Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lengo letu ni kuhakikisha kila mtu Afrika anakijua na kukizungumza Kiswahili-Wadau

Wadau wa lugha ya Kiswahili wakizungumza na Flora Nducha hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
UN News
Wadau wa lugha ya Kiswahili wakizungumza na Flora Nducha hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Lengo letu ni kuhakikisha kila mtu Afrika anakijua na kukizungumza Kiswahili-Wadau

Utamaduni na Elimu

Maadhimisho ya pili ya siku ya lugha ya Kiswahili duniani yamewadia ni wiki ijayo tarehe 7 ya mwezi Julai ambapo wadau wote wa kiswahili duniani kuanzia kwenye shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, kwenye Mataifa wazungumzaji wa lugha hii adhimu hadi ughaibuni mambo yatakuwa bambam, lakini hapa kwenye makao makuu ya umoja wa Mataifa maandalizi yamefikia wapi? Na nini kitajiri? Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa imewaalika wadau wa Kiswahili hapa kwenye makao makuu kufahamu maandalizi yanaendeleaje.

Hussein Kattanga ambaye ni balozi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa amesema maandalizi hayo yanaendelea viizuri kama yalivyopangwa na kikubwa zaidi “Mwaka huu tumeona kwamba sisi watu wa Afrika Mashariki tumeona jambo hili tulifanye kwa pamoja , tumeshirikisha UNESCO shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, tumeshirikisha SAD nchi zote 16 wanachama wa jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika na pia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pia.”

Mwaka huu watu watarajie nini tofauti na mwaka jana?

Balozi Kattanga amesema  kikubwa ambacho wangependa kukiona ni utofauti katika wazungumzaji wa Kiswahili “Kwa mfano tumegundua kuna Watanzania hapa wanawafundisha watoto wa diaspora  wa wale watu wetu wa Congo, Rwanda, Tanzania na kadhalika ambao wanaurithi wa lugha ya Kiswahili. Ukimfundisha mtoto tangu mdogo anaanza kuelewa mila na desturi zake mapema , kwa hilo tutawaalika na watu wengine kama Profesa Guna aliyeshinda tuzo ya Amani ya Nobel kwa ajili ya Kiswahili, lakini pia tutawaalika wanafunzi wa vyuo mbalimbali hapa wanaofundishwa Kiswahili .”

Hussein Kattanga, Balozi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
UN News
Hussein Kattanga, Balozi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Akaenda mbali zaidi na kusema hapa kwenye umoja wa Mataifa pia kuna mabalozi mbalimbali wanaozungumza Kiswahili wataalikwa pia na kutoka Afrika wanatarajia kupata ujumbe wa video kutoka kwa Marais mbalimbali wanaozungumza Kiswahili na wengineo.

DRC na SADC ni wadau wakubwa wa Kiswahili

Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambayo imejiunga hivi karibuni na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC na ambayo pia kwasasa ni mwenyekiti wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC Kiswahili kitakuwa na faida gani kwao na SADC kwa ujumla? Afisa msaidizi wa ubalozi wa kudumu wa DRC kwenye umoja wa Mataifa Serge Banza anasema “ DRC ina miguu miwili mmoja uko Jumuiya ya Afrika Mashariki na mwingine SADC kama ilivyo Tanzania sasa sisi ndio tutakuwa makapteni wa kusukuma mbele Kiswahili ndani ya SADC, kwani kwas asa Kiswahili tayari ni lugha rasmi ndani ya SADC, na hivyo kuanzia hapo tutatafari jinsi gani ya kukisambaza Kiswahili zaidi na zaidi.”

Serge Banza, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Congo DRC kwenye Umoja wa Mataifa, DRC ambaye pia ni mwenyekiti wa SADC akizungumza na Flora Nducha jijini New York Marekani.
UN News
Serge Banza, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Congo DRC kwenye Umoja wa Mataifa, DRC ambaye pia ni mwenyekiti wa SADC akizungumza na Flora Nducha jijini New York Marekani.

Ameendelea kusema kwamba hata katika nchi yake ya DRC kiswahili kinazidi kuchanja mbuga kwani “Leo hii hata Kinshasa watu wote wanajua salamu ya Kiswahili jambo, habari gani? Hivyo lugha hiyo inaendelea kuingia polepole.”

Akitoa mfano amesema "Mimi nilizaliwa Kalemie lakini nimejifunza Kiswahili Kinshasa na sio Kalemie."

Ughaibuni Kiswahili pia kinashika kasi

Ughaibuni na hasa nje ya bara la Afrika Kiswahili kimeendelea kukumbatitwa n anchi nyingi watu wake wanajifunza na hasa wanapopata fursa za kutembelea Afrika Mashariki. 

