Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Darasani kunapaswa kuwa sehemu ya amani na kusoma:Guterres

Watoto wanachungulia dirishani wakiwa darasani
© UNESCO/Yayoi Segi-Vltchek
Watoto wanachungulia dirishani wakiwa darasani

Darasani kunapaswa kuwa sehemu ya amani na kusoma:Guterres

Utamaduni na Elimu

Elimu ni haki ya msingi ya binadamu na kichocheo muhimu cha kufikia amani na maendeleo endelevu, amesisitiza leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres  katika siku ya kimataifa ya kulinda elimu dhidi ya mashambulizi.

"Kwa bahati mbaya, haki hii inaendelea kushambuliwa, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro," amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika taarifa yake ya kuadhimisha siku hiyo.

Quote: "Madarasa lazima yabaki kuwa mahali pa amani na kujifunza"-Antonio Guterres

Mashambulizi lazima yakome mara moja

Mwaka 2020 na 2021, muungano wa kimataifa wa kulinda elimu dhidi ya mashambulizi uliripoti zaidi ya mashambulizi 5,000 na visa vya matumizi ya kijeshi dhidi ya shule na vyuo vikuu.

Na zaidi ya wanafunzi na waelimishaji 9,000 waliuawa, kutekwa nyara, kukamatwa kiholela, au kujeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na wasichana.

"Mashambulizi haya yanawanyima mamilioni ya wanafunzi walio katika mazingira magumu fursa ya kupata elimu na kuongeza hatari ya unyanyasaji wa kijinsia ajira ya watoto na kutumbukizwa kwenye makundi yenye silaha. Ni lazima yakome mara moja,” ameendelea kusema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Tuungane kwa ajili elimu salama

Bwana Guterres amekaribisha hatua zilizochukuliwa na nchi nyingi kulinda taasisi za elimu na kuhimiza "Nchi zote wanachama kuidhinisha na kutekeleza azimio la shule salama".

Ameongeza kuwa “Sheria za kimataifa na majukumu ya sheria za kimataifa za kibinadamu lazima ziheshimiwe. Ni lazima tuhakikishe ufuatiliaji, kuchunguza mashambulizi yote na kuwawajibisha wahalifu.”

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa na kuelekea mkutano wa kubadilisha elimu, ambao utaitishwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York kuanzia tarehe 16 hadi 19 Septemba, amehimiza kila mtu "kuchukua hatua kwa pamoja ili kuhakikisha elimu salama kwa wote".

Kukuza uelewa

Baraza Kuu lilianzisha siku hiyo kwa kauli moja, likitoa wito kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) kutoa kuelimisha kuhusu madhila ya mamilioni ya watoto wanaoishi katika nchi zilizoathiriwa na migogoro.

Kwa azimio lake, Baraza Kuu lilithibitisha kuwa serikali zina jukumu la msingi la kutoa ulinzi na kuhakikisha elimu jumuishi na yenye usawa katika ngazi zote kwa wanafunzi wote hasa wale walio katika mazingira hatarishi.

Pia lisisitiza haja ya kuongeza juhudi na kuongeza ufadhili ili kukuza mazingira salama na usalama wa shule katika dharura za kibinadamu kwa kuchukua hatua zote zinazowezekana ili kulinda shule, wanafunzi na wafanyakazi wa elimu dhidi ya mashambulizi, kujiepusha na vitendo vinavyozuia watoto kupata elimu, na kuwezesha upatikanaji wa elimu katika mazingira ya vita.