Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa Mpango wa Bahari Nyeusi: Mambo muhimu na takwimu

Meli ya WFP RC Vanessa ikisubiri ukaguzi wa kituo cha pamoja cha uratibu (JCC) katika bahari ya Marmara , meli hii imebeba ngano kutoka Ukraine kwenda Afghanistan
UN Photo/Levent Kulu
Meli ya WFP RC Vanessa ikisubiri ukaguzi wa kituo cha pamoja cha uratibu (JCC) katika bahari ya Marmara , meli hii imebeba ngano kutoka Ukraine kwenda Afghanistan

Mwaka mmoja wa Mpango wa Bahari Nyeusi: Mambo muhimu na takwimu

Msaada wa Kibinadamu

Kwa karibu mwaka mzima, Mpango wa Bahari Nyeusi ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa uliokubaliwa na Urusi, Uturuki na Ukraine umeruhusu mamilioni ya tani za nafaka na vyakula vingine kuondoka kwenye bandari za Ukraine, na kuwa na jukumu muhimu katika uhakika wa chakula duniani, kwa mujibu wa Katibu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Pia mpango huo unaojulikana kama Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi, unaendeshwa na kituo cha uratibu wa pamoja (JCC) huko Istanbul, chenye wafanyikazi kutoka Urusi, Uturuki, Ukraine, na Umoja wa Mataifa.

Haya ni mamuhimu na takwimu unazohitaji kujua:

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi umefanikisha nini tangu kutiwa saini Julai 2022?

Takriban mwaka mmoja ndani ya makubaliano hayo, zaidi ya tani milioni 32 za bidhaa za chakula zimesafirishwa kutoka bandari tatu za Bahari Nyeusi za Ukraine hadi nchi 45 katika mabara matatu.

Kurejeshwa kwa sehemu ya mauzo ya nje ya bahari ya Ukraine kumewezeshwa na mpango huo na kumefungua bidhaa muhimu za chakula ikiwa ni pamoja na kusaidia kupunguza kupanda kwa bei za vyakula duniani, ambazo zilifikia rekodi ya juu muda mfupi kabla ya mkataba kusainiwa.

Ripoti ya bei ya chakula ya shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ilionyesha kushuka kwa kasi kwa mwezi katika mwaka uliopita, na kushuka kwa zaidi ya asilimia 23 kutoka kilele chake mwezi Machi 2022.

Mpango huo umeruhusu shirika la mpango wa chakula duniani (WFP) kusafirisha zaidi ya tani 725,000 za ngano kusaidia watu wanaohitaji msaada katika nchi za Afghanistan, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan na Yemen. 

Ukraine ilitoa zaidi ya nusu ya nafaka ya ngano ya WFP mwaka 2022, kama ilivyokuwa mwaka 2021.

Idadoi ya mzigo unaosafoirishwa na mpango wa nafaka wa Bahari nyeusi , ifdadi yake kila unakokwenda
United Nations
Idadoi ya mzigo unaosafoirishwa na mpango wa nafaka wa Bahari nyeusi , ifdadi yake kila unakokwenda

Bei za vyakula na mfumuko wa bei bado viko juu. Mpango huo umesaidiaje mamilioni ya watu wenye njaa ulimwenguni pote?

Ingawa bei za bidhaa za chakula duniani kwa ujumla zimeshuka, mambo mengi yanaathiri upatikanaji wa chakula na mfumuko wa bei wa vyakula vya ndani, ikiwa ni pamoja na viwango vya ubadilishaji. 

Mpango huu umesaidia kuunganisha tena vyakula kutoka Ukraine hadi kwenye minyororo ya kimataifa ya usambazaji bidhaa, na hivyo kuchangia katika kupunguza bei katika masoko ya dunia.

Tathimini ya bei ya chakula ya FAO ilisimama kwenye pointi 140.6 mwezi Julai 2022, mpango huo ulipozinduliwa. 

Na sasa imepungua kwa asilimia 11.6 tangu wakati huo, na kufikia pointi 122.3 mwezi Juni 2023.

