Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatiwa hofu na ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na machafuko Haiti 

Njia kandoni mwa barabara iliyojaa bidhaa za kuuza katika mtaa Port-au-Prince, Haiti.
© UNDP/Borja Lopetegui Gonzalez
Njia kandoni mwa barabara iliyojaa bidhaa za kuuza katika mtaa Port-au-Prince, Haiti.

UN yatiwa hofu na ukiukwaji wa haki za binadamu kutokana na machafuko Haiti 

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Michelle Bachelet, amesema anatiwa hofu na kusikitishwa sana na madhara makubwa ya haki za binadamu kutokana na kuongezeka kwa machafuko na ghasia zinazohusisha magenge yenye silaha nzito nzito huko Port-au Prince, nchini Haiti. 

Katika taarifa iliyotolewa leo na hofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, mjini Geneva Uswis Bi. Bachelet amesema "Machafuko ya silaha yamefikia kiwango kikubwa na kisichovumilika Haiti. Ni muhimu sana kwamba hatua zikachukuliwa sasa ili kurejesha utawala wa sheria, kulinda watu dhidi ya machafuko hayo ya silaha na kuwawajibisha wafadhili wa kisiasa na kiuchumi wa magenge hayo ya wahalifu. " 

Ukatili uliokithiri 

Katika muda wa wiki tatu zilizopita, takriban washirika 92 wasio wanachama wa magenge na baadhi ya washukiwa 96 wa magenge hayo wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi ya kupangwa ya silaha huko Port-au-Prince.  

Kulingana na takwimu zilizothibitishwa na Umoja wa Mataifa, watu wengine 113 wamejeruhiwa, 12 wameripotiwa kutoweka na 49 walitekwa nyara kwa ajili ya kudai kikombozi, hata hivyo idadi halisi ya watu waliouawa inaweza kuwa kubwa zaidi. 

Taarifa hiyo inasema « ghasia kubwa zimeripotiwa ikiwa ni pamoja na watu kukatwa vichwa, kukatwa viungo na miili kuchomwa moto, pamoja na mauaji ya watoto wadogo wanaodaiwa kuwa watoa habari wa magenge pinzani. »  

Bi. Bachelet amesema « Unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa magenge ya watoto wenye umri wa miaka 10, pia umetumiwa na magenge hayo yenye silaha kuwatishia na kuwaadhibu watu wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na magenge hasimu. » 

Duru za habari pia zimeripoti kuwepo kwa watoto wadogo miongoni mwa magenge hayo. 

Maelfu ya watu wakiwemo watoto wamelazimika kuyahama makazi yao katika muda wa wiki tatu zilizopita na kutafuta hifadhi katika makazi ya muda au kwa familia zinazowapokea katika maeneo mengine ya nchi. 

Athari kubwa kwa haki za msingi za binadamu na uchumi 

"Unyanyasaji wa magenge umekuwa na athari kubwa kwa haki za msingi za binadamu. Makumi ya shule, vituo vya matibabu, biashara na masoko yamesalia kufungwa, na watu wengi wanatatizika kupata mahitaji ya msingi, ikiwa ni pamoja na chakula, maji na dawa,” ameongeza kusema Bi. Bachelet. 

Msongamano katika barabara kuu mbili za kitaifa zinazounganisha mji mkuu na maeneo mengine ya nchi umekuwa mkubwa na kuleta athari, kwani magenge yamedhibiti ufikiaji wa maeneo yaliyo chini ya ushawishi wao. 

"Vizuizi hivi kwa usafirishaji wa watu na bidhaa vinaweza pia kuwa na athari mbaya za muda mrefu kwa hali ngumu ya kiuchumi nchini Haiti," ameongeza Kamishna mkuu. 

Udhaifu wa taasisi za serikali, ni sababu inayochangia 

Kulingana Bi. Bachelet udhaifu wa taasisi za serikali, haswa polisi na mahakama, umechochea kutozingatiwa kwa utawala wa sheria, akielezea hofu kwamba ghasia zitaongezeka tu. 

Operesheni za polisi zinazoendelea zimeshindwa kurejesha utulivu wa umma au kulinda wakazi wa eneo hilo, na kuna ripoti za ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni hizi. 

“Licha ya changamoto zake nyingi za muda mrefu, Haiti lazima isisahaulike na lazima ibaki kuwa kipaumbele kwa jumuiya ya kimataifa. Ninaiomba jumuiya ya kimataifa kuzidisha juhudi zake ili kuzuia hali kuendelea kutoka nje ya udhibiti,” amesihi Bi. Bachelet  

Ametoa wito wa kuimarishwa kwa taasisi za serikali ili kupambana na hali ya kutokujali na ufisadi. 

"Mamlaka zina wajibu wa kulinda maisha dhidi ya vitisho vyote vinavyoonekana, vikiwemo vile vinavyotoka kwa watu binafsi na mashirika, kama vile magenge ya wahalifu wenye silaha," amekumbusha afisa huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

"Katika wiki zijazo, wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajadili jukumu la siku zijazo la uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti, ni muhimu kwamba haki za binadamu za Haiti ziwe kiini cha hatua za kimataifa, hasa juu ya masuala yanayohusiana na ukatili wa kingono na jinsia na unyanyasaji wa msingi," amesema Bi Bachelet.