Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shehena ya Mbolea ya Urusi njiani kuelekea Malawi

Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi unaruhusu kiasi kikubwa cha mauzo ya chakula cha kibiashara kutoka bandari tatu muhimu za Kiukreni katika Bahari Nyeusi.
UN News
Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi unaruhusu kiasi kikubwa cha mauzo ya chakula cha kibiashara kutoka bandari tatu muhimu za Kiukreni katika Bahari Nyeusi.

Shehena ya Mbolea ya Urusi njiani kuelekea Malawi

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha mchango wa tani 260,000 za mbolea kutoka kwa wazalishaji wa mbolea nchini Urusi kwenda kupunguza mahitaji ya kibinadamu na kuzuia janga la uharibifu wa mazao barani Afrika, ambako kwa sasa ni msimu wa kupanda mazao.

Taarifa iliyotolewa hii leo jijini New York Marekani na msemaji wa Katibu Mkuu Stephane Dujarric imesema wazalishaji hao wa mbolea wa Urusi walikuwa wamehifadhi mbolea katika bandari na maghala barani ulaya.

Dujarric amesema Katibu Mkuu Guterres anazishukuru Serikali za Urusi, Malawi na Uholanzi, kwa uratibu wa karibu na Muungano wa Ulaya, kwa nia yao ya kuwezesha usafirishaji huu wa kwanza muhimu wa kibinadamu wa mbolea na WFP kwa kuhakikisha upatikanaji wa chakula duniani.

“Mpango huu wa uchangiaji wa mbolea ni sehemu ya makubaliano yaliyotiwa saini mjini Istanbul tarehe 22 Julai 2022 ili kushughulikia uhaba wa chakula duniani, ili kuhakikisha usafirishaji usiozuiliwa wa chakula na mbolea kutoka Ukraine na Urusi hadi katika masoko ya dunia.” Alisema Guterres.

Meli iliyokodishwa na WFP iitwayo MV Greenwich yenye shehena ya MT 20,000 za mbolea imeondoka Uholanzi hii leo kuelekea Malawi kupitia Msumbiji.

Guterres amesema hii itakuwa ni mara ya kwanza kati ya msururu wa shehena ya mbolea inayotumwa kwa mataifa kadhaa katika bara la Afrika katika miezi ijayo. Na kusema hili ni jambo jema kwani mbolea ina jukumu muhimu katika mifumo ya chakula, asilimia 50 ya idadi ya watu ulimwenguni hutegemea bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa msaada wa mbolea.

“Tangu mwaka 2019, bei ya mbolea imeongezeka kwa asilimia 250, kiwnago hiki kimesababisha upungufu wa mbolea jambo ambalo limewafanya wakulima kupunguza uzalishaji, haswa wakulima wadogo kutoka mataifa yanayoendelea. Uhaba wa mbolea ya nitrojeni mwaka huu unaweza kusababisha hasara ya uzalishaji mwaka ujao wa tani milioni 66 za mazao makuu (mahindi, mchele na ngano), ya kutosha kulisha watu bilioni 3.6, karibu nusu ya wanadamu, kwa mwezi.”

Guterres pia amesema kuunganisha upya masoko ya mbolea ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuna usalama wa chakula duniani kwa mwaka wa 2023 na Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya kila juhudi, kwa pande zote, kufikia lengo hili.

Umoja wa Mataifa pia unaendelea na juhudi kubwa za kidiplomasia na pande zote za Ukraine na Urusi kuhakikisha usafirishaji usiozuiliwa wa chakula na mbolea, bila vikwazo, kwa ajili ya masoko ya dunia.