Katika kipindi hicho,tathimini  ya bei ya nafaka ya FAO imeshuka kwa asilimia 14 kutoka pointi 147.3 hadi pointi 126.6, shukrani kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa usambazaji wa kimataifa uliowezeshwa na Mpango huo.

Kwa nini Mpango wa Bahari Nyeusi uendelee?

Kabla ya mzozo huo, Ukraine ilikuwa mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa kuuza nje nafaka na msafirishaji mkuu wa kimataifa wa mafuta ya alizeti. 

Mazao yake lazima yaendelee kutiririka bila kuzuiwa na soko la usambazaji na kusaidia kudhibiti bien ya vyakula.

Ukosefu wa chakula huleta madhara makubwa kwa maisha ya mamilioni ya watu, hasa maskini zaidi, na kuwaathiri sana katika nyanja za afya, elimu, na mshikamano wa kijamii.

Mpango huo umeruhusu kuanza tena kwa sehemu ya bidhaa muhimu za chakula kwenye soko. 

Pia umewapa wakulima wa Kiukreni kiwango fulani cha kutabirika katika uzalishaji na mavuno na umefufua njia kuu za usafirishaji.

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wakipanda melini kuendesha ukaguzi kwa ajili ya kituo cha pamoja cha uratibu (JCC)
United Nations
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wakipanda melini kuendesha ukaguzi kwa ajili ya kituo cha pamoja cha uratibu (JCC)

 

Je, Mpango huo unakusudiwa kusambaza chakula kwa nchi zenye kipato cha chini barani Afrika na kwingineko? Je, kimsingi ni wa kibinadamu au wa kibiashara?

Lengo la Mpango wa Bahari Nyeusi ni kuwezesha mauzo ya nje kutoka bandari tatu za bahari ya Ukraine. 

Mazao kutoka Ukraine yanauzwa duniani kote, ikiwa ni pamoja na nchi ambazo baadhi ya wakazi wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Mizigo inaweza kuchakatwa na kusafirishwa tena kutoka maeneo ya awali. Mpango huo hauelezi ni wapi mauzo ya nje yanapaswa kwenda. 

Mauzo ya nje kwa nchi yoyote, tajiri au maskini, hata hivyo, yanaweza kusaidia kutuliza masoko ya kimataifa na kupunguza mfumuko wa bei za vyakula.

Ugavi unaosafirishwa chini ya Mpango wa WFP unasaidia moja kwa moja watu wanaohitaji katika majanga ya kibinadamu. 

Kufikia Julai 2023, WFP ilinunua asilimia 80 ya nafaka yake ya ngano duniani kutoka Ukraine chini ya Mpango huo, kutoka asilimia 50 mwaka 2021 na 2022.

Katika operesheni hii ya kipekee, mauzo ya nje ya kibiashara yana manufaa ya kimataifa.

Je mpango huo utaongewa muda lini, na kwa muda gani?

Shamba kubwa la mazao mjini  Baranove, katika jimbop la Odesa nchini Ukraine
© OCHA/Matteo Minasi
Shamba kubwa la mazao mjini Baranove, katika jimbop la Odesa nchini Ukraine

Muda wa awali wa Mpango wa Bahari Nyeusi ulikuwa wa siku 120 kuanzia tarehe 22 Julai 2022. 

Uliongezwa muda na wahusika wote tarehe 18 Novemba kwa siku 120 nyingine.

17 Machi  mwaka huu, pande zote zilikubali kuanzishwa upya, lakini Urusi ilikubali tu nyongeza ya siku 60 ikisubiri mapitio. 

Tarehe 18 Mei , Urusi ilithibitisha ushiriki wake katika mpango huo kwa siku nyingine 60. 

Kama matokeo, makubaliano sasa yamewekwa upya tarehe 17 Julai.

Umoja wa Mataifa ungependa kuona Mpango huo unatekelezwa na kupanuliwa kwa muda unaohitajika ili chakula kiweze kusafirishwa kutoka Ukraine kwa kutumia njia ya Bahari Nyeusi kwa usalama na kwa gharama nafuu.

Kwa nini mauzo ya chakula nje ya nchi kupitia Mpango huo yameshuka sana katika miezi ya hivi karibuni?