Miongoni mwao ni Janosch Kullenberg afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Ujerumani hapa Umoja wa Mataifa aliyeieleza Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kilichomsukuma kujifunza Kiswahili anasema “Baada ya kumaliza jeshi nilikuwa mwalimu Tanzania na nilikuwa katika eneo lijulikanalo kama Ananasifu jijini Dar Es Salaam. Na wakati huo ilinibidi nijifunze Kiswahili ili niweze kufundisha watoto kwani walikuwa ni wadogo.”

Janosch Kullenberg, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha jijini News York Marekani.
UN News
Janosch Kullenberg, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha jijini News York Marekani.

Kwa mataifa kama Ujerumani kujifunza Kiswahili kuna faida?

Janosch alipoulizwa endapo kwa mataifa kama Ujeruniani kuna faida yoyote ya watu kujifunza Kiswahili alisema “Ndio haswaa, ingawa siwezi kusema kuwa Kiswahili kinapaswa kuwa lugha ya taifa Ujerumani lakini ingekuwa vyema ikiwa itakuwa rahisi zaidi kwa watu wanaopenda kujifunza Kiswahili.”

Akaenda mbali na kusema watu wengi wanaosafiri kwenda Afrika Mashariki wanajifunza Kiswahili na hata wale wanaosoma shuleni hivyo “Unaweza kushangaa kwamba kuna watu wengi wanaozungumza Kiswahili Ujerumani.”

Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa kutachagiza wengi kujifunza?

Kiswahili sasa kimekuwa bidhaa ya kimataifa hili linaweza kuchagiza watu wengi kujifunza lugha hiyo? Yanosch anasema ”Nsafikiri kwa kila mtu kujifunza lugha inaruhusu mgeni kuwasiliana na watu , kufahamu utamaduni na kufurahia desturi. Faida moja kubwa ya Kiswahili ni kwamba Kiswahili kinazungumzwa kote Mashriki na Afrika ya Kati kama Congo.” 

Wadau wa lugha ya Kiswahili wakizungumza na Flora Nducha hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
UN News
Wadau wa lugha ya Kiswahili wakizungumza na Flora Nducha hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Nafasi ya Kiswahili katika kukuza uchumi

Je Kiswahili kina nafasi gani katika jumuiya kama SADC kwenye kukuza uchumi? Balozi Kattanga anasema tayari Kiswahili kimeshakumbatiwa na kinazungumzwa katika nchi za SADC “Na mkizungumza ni rahisi hata kufanya biashara na uchumi ni biashara, kwa sababu uwekezaji unaanza kwenye biashara kwa hivyo lugha inachochea uchumi lakini pia lugha inachochea amani.”

Akitoa mfano Balozi Kattanga amesema kuna nchi kama Namia, Botswana na Afrika Kusini wameshaingiza Kiswahili katika mitaala yako ya shule za masingi na sekondari kwa ajili ya kusongesha Kiswahili.”

Nini ujumbe wa wadau hawa katika siku ya Kiswahili

Gisele Kasongo afisa kwenye ubalozi wa kufumu wa Congo DRC kwenye Umoja wa Mataifa anasema ni wakati wa Afrika kushikamana kuidumisha lugha hii “Kuzungumza Kiswahili kuna umuhimu mkubwa , hivi sasa watu wengi duniani wanazungumza Kiingereza , sasa kama sisi Waafrika tutapambana na kushikamana Kiswahili kitasongambele na kesho kiswahili kitazungumzwa kila kona.”

Gisele Kasongo, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Congo DRC kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili, New York Marekani.
UN News
Gisele Kasongo, Afisa kwenye ubalozi wa kudumu wa Congo DRC kwenye Umoja wa Mataifa akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili, New York Marekani.

Yanosch kwa upande wake anatoa wito”Tafadhali jifunze Kiswahili ni lugha nzuri sana na inaweza kukusaidia kwenye maisha yako.”

Bwana Banza naye amekumbusha kuwa “Kiswahili ni lugha moja ya heshima sana na Kiswahili kinaweza kuiunganisha Afrika , hivyo Kiswahili ni kesho ya Afrika.”

Akikamisha mjadala Balozi Kattanga amewasihi wadau na wazungumzaji wote wa Kiswahili kukaribia na kujumika siku hiyo ya tarehe 7 Julai kwenye Umoja wa Mataifa katika hafla maalum ya kuienzi lugha hii adhimu lakini pia kutumia fursa iliyopo kujifunza lugha hii “Kwa kubidhaisha Kiswahili na kutafuta wazungumzaji wengi balozi zetu pia kote zinafundisha Kiswahili. Lugha ni thamani, utamaduni na ni urithi wa mtu yeyote na lugha yake amngependa impe heshima kwa sababu lugha inamtambulisha mtu na mila zake hivyo nawakaribisha watu wote kuja kushiriki kuienzi siku hii.”