya maelezo hayo ya hali ya kibinadamu na kisiasa wajumbe wa baraza walipitisha azimio linaloendelea kuruhusu utoaji wa misaada ya kuokoa kwa Wasyria mpakani kwa mwaka mwingine mmoja. Azimio hilo linaitaka serikali ya Syria kuharakisha utekelezaji wa maombi yote ya Umoja wa Mataifa na washirika wake ya kuruhusu misaada kuingia kwenye uwanja wa mapambano.