Uuzaji wa chakula nje kupitia Mpango huu umepungua kwa kiasi kikubwa katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kasi ndogo ya ukaguzi na kutengwa kwa bandari ya Yuzhny/Pivdennyi kwenye Mpango huo.

Kutoka kwenye rekodi ya wastani ya juu ya kila siku ya ukaguzi 11 mwezi Oktoba 2022, wastani wa kila siku umeshuka chini ya kaguzi tano katika miezi ya Aprili, Mei, na Juni 2023.

Mauzo ya kila mwezi yalifikia kilele cha tani milioni 4.2 mwezi Oktoba 2022, lakini yalikuwa tani milioni 1.3 pekee mwezi Mei 2023.

Maelezo na takwimu juu ya wingi na marudio ya mizigo zinapatikana hapa.

Kiasi cha shehena na ukaguzi kuanzia tarehe 1 Agosti 2022 hadi tarehe 10 Julai 2023:

Mzigo uliosafirishwa katika kila bandari na mwezi gani
United Nations
Mzigo uliosafirishwa katika kila bandari na mwezi gani

Kwa nini amonia haijasafirishwa nje?

Usafirishaji wa mbolea, ikiwa ni pamoja na amonia, ni muhimu kwa uzalishaji wa kilimo na uhakika wa chakula. 

Mpango huo unatoa usambazaji wa mbolea nje ya nchi, pamoja na amonia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza umuhimu wa kuongezeka kwa mbolea na vifaa vya amonia ili kusaidia uhakika wa chakula duniani. 

Hata hivyo, hadi sasa hakuna mbolea au amonia ambayo imesafirishwa nje ya nchi chini ya Mpango huo.

Usafirishaji wa amonia chini ya Mpango huu ungetegemea kuanza tena kwa bomba la amonia kutoka Togliatti nchini Urusi hadi bandari ya Ukraine ya Yuzhny/Pivdennyi. 

Uharibifu wa bomba hilo uliripotiwa tarehe 5 Juni, na hali yake ya sasa haijulikani.

Kwa nini UN haidai ukaguzi zaidi wa meli ili kuongeza usafirishaji?

Umoja wa Mataifa unasalia na nia thabiti ya kusaidia utekelezaji mzuri wa Mpango huo na kuendelea kwake. 

Hata hivyo, utekelezaji unategemea makubaliano, hivyo pande zote zinapaswa kukubaliana juu ya kasi ya operesheni.

Ukaguzi unafanywa kwa pamoja na wahusika wote husafisha kila chombo kwa safari yake ya kuingia na kutoka. 

Timu ya Umoja wa Mataifa katika JCC ipo kuwezesha na kufanya kazi na wahusika kujaribu kutatua changamoto za kiutendaji.

Ushirikiano wa hali ya juu na wahusika unaendelea katika juhudi za kupata makubaliano juu ya orodha ya hatua za kushughulikia maswala yao muhimu kwa njia inayokubalika kwa pande zote.

Mkaguzi wa UN Metin Gezer akiendesha ukaguzi wa JCC katika bahari ya Marmara
United Nations
Mkaguzi wa UN Metin Gezer akiendesha ukaguzi wa JCC katika bahari ya Marmara

Je, Mpango huo unatekelezwa vipi? Kwa nini mauzo ya nje kutoka Ukraine lazima yapitie utaratibu wa ukaguzi wakati usafirishaji kutoka Urusi haufanyi hivyo?

Jukumu la JCC ni kuwezesha upitishaji salama wa meli za kibiashara zinazobeba nafaka, vyakula, na mbolea, ikijumuisha amonia, ndani na nje ya bandari tatu za Ukrainia ambazo ni Odesa, Chornomorsk, na Yuzhny/Pivdennyi.

JCC pia ina jukumu la ukaguzi wa meli zinazoingia na kutoka nje ili kuhakikisha kuwa hakuna mizigo au wafanyakazi ambao hawajaidhinishwa. 

JCC inaripoti hadharani juu ya safari na usafirishaji wa meli unaowezeshwa chini ya Mpango huo.

Mpango wa Bahari Nyeusi haushughulikii mauzo ya nje kutoka bandari za nchini Urusi.